Mwaka 2019 ulikuwa mzuri kwa Taifa Stars

30Dec 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mwaka 2019 ulikuwa mzuri kwa Taifa Stars

KWANZA kabisa tunapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha salama hadi siku ya leo.

Ikiwa imebakia siku moja ili kumaliza mwaka 2019, wadau wa soka nchini Tanzania hawataweza kuusahau kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia timu yake ya Taifa (Taifa Stars).

Timu hii ambayo wakati huo ilikuwa chini ya Mnigeria Emmanuel Amunike, ilionekana kama imekata tamaa ya kufanya vema katika safari ya kufuzu kushiriki katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2019), ambazo zilifanyika Juni mwaka huu nchini Misri.

Ni mwaka ambao Tanzania iliweka rekodi kubwa ya kushiriki fainali hizo ikiwa imepita miaka 39 tangu iliposhiriki kwa mara ya mwisho mwaka 1980, ikiongozwa na nahodha wake Leodegar Tenga, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

Hata kama Taifa Stars haikufanya vema katika fainali hizo ikiwa imepangwa kundi moja pamoja na mabingwa wa michuano hiyo Algeria, Senegal na majirani zao Harambee Stars ya Kenya, lakini kitendo cha kushiriki fainali hizo ni mafanikio.

Wapo wachezaji na makocha mbalimbali wamepita katika kikosi hicho cha Taifa Stars, ambao walishindwa kufikia hatua hiyo, lakini kwa mwaka huu, timu hiyo ilifaulu na kupeperusha bendera ya Tanzania pamoja na wimbo wake wa taifa kuimbwa kwenye fainali hizo.

Ikionekana kuwa na nafasi finyu baada ya kufungwa na Lesotho, ndio timu pekee iliyozoa pointi nyingi kutoka kwa Uganda (timu iliyoonekana) ngumu katika kundi lao wakati wa kusaka tiketi, ilianza kwa kuishangaza Uganda baada ya kutoka nao sare tasa jijini Kampala na kuipa kichapo cha bila huruma cha magoli 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Na katika kuthibitisha au kuonyesha Taifa Stars haikubahatisha katika kukiandaa kikosi chake, ikiwa bila nyota wake wanaocheza soka nje ya Tanzania, iliweza pia kukata tiketi ya kushiriki kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), fainali ambazo zitachezwa Aprili mwakani nchini Cameroon.

Kwa mara nyingine, Taifa Stars, ambayo sasa inanolewa na Kocha Mkuu Mrundi Etienne Ndayiragije, iliweza kuifunga Sudan nyumbani kwao na kukata tiketi ya kucheza CHAN kwa mara ya pili, mara ya mwisho Tanzania ilishiriki fainali hizo mwaka 2008.

Ili mafanikio haya yaweze kudumu, huu ni wakati wa kila mdau wa soka kushiriki kikamilifu katika kuifanya Taifa Stars iweze kuwa timu yenye ushindani na si kusindikiza timu nyingine.

Mafanikio ya timu hiyo yanaanzia katika ngazi za familia kwa kuwa wepesi kusaidia kuendelea vijana ambao mwisho wa siku, huvaa jezi ya Taifa Stars katika mashindano mbalimbali.

Huu ni wakati wa kutoa ushirikiano na kuwaunga mkono makocha na klabu zetu mbalimbali ili ziweze kutimiza malengo yao, kufanya kazi kwa weledi na kuacha kusubiri kusema viongozi hawafai pale Taifa Stars inapopata matokeo mabaya.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na serikali haiwezi kuipa matokeo chanya Taifa Stars, kama wadau wengine watajiweka pembeni wakati wa maandalizi.

Nipashe inakumbusha kuwa ni muhimu wadau wote wakashiriki kuanzia hatua ya maandalizi, ili mwisho wa siku, kama ni kucheza au kulia, iwe ni kwa pamoja.

Mwaka huu pia Tanzania iliweza kushiriki na kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wa umri chini ya miaka 17 (Afcon 2019).

Hii ni rekodi nyingine ambayo Watanzania tunatakiwa kujivunia, tunaamini nguvu ambazo zilitumika kufikia hapa, ziendelezwe ili mwaka ujao wa 2020 pia uwe wa mafanikio zaidi.

Katika mpira hakuna miujiza, endapo maandalizi sahihi yatafanyika, timu za Tanzania zitaendelea kufanya vema katika mashindano mbalimbali wanayoshiriki.

Habari Kubwa