Mvua zitoe funzo Dar kuboresha miundombinu

15Mar 2017
Mhariri
Nipashe
Mvua zitoe funzo Dar kuboresha miundombinu

MVUA zilizonyesha juzi katika Jiji la Dar es Salaam na kuharibu miundombinu ya barabara ni dalili za kuanza kwa msimu wa masika.

Mvua hiyo ilisababisha maeneo kadhaa ya jiji kufurika maji huku baadhi ya barabara zikifungwa kutokana na mawasiliano kati ya barabara moja na nyingine kukatika.

Mvua hiyo ilianza kunyesha majira ya asubuhi hadi saa sita mchana na kusababisha baadhi ya wafanyakazi kutumia muda mwingi barabarani kwenda kwenye shughuli zao na kurejea nyumbani kutokana na barabara nyingi kujaa maji.

Kwa mujibu wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, Manispaa ya Kinondoni ndiyo iliyoathirika zaidi kutokana na miundombinu yake kutokuwa imara.

Alisema athari kubwa zilijitokeza kwenye miundombinu kutokana na ujenzi holela na kwamba maeneo ya kupitishia maji yalizidiwa.

Maeneo kadhaa yaliripotiwa nyumba zake kujaa maji hasa ya Kawe, Barabara ya Bagamoyo hadi Mwenge likiwamo eneo la Samaki kujaa maji na kukata mawasiliano ya barabara inayotoka Goba.

Aidha, Barabara ya Bagamoyo ya zamani kupitia Kawe iliathirika kwa kujaa maji na Jeshi la Polisi kuifunga. Maeneo mengine ni barabara ya Mikocheni kupita kwa Mwalimu Nyerere na Barabara kutoka Hospitali ya Mwananyamala hadi Stendi ya Makumbusho.

Mengine ni Mwenge,Sinza, na Msasani, Jangwani, Kigogo na Bonde la Msimbazi na Tandale.

Chanzo cha hali hiyo ambayo wakati mwingine husababisha wananchi kadhaa kuhama nyumba zao kutokana na kuzingirwa na maji, ni ujenzi holela ambao unafanyika kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za mipango miji.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), kipindi cha msimu wa mvua za masika kimeanza, hivyo tutegemee changamoto ya kuharibika kwa miundombinu ya barabara, madaraja na baadhi ya nyumba za wakazi kuzingirwa na maji.

Ili kupunguza ukubwa wa changamoto hii au kuimaliza kabisa, ipo haja ya kuchukuliwa hatua mbalimbali.

Kwanza wananchi waheshimu maagizo yanayowakataza kujenga na kuishi katika maeneo hatarishi hususan ya mabondeni, kwa visingizio vya kutokuwa na uwezo wa kupata viwanja vya ujenzi.

Pili, kuna umuhimu wa kuzuia ujenzi wa majengo na kuta yanayojengwa katika mikondo ya maji kwa kuwa ni sababu kubwa inayochangia mafuriko.

Pia, walioko katika maeneo hayo waondoke mara moja kwa hiyari yao badala ya kusubiri mvua.

Kwa upande wake, mamlaka zetu hususan halmashauri zitimize wajibu wake wa kusimamia sheria na kuhakikisha kwamba suala la mipango miji linazingatiwa.

Halmashauri zinaweza kupunguza tatizo hili kwa kutumia sheria zilizoko kuzibomoa nyumba zinapoanza kujengwa katika maeneo hatarishi.

Kadhalika, halmashauri zinatakiwa kuhakikisha zinajenga mitaro mipya ya maji na kuikarabati mingine ili maji yapite kirahisi badala ya kwenda katika makazi ya watu.

Tunaamini kuwa zikichukuliwa hatua na kupatikana mafanikio kwenye suala la mpango miji ndilo litakalokuwa suluhisho la kudumu la mafuriko katika Jiji la Dar es Salaam ambalo ni tatizo kubwa sugu.

Tunasema ni tatizo kubwa na sugu kutokana na mara kadhaa kusababisha watu kupoteza makazi, uharibifu wa mali na vifo.

Itakumbukwa jinsi mvua ya mwaka 2012 ilivyosababisha vifo vya watu zaidi ya 40 sambamba na watu zaidi ya 5,000 kukosa makazi pamoja na uharibifu wa mali.

Habari Kubwa