Mungu ibariki Stars, Mungu ibariki Tanzania

23Mar 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mungu ibariki Stars, Mungu ibariki Tanzania

DUA na sala zote za Watanzania na hasa wapenda michezo kesho zitaelekezwa kukiombea kikosi cha Timu ya Soka ya Taifa maarufu Taifa Stars.

Kikosi hicho kinachoongozwa na Mnigeria, Emmanuel Amunike kesho kuanzia saa 12:00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kinatarajiwa kuwakaribisha wapinzani wao Uganda (Cranes).

Taifa Stars na Uganda zitakutana katika mechi ya mwisho ya Kundi L ya kuwania tiketi ya kufuzu fainali zijazo za Kombe la Afrika (AFCON 2019) ambazo zitafanyika Juni huko Misri.

Katika mechi ya kesho, Taifa Stars inayoongozwa na Nahodha Mbwana Samatta inahitaji matokeo ya ushindi tu ili iweze kutimiza ndoto zake za kucheza fainali hizo zinazochezwa kila baada ya miaka miwili.

Mara ya mwisho Taifa Stars kushiriki fainali hizo ilikuwa ni mwaka 1980, na nahodha wa kikosi hicho alikuwa ni Leodegar Tenga, ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Kikosi hicho kilichojaa wachezaji nyota wanaocheza nje ya Tanzania na hapa nyumbani, wote wako tayari kwa mchezo huo muhimu, lakini kinachohitajika ni kuendelea kuiombea timu yetu iweze kufanya kile ambacho wadau wa soka wanakisubiri.

Nipashe inaungana na wadau hao kuiombea dua njema Taifa Stars kwa sababu kufanya vema kwa timu hiyo, inamaana jina la Tanzania litaendelea kutajwa katika medani mbalimbali za kimataifa.

Tunaamini kuwa hakuna kisichowezekana kwa Taifa Stars kupata ushindi katika mechi ya kesho na hatimaye kuwapa furaha Watanzania ambao kwa muda mrefu walikuwa watazamaji kwenye fainali hizo zinazofanyika chini ya usimamizi wa CAF.

Kama ilipokwenda Kampala Septemba mwaka jana iliweza kupata pointi moja, hali ya kuwa wenyeji wote waliamini watapata ushindi katika mchezo huo, basi kesho nyota wa Taifa Stars mnatakiwa kuongeza bidii na hatimaye kupata ushindi katika uwanja wa nyumbani.

Lakini ili nyota au askari wetu ambao tunatarajia wapeperushe vema bendera ya Tanzania, ni nafasi yetu kwa Wazalendo kujitokeza kwa wingi kwenda kwenye Uwanja wa Taifa ili kuwashangilia.

Ili timu iweze kufanya vema katika mechi yake yoyote, ni lazima iwe na kikosi kamili chenye wachezaji 12. Wachezaji 11 wanakuwa uwanjani na mchezaji wa 12 ni wewe shabiki ambaye unatakiwa kufika na kukaa jukwaani kuishangilia timu yako.

Hakuna miujiza katika soka, ili Taifa Stars iweze kufanya vema katika mchezo wake wa kesho, sibudi kila mmoja wetu akatimiza jukumu lake na kuwa sehemu ya mafanikio ambayo yatapatikana baada ya kuifunga Uganda.

Hata hivyo, Nipashe linawakumbusha mashabiki wote kuhakikisha wanaingia kuishangilia timu yao kwa utulivu, bila kufanya vitendo vyovyote vya uhalifu au kuvunja amani.

Kwa kufanya hivyo, itaiweka Tanzania katika nafasi nzuri na kujiepusha na adhabu yoyote kutoka CAF au Fifa ambayo inasisitiza Fair Play katika mechi zote.

Nipashe linaendelea kuwakumbusha Watanzania kuiombea dua Taifa Stars ambayo inajukumu zito la kuhakikisha inashinda na kufuzu fainali hizo za mwaka huu wakati tayari wapinzani wao Uganda wameshafuzu na mchezo wa kesho wanakamilisha ratiba.

Mungu ibariki Taifa Stars, Mungu ibariki Tanzania. AFCON 2019 ni zamu yetu.

Habari Kubwa