Nguvu ya ushirika urudi kuchochea maendeleo

05Jul 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Nguvu ya ushirika urudi kuchochea maendeleo

SERIKALI imewalaumu baadhi ya maofisa ushirika, taasisi za fedha, viongozi wa vyama vya ushirika na watendaji wao kwa kushirikiana kuwaibia wanachama kupitia mikopo na riba kubwa.

Lawama hizo zilitolewa na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha, wakati wa maadhimisho ya siku ya Ushirika Duniani (SUD).

Naibu Waziri huyo alisema wanawalimbikizia madeni makubwa yasiyolipika na kusababisha kuyumba au kufa kwa vyama vya ushirika.

Aliongeza kuwa imejengeka tabia miongoni mwa warajisi wasaidizi wa mikoa kutoa ukomo wa madeni bila kuzingatia utaratibu, na kwamba mtindo huo hufanywa kwa manufaa yao au kwa uzembe na hatimaye kuvitumbukiza vyama hivyo katika madeni makubwa.

Mbali na hujuma hiyo dhidi ya wanachama, alisema kutokana na vyama vingi kutofuata misingi ya ushirika, vimekumbwa na matatizo ya ukosefu wa mitaji, wizi na ubadhirifu.

Vyama vya ushirika nchini vimepoteza mwelekeo kutokana na idadi kubwa kufa na vilivyobakia vinaendelea kukabiliwa na hali ngumu kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo zilizobainishwa na Ole Nasha.

Sisi Nipashe tunauchukulia mtikisiko wa vyama vya ushirika kama ni kurudi nyuma kwa maendeleo, kwa kuzingatia kuwa vyama hivyo kabla na baada ya Uhuru ndivyo vilivyokuwa injini ya uchumi wa wakulima na taifa.

Tunasema hivyo kwa kuwa ni vyama hivyo vilivyowahamasisha wakulima kuzalisha mazao kwa wingi na ya viwango vya ubora hususani pamba na kahawa na kulipatia taifa fedha nyingi za kigeni sambamba na kuboresha uchumi wa wananchi wa maeneo yaliyokuwa yanazalisha mazao hayo.

Licha ya lengo kubwa la ushirika kuwa ni la uchumi, lakini pia viliwaunganisha watu na matokeo yake yalikuwa chanya kwani vilichangia kuleta maendeleo, umoja wa kitaifa na amani.

Vitendo vya wizi na ubadhirifu wa mali vilivyofanywa na baadhi ya watendaji, viongozi wa vyama hivyo pamoja na wanasiasa vilisababisha kuyumba kwa vyama hivyo vikiwamo Shirecu, Nyanza, KCU na KNCU, kwa kutaja baadhi.

Tatizo ni kwamba hadi sasa Serikali haijawachukulia hatua viongozi waliochangia hali hiyo, licha ya kutoa ahadi mara kadhaa kwamba watachukuliwa hatua zikiwamo kushtakiwa na kufilisiwa mali.

Hali ya vyama vya ushirika inasikitisha sana kwa kuwa wanachama wa vyama hivyo hawanufaiki na nguvu ya ushirika kwa sasa angalao inaonekana kuwa katika vyama vya kuweka na kukopa (Sacos) kutokana na kuwa tegemeo na kimbilio la watu wengi.

Kama serikali imedhamiria kuifanya Tanzania iwe ya uchumi wa kati kupitia ujenzi na ufufuaji wa viwanda, suala la kufufua ushirika halikwepeki kwa sababu wakulima kupitia vyama vyao vya ushirika watazalisha mazao kama malighafi yakiwamo kahawa, pamba, chai, ufuta, korosho na mengine kwa ajili ya viwanda hivyo.

Tunashauri kwamba kwa kuanzia, wale wote waliohusika kuvihujumu vyama vya ushirika wakachukuliwe hatua za kisheria ili liwe fundisho kwa wengine wakati taratibu nyingine zikiendelea.

Tunaamini pia kwamba baadhi ya changamoto zilizoko za wizi, ubadhirifu, kupungua imani ya wanachama kwa viongozi, mitaji midogo, kuchelewa kwa kesi za ushirika mahakamani zinaweza kupatiwa ufumbuzi kutokana na kutungwa kwa Sheria ya Ushirika namba 6 ya mwaka 2013 pamoja na kuanzishwa kwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika.

Ni matarajio yetu kwamba kuchukuliwa kwa hatua hizo na umakini wa Serikali, itawezekana kuwa na vyama vya ushirika imara na endelevu vyenye kukidhi mahitaji ya kiuchumi na kijamii.

www.guardian.co.tz/circulation

Habari Kubwa