NEMC itilie mkazo elimu

02Nov 2017
Mhariri
Nipashe
NEMC itilie mkazo elimu

BARAZA la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ndilo lenye jukumu la kusimamia shughuli za utunzaji wa mazingira nchini chini ya sheria ya Utunzaji na Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004.

Chini ya sheria hiyo, baraza linawajibika kuhakikisha kuwa mazingira yanatunzwa ili kuwa na matumizi endelevu ya rasilimali, ustawi na maisha bora ya wananchi.

Aidha, chini ya sheria hiyo pia, NEMC ina wajibu wa kufanya ukaguzi wa mazingira na kutoa maelekezo mbalimbali yanayolenga kuboresha hali ya mazingira au kutoa makatazo mbalimbali ya kisheria yenye kudhibiti uchafuzi na uharibifu wa mazingira kutoka katika baadhi ya viwanda visivyozingatia sheria ya mazingira.

Ni kwa kutumia sheria hiyo ndiyo maana tunaona, kwa mfano, Mei 2 mwaka huu NEMC iliyatoza faini ya jumla ya Sh. milioni 20 mashamba ya mifugo ya Tommy na Ndoto mkoani Iringa kutokana na kulima mahindi na migomba ndani ya mita 60 kutoka ukingo wa Mto Ruaha mdogo au kufanya biashara bila kuwa na cheti cha tathmini ya hali ya mazingira kutoka NEMC.

Aidha, faini hizo zilikuwa na lengo la kunusuru ikolojia ya Mto Ruaha Mkuu ambao ni moja ya vyanzo vikubwa vya manufaa ya kiuchumi na kijamii nchini.

NEMC pia imetoza faini za mamilioni ya shilingi kwa viwanda vingi ambavyo imevikuta na hatia ya kwenda kinyume na sheria yake tangu ianzishwe miaka 13 iliyopita, na katika hali inayoonyesha kuwa Baraza hilo haliangalii 'sura', mkono wake umezifikia mpaka halmshauri za manispaa na miji.

Mwezi uliopita, kwa mfano, NEMC iliipiga faini ya Sh. milioni 25 Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam kutokana na kosa la uchafuzi wa mazingira.

Baraza hilo liliitoza faini Manispaa ya Ilala baada ya kupatikana na kosa la kutohudumia ipasavyo dampo la Pugu Kinyamwezi na hivyo kutoa harufu mbaya, vumbi na maji yenye sumu kali hivyo kuhatarisha afya ya wakazi wa maeneo jirani, viumbe hai na mazingira kwa ujumla.

Lakini faini hizi zina tija katika kufanikisha msingi wa kuanzishwa kwa NEMC - kuhakikisha kuwa mazingira yanatunzwa ili kuwa na matumizi endelevu ya rasilimali, ustawi na maisha bora ya wananchi?

Jibu la Nipashe ni hapana kwa sababu kuzuia ni bora kuliko kuponya, wahenga walisema, hata kama faini si uponyaji kutokana na udogo wa adhabu hiyo mpaka sasa.

Kwa bahati nzuri, kwamba adhabu kwa wachafuzi wa mazingira si dawa ya kukomesha uchafuzi, ndiyo pia mtazamo wa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Joseph Mallongo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Mallongo aliwaagiza wakaguzi wa mazingira wa NEMC kujielekeza ZAIDI katika kutoa elimu kwa umma ili ufahamu umuhimu wa kutunza na kuhifadhi mazingira.

Tunashauri, Nipashe, kwamba elimu ya uhifadhi wa mazingira ni muhimu kutolewa kwa umma ili ufahamu umuhimu wa utunzaji wa mazingira badala ya kujikita kutoa adhabu.

Tunashauri, Nipashe, kwamba elimu ya uhifadhi wa mazingira ni muhimu kutolewa kwa umma kwasababu kwanza, faini za NEMC ni ndogo kwa wachafuzi wa ngazi za wamiliki wa viwanda, na pia haziwezi kurejesha mazingira husika katika hali yake kabla ya uchafuzi.

Hivyo tuchukue fursa hii, Nipashe, kushauri NEMC kutilia mkazo elimu kwa wananchi kama ambavyo faida ya njia hiyo imeonekana katika nyanja ya ulipaji kodi stahiki kwa hiari, kwa jitihada za Kitengo cha Elimu na Huduma kwa Mlipakodi cha Mamlaka ya Mapato (TRA).

Habari Kubwa