Ni wakati mwafaka sasa wa kutafuta maridhiano bungeni

22Jun 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Ni wakati mwafaka sasa wa kutafuta maridhiano bungeni

MKUTANO wa Tatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ambao jukumu lake kubwa lilikuwa kujadili na kupitisha Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/17, umefanyika katika mazingira yenye mpasuko, kutokana na wabunge wa Upinzani kususia vikao vingi vilivyoongozwa na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson.

Wabunge wa Upinzani walitangaza kususia vikao vyote vinavyoongozwa na Dk. Ackson, wakisema kuwa hawana imani naye kutokana na anavyoendesha shughuli za Bunge. Kimsingi, wapinzani wanamtuhumu Dk. Ackson kuwa anawapuuza na kutetea maslahi ya Serikali bungeni.

Sababu hasa iliyosababisha kuibuka kwa madai hayo ni uamuzi wa Naibu Spika huyo kukataa kutoa fursa kwa Bunge zima kujadili kwa dharura tukio la Serikali kuwaamuru wanafunzi zaidi ya 7,000 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kuondoka chuoni hapo ndani ya sasa 24, kufuatia mgomo wa wahadhiri wao hivi karibuni.

Takribani zaidi ya wiki tatu sasa, wabunge hao wamekuwa wakitoka nje ya ukumbi wa Bunge pale Naibu Spika huyo anapoingia kuongoza shughuli za Bunge na kuacha mijadala yenye maslahi kwa wananchi na taifa ikiendelea.

Kibaya zaidi ni kwamba zimeanza kuonekana dalili za mpasuko zaidi na zenye viashiria vya kubaguana. Tunasema hivyo kutokana na kauli za wabunge wa Upinzani juzi kwamba wataweka msimamo wa kutosalimiana na kushirikiana na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hadi Bunge litakapoahirishwa Julai Mosi, mwaka huu.

Sisi Nipashe tumeshtushwa na kusikitishwa na mpasuko unaoendelea kuonekana ndani ya mhimili wa Bunge ambao una umuhimu mkubwa kwa nchi yetu kwani jukumu lake ni kusimamia utendaji wa Serikali, kutunga na kurekebisha sheria pamoja na wabunge kuwa mdomo wa kuwasemea wananchi waliowachagua kuwa wawakilishi wao.

Kila mwananchi angependa kujiwakilisha katika vikao vya kuamua mustakabali wake kama ilivyokuwa ikifanyika wakati wa demokrasia ya kale ya Ugiriki, lakini hilo haliwezekani tena katika demokrasia ya sasa kutokana na kuwako wawakilishi wao.

Kutokana na kukosekana kwa uvumilivu na maridhiano baina ya Naibu Spika na wabunge wa Upinzani, imekuwa vigumu kwa Watanzania waliowachagua wabunge waliosusia kunufaika kutokana na kero zao kutowasilishwa ili zijadiliwe na Serikali kuzitolea majibu wakati wa kuhitimisha mjadala wa bajeti juzi.

Wananchi katika maeneo yote ya nchi yetu wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kama za afya, elimu, maji, miundombinu, unaskini, mazingira na walitarajia kusikia wawakilishi wao wakizisema na Serikali kueleza imejipanga vipi kuzitafutia ufumbuzi katika mwaka 2016/17.

Hali iliyojitokeza bungeni kwa zaidi ya wiki tatu na Bajeti kupitishwa na wabunge wa upande mmoja imetoa picha mbaya ndani na nje, hivyo, njia pekee ya kurejesha maridhiano ndani ya chombo hicho haraka iwezekanavyo ni Bunge zima kukutana kujadili na kufikia maelewano kwa kutumia busara na kutanguliza mbele maslahi ya taifa.

Kuonyeshana ubabe kwa kutosalimiana, kutoshirikiana na matumizi ya kanuni haiwezi kuwa suluhisho la tatizo lililopo na ndiyo maana tunasisitiza kutumika kwa busara na maridhiano kwani hakutakuwa na mshindi wala aliyeshindwa.

Ni imani yetu kuwa wahusika wameliona hilo na watajitafakari na kuanza kusaka maridhiano mapema ili Bunge letu liendelee kuwa chombo chenye umoja na imara cha kutetea na kusimamia maslahi mapana ya taifa letu.

Habari Kubwa