Nguvu ya pamoja muhimu  kuepusha watoto Ukimwi

05Dec 2017
Mhariri
Nipashe
Nguvu ya pamoja muhimu  kuepusha watoto Ukimwi

RIPOTI mpya ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) imebainisha tishio kubwa ambalo kinaashiria kuangamiza maisha ya watoto ikiwa jitihada za pamoja hazitachukuliwa haraka iwezekanavyo.

Ripoti  hiyo ya kutisha iliyotolewa juzi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef), inabainisha  wazi kuhusiana na hatari hiyo kutokana na kuonyesha bayana kwamba watoto 18 duniani huambukizwa VVU kila baada ya saa moja.

Mkurugenzi wa shirika hilo anayeshughulikia masuala ya Ukimwi, Dk. Chewe Luo, akitoa ripoti hiyo jijini Dar es Salaam, alisema tishio la ugonjwa huo hatari duniani halijaisha, na kushauri kwamba inahitajika nguvu kubwa ya kupambana nalo.

Tafsiri ya ripoti hiyo ni kuwa watoto kwa sasa ndio walengwa wa maambukizi ya ugonjwa huo ambao hadi sasa haujapata tiba wala dawa, hivyo kuangamizi nguvukazi kubwa duniani sambamba na kuongeza mzigo wa umaskini kwa familia nyingi.

Tunakubaliana na kauli hiyo kuwa  idadi hiyo ya watoto wanaoambukizwa virusi vya ugonjwa huo ni kubwa, hivyo haipaswi kuvumiliwa na kuna haja kuunganisha nguvu za pamoja kupambana nao ili kuokoa maisha ya watoto.

Wakati  ripoti mpya ikionyesha tishio hilo lwa watoto, kundi la vijana nalo linatajwa kutokana na takwimu kuonyesha kuwa takriban watu milioni 37 duniani wanaishi na VVU na kati yao, vijana ni milioni 2.1 waliofikia hatua ya kubalehe.

Desemba Mosi mwaka huu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alisema kundi la vijana, hasa wasichana, limekuwa kwenye hatari kutokana na kuwa na ongezeko la maambukizi ya VVU.

Alieleza kuwa takwimu zinaonyesha kati ya vijana 10, wasichana wanane wana maambukizi ya VVU na wawili ni wanaume, na kwamba hali hii ni changamoto na kuongeza kuwa kundi lililo kwenye hatari hiyo ni la kuanzia umri wa miaka 15 hadi 24.

Kutokana na takwimu hizo kuonyesha hatari kubwa iliyo mbele ya vijana, Samia aliwaonya wasichama wanaofanya vitendo vya kuuza miili yao wabadilike. 

Tunawapa angalizo vijana hususan wanaojiingiza katika vitendo vya ukahaba na matumizi ya dawa za kulevya nao kuchukua hatua kwa kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyochochea maambukizi ya VVU. 

Tamaa ya fedha, mali na starehe visiwafanye vijana kujidanganya kuwa wakivipata vitawasaidia, la msingi wanapaswa kufahamu kuwa  matokeo yake ni kupata Ukimwi ambao hautawatesa peke yao bali familia zao na Taifa kwa ujumla.

Angalizo letu kuhusu maambukizi ya VVU  haliishii kwa vijana tu, bali pia kwa watu wazima kwa kuwa yamekuwapo matukio mbalimbali ya kuchangia maambukizu hayo ambayo yamekuwa yakiwahusisha.

Baadhi ya watu wazima wamekuwa wakitajwa kuwa hawazingatii maadili, hivyo kujihusisha na vitendo mbalimbali vikiwamo vya kufanya  ngono na wasichana wadogo.

Litakuwa jambo la maana ikiwa jamii itajenga tabia na mwamko wa kupima afya ili kama mtu atabainika kuambukizwa VVU apate ushauri nasaha na kutumia dawa za kufubaza virusi.

Elimu kwa umma kuhusu VVU na Ukimwi inapaswa pia kuwa endelevu badala ya kuridhishwa na tamwimu zinazoonyesha kupungua kwa maambukizi.

Tunaunga mkono hatua zilizochukuliwa na serikali kwa ushirikiano wa wadau na wananchi kwa ujumla zilizosababisha kupungua kwa  kiwango cha maambukizi kutoka nchini kutoka asilimia 5.1 mwaka 2011/2012 hadi kufikia asilimia 4.7 mwaka 2016/2017.

Tunasisitiza kuwa mafanikio hayo yasitufanye tubweteke, kwa kuwa Ukimwi bado upo kwa kiwango kikubwa na ni tishio.

Habari Kubwa