Mwansasu amewapata wapi wachezaji Soka la Ufukweni?

14Aug 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Lete Raha
Mwansasu amewapata wapi wachezaji Soka la Ufukweni?

KOCHA wa Timu ya Taifa ya soka la Ufukweni, John Mwansasu, ametangaza kikosi cha wachezaji 16 watakaoingia kambini kujiandaa na mechi ya raundi ya kwanza dhidi ya Ivory Coast kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika Nigeria, utakaochezwa Agosti 26, mwaka huu.

Kikosi hicho kilichotangazwa juzi, kinaunda na Talib Ame, Ahamada, Mohammed Makame, Ahamed Rajab, Khamis Said na Yacob Mohamed wote kutoka Zanzibar, Ally Raby, Mwalimu Akida, Khalifa Mgaya, Rolland Revocatus, Juma Sultan, Rajab Ghana, Samuel Salonge, Kashiru Salum, Juma Juma na Kevin Baraka.

Mechi ya kwanza itafanyika Abidjan kati ya Agosti 26 na 27, wakati ile ya marudiano itafanyika Dar es Salaam kati ya Septemba 16-18, mwaka huu.

Timu nyingine zilizomo kwenye kinyang’anyiro hicho ni Cape Verde, Ghana, Misri, Liberia, Libya, Kenya, Madagascar, Morocco, Msumbiji, Senegal, Sudan na Uganda.

Ratiba ya mechi hizo inaonyesha kutakuwa na mechi moja moja tu za kuwania kufuzu na washindi saba wataungana na wenyeji Nigeria kwenye fainali hizo zinazotarajiwa kuanza Desemba 13 hadi 18, mwaka huu.

Timu zitakazoingia fainali ya michuano hiyo, zitaiwakilsha Afrika kwenye Kombe la Dunia la Fifa la Soka ya Ufukweni ambalo fainali zake zitafanyika Bahamas kuanzia Aprili 27 hadi Mei 7, mwakani.

Kwa mara ya kwanza, Tanzania ilishiriki michuano ya soka la ufukweni mwaka jana na kutolewa na Misri baada ya kufungwa nyumbani na ugenini.

Hata hivyo, wakati Mwansasu anataja kikosi cha kumenyana na Ivory Coast mwaka huu, Tanzania hakujafanyika mashindano yoyote ya mchezo huo na hakujawa na mkakati wowote wa kujipanga kushiriki kivitendo.

Mwaka jana, angalau kulilifanyika mashindano maalum ya kutafuta wachezaji wa kuunda timu hiyo, jambo ambalo kwa kiasi fulani lilionyesha dhamira kivitendo.

Imekuwa kawaida kwa baadhi ya timu zetu za taifa kushiriki michuano mbalimbali kwa kukurupupa jambo ambalo mwisho wa siku hulitia taifa aibu kubwa.

Ni wazi ratiba ya michuano hiyo haikutangazwa ghafla, na Shirikisho la Soka nchini (TFF), linatambua kalenda nzima za Fifa katika michuano mbalimbali, jambo ambalo linatufanya kuhoji kilipotoka kikosi hicho na matarajio yake kwenye kinyang'anyiro hicho.

Lete Raha kama mdau mkubwa wa michezo nchini, tunaishauri TFF kuwa na mkakati mzuri wa kuziandaa timu za taifa kulingana na kalenda ya Fifa kwa michuano husika na si kukurupuka kutangaza timu pasipo maandalizi yoyote.

Habari Kubwa