NDC ina mpango mzuri kwa wakulima lakini…

03Jul 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
NDC ina mpango mzuri kwa wakulima lakini…

TANZANIA inaendelea kutegemea kilimo katika maendeleo ya uchumi wake. Sekta ya kilimo imekuwa tegemezi kutokana na kuongoza katika kuchangia kwenye pato la taifa tangu uhuru.

Tangu wakati huo asilimia kubwa ya Watanzania wameendelea kuishi vijijini na kutegemea kilimo katika kuendesha maisha yao. Kutokana na mchango huo mkubwa wa sekta ya kilimo, ndiyo maana ilianzishwa kaulimbiu ya ‘kilimo ni uti wa mgongo’.

Licha ya serikali kubuni na kuanza kutekeleza mpango wa kuipeleka nchi yetu kwenye uchumi wa kati kupitia ujenzi wa viwanda ifikapo mwaka 2025, bado kilimo kitaendelea kuwa sekta muhimu kwa kuwa kitategemewa kwa ajili ya kusapoti viwanda.

Tunasema hivyo kwa kuwa mazao yatakayozalishwa ndiyo yatakayotumika kwenye viwanda kama malighafi za kuzalisha bidhaa za viwandani.

Kutokana na umuhimu huo, bila shaka msukumo mkubwa utahitajika ili uzalishaji mashambani uongezeka mara dufu kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya malighafi za viwanda.

Kikubwa ambacho serikali ina wadau wa kilimo watatakiwa kufanya ni kupitia kwa umakini changamoto zote ambazo zimekuwa zikiwakabili wakulima na kuzipatia ufumbuzi ili kuwapa moyo na morali wakulima wazalishe zaidi.

Kadhalika, suala la motisha kwa wakulima haliwezi kuepukika kama kweli kama taifa timedhamiria kwa dhati kuboresha kilimo chetu kiwe cha kisasa na chenye tija.

Wakati taifa likiwa njiani kuelekea kwenye uchumi wa kati kupitia ujenzi wa viwanda, Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), limesema kuwa limelenga kuondoa jembe la mkono kwa wakulima kwa kuleta mradi wa kuunganisha na kusambaza matrekta nchini.

Shirika hilo linasema kwamba mradi huo ambao utawawezesha wakulima watakaofika katika Viwanja vya Maonyesho ya 43 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) kupata trekta kwa mkopo kwa kutoa Sh. milioni tatu kama kianzio, kisha fedha zingine kulipa kidogo kidogo mpaka atakapomaliza deni.

Akizungumza juzi katika maonyesho hayo, Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Prof. Damian Gabagambi, alisema mradi huo ni mpango kati ya Tanzania na Poland wenye lengo la kuwasaidia wakulima kuwaondolea jembe la mkono.

Alisema matreka hayo hupatikana kwa mkulima kwa kutoa asilimia 25 ya fedha ya bei yake, lakini katika msimu huu wa Sabasaba wametoa ofa kwa wananchi kupata mkopo wa matrekta kwa masharti nafuu kwa kuanza kutoa Sh. milioni tatu.

Mpango huo wa NDC una lengo zuri la kuwawezesha, kuwajengea mazingira bora pamoja na kuwapa motisha wakulima ili wachangamkie kilimo cha kisasa na chenye tija.

Tunasema hivyo kutokana na uzalishaji wa wakulima wengi nchini kuwa duni kutokana na kutegemea kilimo cha jembe la mkono pamoja na kukosa mbinu za kisasa za uzalishaji.

Hata hivyo, shirika hilo lilitakiwa kwanza kutekeleza mradi huo kwa majaribio kwa lengo la kuelewa changamoto zake, ikiwamo uwezo wa wakulima kurejesha mikopo kwa wakati mwafaka.

Kilichotokea kwa mikopo ya matrekta aina ya power tiller iliyotolewa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kupitia Shirika lake la Uzalishaji Mali (Suma-JKT) kwa watu mbalimbali hususan vigogo, lakini wakashindwa kulipa deni hadi leo lilipaswa kuwa ni fundisho.

Kwa upande wa bei ya kununulia, inaweza kuonekana ndogo, lakini suala la kurejesha mkopo ni lingine, kutokana na changamoto zake hususan riba.

Kauli ya Prof. Gabagambi kuwa matrekta hayo yatakopeshwa kwa miaka miwili bila riba isipokuwa atakaposhindwa kulipa ndani ya muda huo, atalazimika kulipa kwa riba, linapaswa kuwa ni angalizo.