Ni aibu CAG kukosa fedha

16Mar 2017
Mhariri
Nipashe
Ni aibu CAG kukosa fedha

TAARIFA kwamba Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi hadi sasa haijapewa fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli mbalimbali, hivyo kukwama, ni aibu.

Ni aibu kwa kuwa jukumu la msingi la ofisi hiyo ni kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa mapato na matumizi ya fedha za umma kisha kuweka taarifa hadharani.

Kwa hiyo kama haipewi fedha za kutosha na kwa wakati, maana yake ni kuwa hakuna shughuli zitakazofanyika za kudhibiti matumizi ya fedha za walipakodi.

Hayo yalibainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Juma Assad, juzi mjini Dodoma wakati wa mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa ofisi hiyo.

Alisema ofisi yake huhitaji Sh. bilioni 10 kwa ajili ya uendeshaji, lakini haijapata licha ya kupeleka maombi serikalini.

Kwa mujibu wa Profesa Assad, Sh. bilioni nane huhitajika kwa matumizi ya kawaida ya kila mwaka, ikiwamo kuwapeleka wakaguzi kwenye mafunzo ya ukaguzi ya kimataifa.

Alisema kutokana na kupatiwa fedha hizo hadi sasa, kazi zao za kila siku zimelala, ikiwamo kushindwa kuendelea na ujenzi wa ofisi zake katika mikoa kadhaa.

Kadhalika, ofisi hiyo imeshindwa hata kupeleka wakaguzi katika mafunzo ya ukaguzi wa kimataifa, kutokana na ukata huku akieleza faida za mafunzo hayo kwa wakaguzi kuwa ni kuepuka kudanganywa kila uchao kwa kuwa watakuwa na wakaguzi wa kimataifa kutoka nchini.

Tunakubaliana na kuunga mkono jitihada za serikali za kubana matumizi yake, lakini tunaona kuwa kutokana na umuhimu mkubwa wa Ofisi ya CAG, ipewe kipaumbele kwa kupewa bajeti ya kutosha na kwa wakati mwafaka ili itekeleze makukumu yake ya kila siku kwa tija na ufanisi.

Ukweli ni kwamba Ofisi ya CAG ina majukumu mengi kila siku lengo likiwa kutoa huduma bora za ukaguzi zenye kuleta tija kwa nia ya kuimarisha uwajibikaji ili kupata thamani ya fedha katika kukusanya na kutumia rasilimali za umma.

Ofisi hiyo imekuwa ikifanya ukaguzi wa taarifa za fedha kwa kipindi chote cha mwaka unaoishia kila Juni 30 katika taasisi za serikali zaidi ya 400 na mamlaka za Serikali za Mitaa hususani halmashauri 185 yakiwamo majiji 5, manispaa 21, miji 22 na wilaya 137.

Hii ni kazi kubwa na yenye changamoto kubwa inayohitaji rasilimali watu na fedha za kutosha, hivyo anachokisema Profesa Assad kina ukweli kwa asilimia 100.

Umuhimu wa ripoti ya CAG ulianza kuonekana kwa watu wengi katika miaka ya karibuni kuanzia uongozi wa Ludovick Utouh, kutokana na kubainisha madudu mengi ya kifisadi na matumizi mabaya ya fedha za umma. Ripoti hiyo ilichangia kuwang’oa mawaziri kadhaa mwaka 2012.

Mbali na ukaguzi wa CAG kuibua wizi wa fedha taslimu, lakini pia umekuwa ukitumika kubaini kama miradi ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa inatekelezwa kwa kutumia fedha halisi (value for money.

Kwa kuwa serikali ya Rais John Magufuli inajipambanua kwa kupambana na rushwa na ufisadi, haitakuwa sahihi kama itatekeleza majukumu yake bila kuipatia Ofisi ya CAG fedha za kutosha na kwa wakati. Bila hivyo itashindwa kumsaidia kufuatilia matumizi ya fedha za umma na matokeo yake ajenda ya serikali itakwama.

Sisi tunaona kwamba siyo vizuri CAG kulalamikia ukata hadharani, badala yake serikali iwapatie haraka fedha wanazozihitaji ili waanze kugharamia vitu ambavyo vina uhitaji wa haraka, vinginevyo itakuwa aibu kwa chombo hicho kukwama kutekeleza majukumu yake kutokana na ukata.

Habari Kubwa