Nakumbushia ahadi ya pensheni kwa wazee wote

07Jan 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Nakumbushia ahadi ya pensheni kwa wazee wote

SERIKALI iliahidi kuwaenzi wazee wote wenye umri wa zaidi ya miaka 60 kwa kuwalipa pensheni ya Sh. 45,000 kwa mwezi kuanzia mwaka wa fedha 2011/2012.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda na kutangazwa na vyombo vya habari yakiwamo magazeti.

Wazee walifurahi jinsi serikali inavyowaandalia maisha bora uzeeni na wengine wakajawa na furaha iliyopitiliza na kuimba wimbo wa taifa na kuitukuza nchi.

Wakati ulipofika, wazee walikwenda kuuliza kwenye ofisi za vijiji, za kata na hata wilayani na za mkoa na kuambulia kuwa hakuna taarifa yoyote kuhusu malipo hayo.

Wakati wazee wakiendelea kufuatilia walichokuwa wameahidiwa mwaka wa fedha 2011/2012, serikali ikatangaza tena kupitia kwa Waziri wa Kazi na Ajira wa wakati huo, Gaudensia Kabaka, kwamba wazee wa miaka 60 na zaidi nchi nzima watalipwa pensheni kuanzia mwaka wa fedha 2013/2014.

Ahadi hii imezidi kuwaacha wazee solemba maana hakuna maelekezo kwamba watalipwa lini, kiasi gani wala na mamlaka zipi?

Baada ya wazee kuahidiwa mara mbili bila utekelezaji, serikali ikatangaza tena kwa mara ya tatu kupitia kwa Naibu Waziri wa Fedha, Dk. Ashatu Kajaji kwamba serikali itatenga bajeti maalum na itaanza kuwalipa pensheni wazee wa umri wa zaidi ya miaka 60 kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017.

Ahadi hii ilitangazwa na vyombo vya habari likiwamo gazeti la Nipashe la Februari 15, 2016. Hapa tena hakuna utaratibu uliotolewa kwamba ni wapi watalipwa na kiasi gani.

Pamoja na hayo, bado wazee wanayo imani kubwa kwa serikali yao na wanaiunga mkono kwa dhati; hivyo ili kudumisha hiyo imani ni vizuri kutimiza ahadi.

Ni imani yangu kwamba hilo likifanyika itakuwa ni faraja kubwa kwa wazee wasio na pensheni kwa sasa katika dhima nzima ya kujenga ustawi wao katika maisha ya uzee wao.

 

Samson Kissenge

Usangi, Mwanga

Maoni: 0784- 227 487

 

 

 

Habari Kubwa