Ofisi za ardhi mikoani ukombozi kwa wengi

12May 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Ofisi za ardhi mikoani ukombozi kwa wengi

SERIKALI imetangaza fursa kwa wananchi, baada ya kusema kuwa ofisi za ardhi za mikoa zitaanza rasmi kufanya kazi katika mikoa 26 ya Tanzania Bara mwezi huu.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli kuitaka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuondoa kero na mzigo wa gharama kwa wananchi katika masuala ya ardhi.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni usogezaji wa huduma za sekta ya ardhi karibu na wananchi sambamba na kuwapunguzia gharama za kufuata huduma hiyo umbali mrefu, ambapo huduma za ardhi awali zilikuwa zikitolewa kwenye ofisi za Ardhi za Kanda na Makao Makuu.

Uamuzi huo ulitangazwa jijini Dodoma juzi na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, na kubainisha kuwa wizara imeanzisha ofisi za ardhi katika kila mkoa ili kutoa huduma zote zilizokuwa zinatolewa kwenye ofisi za kanda au makao makuu.

Alisema, kuanzia sasa wananchi watapata huduma zote katika mikoa yao, na kubainisha kuwa wananchi wa mikoa ya Kigoma na Katavi hawataenda tena Tabora kuchukua hati kama walivyokuwa wakifanya awali huku wale wa Tanga, Manyara na Arusha wakipata huduma katika mikoa yao badala ya kwenda Moshi na wale wa mikoa ya Iringa, Njombe, na Rukwa wakisalia mikoa husika badala ya kwenda Mbeya.

Kwa upande wa wananchi wa mikoa ya Ruvuma na Lindi, hawataenda mkoa wa Mtwara kupata huduma za ardhi na wananchi wa Kagera na Geita nao hawatalazimika kwenda Mwanza, huku wa mikoa ya Mara na Shinyanga wakisalia mikoa yao kupata huduma za ardhi, hivyo hawataenda Simiyu na wale wa Singida na Morogoro wakiepuka kwenda mkoa wa Dodoma kuchukua hati.

Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, nyaraka zote, watumishi pamoja na vitendea kazi tayari vipo mikoani na kubainisha kuwa sasa taasisi kama benki zitaweza kukopesha kwa kasi kwa kuwa dhamana za wakopeshwaji zipo mikoani na masijala za hati zimerudishwa kila mkoa.

Kwa kuzingatia usumbufu ambao wananchi walikuwa wakiupata kufuata huduma za masuala ya ardhi nje ya mikoa yao, zikiwamo gharama kubwa, tunaona kuwa hatua hii ya kuwasogezea huduma hizo katika mikoa yao ni ukombozi kwao.

Tunasema hivyo kwa kuwa wananchi wamekuwa wakitumia muda mtefu kusafiri kwenda katika kanda ambako ni mbali, hivyo kutumia gharama za usafiri pamoja na za chakula na malazi, kwa kuwa haiwezekani kwenda siku moja na kurudi.

Kwa hiyo serikali inahitaji pongezi kwa kulitafutia ufumbuzi suala hilo, ambalo limekuwa likiwatesa sana wananchi wengi, ambao uwezo wao kiuchumi ni mdogo.

Kadhalika, hatia hii inathibitisha kuwa serikali inazingatia kuwa masuala ya ardhi zikiwamo changamoto zinawagusa wananchi wengi, hivyo kuona umuhimu wa kuweka mazingira bora ya kutolea huduma husika.

Suala lingine ambalo tunaona kuwa wananchi wamepunguziwa mzigo na usumbufu ni la utoaji wa hati, kutokana na Waziri Lukuvi kusema wasajili wa hati wa mikoa watatoa hati kwa wananchi kupitia ofisi za ardhi za wilaya badala ya wananchi kufuata hati kwenye kanda au mkoani, na kuongeza kuwa, vifaa vya upimaji vimenunuliwa na kusambazwa ofisi hizo za mikoa ili halmashauri za wilaya ziweze kuazima na kupima maeneo yao bila gharama za kuvikodisha.

Tunawapongeza viongozi na watendaji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kubadilika na kufanyakazi kwa bidii na ubunifu badala ya mtindo wa zamani wa kufanyakazi kwa mazoea, ambao ulichochea vitendo vya rushwa, ufisadi na kuwakosesha haki wananchi wengi.

Tunaamini kwa kuendeleza utendaji huu, mipango na mingi itatekelezwa, hivyo kuwawezesha Watanzania kunufaika na rasilimali hiyo muhimu kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Habari Kubwa