Nguvu ziongezwe usimamizi, uendeshaji mamlaka za maji

21Apr 2017
Mhariri
Nipashe
Nguvu ziongezwe usimamizi, uendeshaji mamlaka za maji

WAKATI suala la upatikanaji wa majisafi na salama kwa watu wote likiwa ni miongoni mwa ajenda kuu katika mpango wa Maendeleo Endelevu (SDGs) ifikapo mwaka 2030, -

-Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad, amebaini udhaifu mkubwa katika usimamizi na uendeshwaji wa mamlaka za maji.

Katika ripoti yake ya 2015/16 iliyowasilishwa bungeni wiki iliyopita, CAG anasema amebaini udhaifu kwa Wizara ya Maji na Umwagiliaji na mamlaka hizo katika kuendesha miradi ya maji ikiwamo kutokusanya mabilioni ya fedha ada za watumiaji maji.

Sheria ya Usimamizi wa Vyanzo vya Maji ya Mwaka 2009 inazitaka mamlaka za maji kukusanya ada na tozo kutoka kwa watumiaji maji, lakini anasema ukaguzi umebaini miaka mitano ya fedha iliyopita, mamlaka zimeacha Sh. bilioni 5.039 mikononi mwa wateja huku zikikukusanya Sh. milioni 488 wakati Dawasco (Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam) pekee ina deni la Sh. milioni 869.

Kifungu cha 44(1) cha Sheria ya Usimamizi wa Vyanzo vya Maji ya Mwaka 2009 kinazitaka mamlaka za maji kuwekeza udhibiti kwa kutoa vibali kwa wachotaji wa maji, lakini ukaguzi umebaini kuna uchotwaji wa kiwango kikubwa cha maji kinachozidi vibali vilivyotolewa.

Mfano, Mamlaka ya Majisafi na Majitaka mjini Mwanza (Mwauwasa), CAG anasema ukaguzi umebani kiwango kinachochotwa na mamlaka hiyo kwa siku kwenye Ziwa Victoria ni zaidi ya ilichoidhinishiwa.

Wanatakiwa kuchota mita za ujazo 53,000 kwa siku, lakini wanachota mita 90,000, hivyo kuisababishia serikali hasara ya Sh. milioni 40.515 ambayo ingekusanywa kama ada ya matumizi ya maji yanayozidi kiwango walichoruhusiwa kwa mwaka.

Ipo pia changamoto ya ukaguzi kutokana na ukaguzi kubaini wahusika hawatekelezi jukumu hilo kutokana na ukosefu wa fedha kutokana na bajeti finyu (baadhi ya miaka ya fedha hawapangiwi fedha, umbali wa maeneo viliko vyanzo vya maji na uhaba wa watumishi.

Kutokana na changamoto hiyo, anasema ukaguzi wake umebaini kutumika kwa mashine na mabomba ya maji yasiyoruhusiwa kisheria.

Ukaguzi wa CAG katika mamlaka chache za maji umegundua madudu mengi, ambayo yanaonyesha kuwa ni kikwazo katika jitihaza za serikali kuhakikisha wananchi wote wa mijini na vijijini wanapata majisafi na salama kwa mujibu wa ajenda ya maendeleo endelevu ifikapo 2030.

Kubainika kwa kasoro hizo linapaswa kuwa ni fundisho kwa wizara husika pamoja na mamlaka za maji kwa kufanya marekebisho, ambayo yataongeza wigo katika ukusanyaji wa mapato yatokanayo na ada za maji. Makusanyo ya kutosha ya ada za maji ndiyo yanayopaswa kutumiwa na serikali kugharamia miradi mingine zaidi ya maji katika maeneo yenye uhaba nchini.

Tunashauri pia Wizara na mamlaka za maji watajipanga upya kwa kuweka taratibu zitakazodhibiti ipasavyo utolewaji wa vibali kwa uchotaji wa maji, lengo likiwa kuhakikisha wachotaji wa maji wanachota kiasi walichopangiwa.

Tunaamini kuwa udhibiti huo utasaidia wahitaji kupata kiasi cha maji wanachostahili ili wote wapate huduma hiyo.

Suala la kuwa na watumishi wa kutosha wa ukaguzi wa maji wenye vifaa na bajeti ya kutosha ni kitu muhimu katika uboreshaji wa huduma za mamlaka za maji.

Ni matarajio yetu kuwa Wizara na mamlaka za maji zitaweka mikakati zaidi na kuitekeleza kama ambavyo taasisi nyingine, ukiwamo Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) unavyochukua hatua ya ufuatiliaji kuhakikisha kuwa SDGs ajenda ya maji inapata mafanikio makubwa ifikapo 2030.

Habari Kubwa