Ni wakati mwafaka wakazi wa Kipunguni kulipwa fidia

04Jul 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Ni wakati mwafaka wakazi wa Kipunguni kulipwa fidia

SASA ni zaidi ya miaka 22 tangu Serikali ilipofanya tathmini ya kuwahamisha wakazi wa eneo la Kipunguni kupisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo ya Serikali imewaweka kwenye wakati mgumu wakazi wa eneo hilo, baada ya kushindwa kuwalipa kwa wakati fidia zao, huku ikiwa imeweka zuio la kutoendelezwa ikiwamo shughuli za ujenzi wa aina yoyote.

Tathmini ilifanywa mwaka 1997 wakati huo Serikali ilikuwa inaongozwa na Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, kisha alipokelewa kijiti na Rais Jakaya Kikwete mwaka 2005 -2015 alipompisha Rais John Magufuli.

Ni jambo linalosikitisha jinsi ambavyo wakazi hao wameishi miaka yote hiyo katika hali ya kuzuiliwa kufanya maendeleo kwenye makazi yao, pia kunyimwa kupata huduma muhimu ikiwamo kuunganishiwa mabomba ya maji.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, juzi alipohojiwa na Nipashe kuhusu fidia hiyo, alijibu kuwa ni suala linalopaswa kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Majibu ya Waziri yanazua maswali ikiwamo ni sheria ipi inayoelekeza malipo hayo yacheleweshwe kwa miaka yote hiyo, huku wananchi wakizuiliwa kuendeleza ujenzi katika maeneo ya makazi yao.

Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mei mwaka 2017, ilielieza Bunge kuwa imetenga Sh. bilioni 30 katika mwaka wa fedha 2017/2018 ili kukamilisha malipo ya fidia kwa wananchi wa Kipunguni wanaopisha upanuzi wa uwanja huo wa ndege.

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani, alilijulisha Bunge kuwa kutokana na gharama za fidia na uhaba wa fedha, Serikali imekuwa ikilipa fidia kwa wakazi hao kwa awamu.

Katika mwaka 2013/14 Serikali ililipa Sh. bilioni 1.2 ikiwa ni fidia kwa wakazi 59 kati ya wakazi 801 kwa eneo la Kipunguni ambapo wakazi 742 ndio hawajalipwa fidia zao.

Je, fedha hizo ambazo Serikali ilitangaza kuwalipa wakazi hao zilikwenda wapi hadi hawajalipwa? Na kama imekwama kuwalipa kwa nini isiwaruhusu waendelee kufanya shughuli za maendeleo?

Ajabu katika jambo hili ni kwamba pamoja na wakazi hao kukwamisha kufanya shughuli za maendeleo katika maeneo hayo, wamelalamika kuwa pia hawajapewa leseni za makazi hivyo wanashindwa hata kupata mikopo ya kuwawezesha wajikwamue kiuchumi.

Serikali ya awamu ya tano tayari imefanya mambo mengi ya maendeleo chini ya uongozi wa Rais Magufuli, tunaamini kwamba sasa itaona umuhimu wa kuhakikisha ahadi ya kulipwa kwa fidia kwa wakati wa eneo la Kipunguni inatekelezwa.

Kadhalika, serikali ya sasa imekuwa ikisisitiza kuwa lazima viongozi wahakikishe wanashughulikia na kutafutia ufumbuzi kero mbalimbali zinazowakabili wanyonge, hivyo tunaamini kuwa wahusika hususan wizara watamaliza suala hilo haraka.

Wakazi hawa wamekuwa ni watulivu ndani ya maumivu mengi ikiwamo kushuhudia maeneo ya wenzao yakistawi kwa maendeleo wakati katika maeneo yao nyumba zina mwonekano wa kuchakaa ikiwamo mabati kujaa kutu. Pia wengine wamekufa wakiwa wanasubiri utekelezaji wa ahadi hiyo.

Tunaamini kuwa hatua ya kuwalipa fidia yao ikitekelezwa itawafanya nao waweze kujiendeleza kiuchumi hivyo kujiletea maendeleo kwenye familia zao, mkoa na taifa kwa ujumla.

Kadhalika, ufumbuzi huo utawaondolea usumbufu viongozi mbalimbali wakiwamo wawakilishi wa wananchi, ambao kila uchao wamekuwa wakihangaikia suala hilo.