Ni lazima kujilinda sikukuu zinavyokaribia

12Dec 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Ni lazima kujilinda sikukuu zinavyokaribia

HUU ni msimu wa sikukuu ambao kila mmoja anafikiria namna ya kujifurahisha, kuburudika na kuifanya familia yake ijisikie vizuri kwa wengine wakati wa Noeli na pia Mwaka Mpya.

Tunapenda kusisitiza kuwa jambo kubwa la kuzingatia wakati huu msimu wa sikukuu unavyokaribia ni usalama na ulinzi wa kila mmoja.

Ni muhimu wakati wote kuwalinda na kuwatunza watoto, wanyonge wakiwamo wahitaji, wazee na wagonjwa hasa wenye matatizo ya akili.

Tunayakumbusha haya kwa kurejea taarifa za Jeshi la Polisi zilizotolewa hivi karibuni kuwa kila siku watu wawili wanabakwa jijini Dar es Salaam.

Takwimu hizo zinazoihusu Kanda Maalum ya Dar es Salaam, zinasema ubakaji katika kipindi cha miezi 10 mwaka huu ni visa 719 ni habari mbaya.

Ulawiti umeongeza kutoka visa 259 mwaka jana na kufikia 319 mwaka huu, habari njema ni kupungua wizi wa watoto kutoka matukio 12 hadi saba.

Hata hivyo ni lazima kujilinda na kujiepusha na madhara yanayotokana na matukio ya uhalifu kama hayo. Japo haya ni baadhi yanayozungumzia ukatili wa kijinsia zipo ripoti nyingine kuhusu mauaji, utekaji wa watu na vipigo, ambazo hatukuzitaja.

Lengo letu ni kukumbushana kuhusu usalama wa watoto na pia ulinzi wetu na mali pia. Tukumbuke ni wakati ambao wazee na wengine wenye mahitaji maalumu wanapotea. Aidha, watoto nao wanapokwenda kwenye michezo wanaweza wasirejee.

Ni msimu huu wa sikukuu ndiko kwenye hatari hizo. Ni vyema kuwa makini na kuwajali watoto na ndugu wasiojiweza.

Lakini pia, ni msimu wa kupata taarifa za kuokotwa miili ikiwa imetupwa sehemu mbalimbali kwa madai ya ama kuuawa na kuporwa au kuchukuliwa baadhi ya viungo, kudaiwa kulewa kupindukia, kunyweshwa sumu na pia kuuliwa kwenye ugomvi.

Ni vyema kujiepusha na ugomvi. Tunakumbushana kuwa baadhi ya waathirika wakubwa wa mauaji ni madereva wa bodaboda na bajaji pamoja na teksi.

Wasijisahau msimu huu usafiri huhitajika sana, lakini hatari ya kuuawa nayo ni kubwa. Ni vyema kujiepusha na ulevi wa kupindukia na kuwakwepa watu wasiowafahamu au kuwatilia shaka.

Pamoja na kuwalinda watoto na wahitaji ni wakati pia wa wanawake kuwa makini na kujali usalama wao kwa vile nyakati za sikukuu ndiko yanakotokea mauaji ya wapenzi hasa kwa kisingizio cha wivu wa mapenzi.

Kwa upande wao tatizo la kuporwa huibuka kwa kasi kubwa, tena linawahusu wanawake na mabinti ambao mara nyingi ni wahanga wa kuibiwa pochi, mifuko na chochote wanachobeba hasa muda wa jioni na usiku.

Ni vyema kuwa makini na kujiepusha kupita maeneo yenye maficho kama vichaka, mapagare, mitaa yenye giza na kwenye sehemu zenye wahalifu hasa vijiwe vya wavuta bangi.

Tunashauri kuwa ulinzi wa mali za nyumbani pia ni jukumu la kila mmoja wakati huu. Ni vizuri kufanga milango na kutunza mifugo hasa kuku, ng’ombe, mbuzi na nguruwe kwa kuwa wengi huiba mali hizo nyakati za sikukuu ili kuuza kitoweo ambacho kinahitajika sana.

Ni vyema pia kukumbushana kuwa huu ndiyo msimu wa kuuziwa kitoweo cha wizi na pia kisicho salama kwani wakati mwingine nyama inaweza kuwa na sumu kutokana na wauzaji kuiba mifugo hasa nguruwe na kuwalisha sumu ili kuwakamata kwa urahisi.

Kwa hiyo ulinzi wa watoto, wasiojiweza, mali kuanzia mifugo na vyombo vya usafiri kama magari, pikipiki na bajaji ni muhimu kuzingatiwa muda wote ili kuepuka kumaliza na kuanza mwaka na majonzi.

Habari Kubwa