Ni miaka 20 kuendelea kutomwona Mwalimu

15Oct 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Ni miaka 20 kuendelea kutomwona Mwalimu

VONGOZI mashuhuri kama Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, kazi, maono na fikra zao haziwezi kufa, bali wanaendelea kuishi. Ndiyo maana shujaa Nyerere aliyevuta pumzi yake ya mwisho Oktoba 14, 1999, hata leo anaishi.

Viongozi kama hawa japo wamefariki dunia kile walichofanya kwa ajili ya mataifa yao kinaendelea kuimarika na kuwa bora kila siku na kila wakati.

Nyerere anaendelea kuishi kwa kuwa kazi zake alizozifanya kila wakati zinang’ara na kuimarika siku hadi siku licha ya kwamba hayupo tena.

Mathalani, vyuo vikuu alivyojenga kuanzia Dar es Salaam na Sokoine, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro na Dar es Salaam, Bandari za Dar na Tanga. Kazi hizo chache ni miongoni mwa mamia ya mambo aliyofanya Mwalimu Nyerere ambayo kila siku yanazidi kung’ara na kuwa mapya kila uchao.

Ndiyo maana tunasema kiongozi huyu mashuhuri na watendaji aliyefanyakazi zilizotukuka kama Nyerere na aliyekuwa anajiamini hafi na wala hasahauliki.

Kwa hiyo tutaendelea kusema Nyerere ni kiongozi mahiri, mwenye weledi, jasiri, rafiki wa Watanzania na Waafrika wote, imara na aliyeongoza kimkakati.

Kama taifa, tutaendelea kumwenzi Nyerere kwa kuwa ameyaongezea thamani maisha ya Watanzania kuanzia mwaka 1961 hadi 1999 akiwa mstari wa mbele kujenga shule, kulinda rasilimali, kuanzisha viwanda, kilimo cha kisasa, kujenga hospitali, barabara, kuanzisha miradi ya umeme na mashirika ya umma ili kuwahudumia Watanzania.

Yote hayo yameongeza thamani katika maisha ya kila mmoja ndiyo leo tunamwita shujaa na mpiganiaji maarufu wa haki za wananchi, amani, usawa na maendeleo.

Licha ya kwamba shujaa huyu alivuta pumzi yake ya mwisho Oktoba 1999 , hadi leo anaishi na ametuachia ujumbe unaotuhamasisha sisi na viongozi wote wa Afrika kumuiga kwa mambo mema na makuu aliyolifanyia taifa.

Watanzania licha ya kifo kututenganisha naye, hatuna kinachotufanya tusikitike kwani tuna hazina ya kazi zake na mambo makubwa aliyoyafanya yanayotufanya tutembee kifua mbele na kuringa kuwa kama taifa tuna zawadi kubwa ya kiongozi ambaye amezaliwa na kukulia katika ardhi yetu.

Nyerere ametuachia urithi (legacy) kwa taifa zima na Afrika. Tunajivunia Watanzania tunaye baba anayeheshimika kwa kazi kubwa za ndani na nje ya mipaka yetu.

Tunajivunia kuwa na kiongozi mwenye nidhamu ya hali ya juu aliyefanyakazi kwa bidii zote, asiyechoka kuwahudumia Watanzania na Afrika nzima.

Tunaposherehekea maisha yake tunaendelea kumuona Nyerere aliyekuwa na maadili na utaratibu wa kipekee katika kujenga nchi kwa misingi ya amani, uzalendo heshima na upendo ambavyo hadi sasa vinaendelea kuonekana na kusimamia kazi zake.

Tutaendelea kumuenzi Baba wa Taifa, kwa kuwa ndiye mbunifu na mchora ramani ya taifa letu tena ndiye sababu wa ushindi na mafanikio yote yanayoonekana Tanzania leo.

Tunamheshimu kwani ndiye aliyeweka misingi ambayo viongozi wengine wameisimamia na kuliwezesha taifa kusimama na kuendelea kuimba wimbo wa ushindi na maendeleo.

Tunapokumbuka kifo chake na kukumbuka maisha aliyoishi tunaendelea kumpongeza Nyerere kuwa alikuwa shujaa na kamanda mwaminifu ambaye hata siku moja hakukimbia mapambano ya kisiasa.

Alipigania kuwe na hali bora ya uchumi duniani, akigombana na mabeberu na wanyonyaji bila kuwajali au kuwaogopa pale alipoona wamekwenda kinyume na kuikandamiza Afrika. Ushujaa wake ndiyo tunaoutumia hadi sasa kuwa na misimamo ya kulinda na kutetea rasilimali zetu kama gesi, madini ardhi ili zitunufaishe na si kuwatajirisha mabeberu.

Tutaendelea kumkumbuka Nyerere.