Nidhamu iboreshwe kwa wachezaji nchini

15Jul 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Nidhamu iboreshwe kwa wachezaji nchini

WAKATI tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), likiwa limeshatangaza kuwa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara utafanyika kuanzia Agosti 23, mwaka huu, klabu zinatakiwa pia ziwaandae wachezaji wao kujitambua.

Ligi hiyo ndiyo inayotoa mwakilishi wa Tanzania Bara katika mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Kwa mara nyingine tena, msimu ujao, ligi hiyo inatarajiwa kushirikisha timu 20, ambazo zitacheza mechi 38 kila mmoja, kwa maana ya mfumo wa nyumbani na ugenini.

Klabu zimekuwa zikiwaandaa zaidi wachezaji wake katika kujiimarisha ndani ya uwanja, ili ziweze kuvuna matokeo mazuri kwenye mechi zote wanazocheza.

Lakini, klabu nyingine zimekuwa zikisahau kuwajenga wachezaji wake kisaikolojia, na hapa ndipo "haiba" ya mchezaji huonekana anapokuwa ndani na nje ya uwanja.

Nipashe zinawakumbusha viongozi wa klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara na zile za Ligi Daraja la Kwanza, kuwapa wachezaji wao, mafunzo maalumu ya kujitambua, ambayo pia yatachangia uwezo wa nyota hao wanapokuwa uwanjani.

Tumeshuhudia wachezaji mbalimbali wenye vipaji, wakishindwa kufanya vema na baadhi yao kuacha kuendelea kucheza kandanda kwa sababu ya kujiunga kwenye makundi ambayo si mazuri katika kukuza na kuimarisha taaluma zao.

Wachezaji wanapokosa mwongozo sahihi, vipaji vyao hupokea na hapo hupelekea klabu iliyomsajili inashindwa kufikia malengo yake na baadhi hushuka daraja wakati nyingine hushindwa kuendelea na ligi au mashindano ambayo ilikuwa inashiriki.

Jukumu hili lisiachwe kwa klabu peke yake, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa kushirikiana na TFF, wanaweza kuandaa madarasa maalumu kwa ajili ya kuwaongezea uelewa wachezaji, kwa sababu zinafahamu uwezo halisi wa vilabu vyake.

Tunaamini kuwa, kwa kufanya hivi, sio tu, Ligi Kuu Tanzania Bara itakuwa yenye wachezaji wanaojitambua, pia serikali itakuwa imewaandaa wachezaji "waliokamilika" ambao wataitumikia Timu ya Taifa (Taifa Stars).

Ni ukweli kuwa, idadi kubwa ya wachezaji wanaounda Kikosi cha Taifa Stars wanatoka kwenye Ligi Kuu (ukiangalia takwimu za Kundi C kwenye Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon), Tanzania ilikuwa na wachezaji wa ndani 14, Kenya wachezaji 9, Algeria ilitoa nyota mmoja wakati Senegal yenyewe haikuwa na hata mchezaji mmoja anayecheza nyumbani, hivyo jitihada zinahitajika kuwaandaa vema wachezaji wanaoshiriki ligi hiyo.

Mafanikio yoyote yanahitaji uwekezaji uliokamilika, endapo wachezaji wanaoshiriki Ligi Kuu Bara wataandaliwa vema, tuna hakika Tanzania itakuwa na wachezaji wenye viwango vizuri ambavyo vitasaidia kuifanya Taifa Stars iwe na uwezo wa kushindana na si kushiriki kwenye mashindano mbalimbali ya kimataifa.

Kama tutabadilika na kuwekeza vema, Afcon ijayo Tanzania itakwenda ikiwa imara na yenye kuogopewa na timu za mataifa mengine.

Habari Kubwa