Oksijeni iongezwe haraka hospitalini

08Jul 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Oksijeni iongezwe haraka hospitalini

JUZI Hospitali ya Rufani ya Kanda Bugando, jijini Mwanza imesema inakabiliwa na uhaba wa mitungi 500 ya kuhifadhia oksijeni kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wenye matatizo ya upumuaji, wakiwamo wa corona.

Hospitali hiyo ina mitungi 100 inayotumika kwa siku, huku mahitaji ya mitungi 300 na kuwaomba wadau kutoa msaada ili ipatikane mitungi 500 inayotosheleza mahitaji kwa idadi ya wagonjwa hospitalini hapo.

Alisema idadi ya wagonjwa wanaofika hospitalini wanaohitaji mitungi ya oksijeni ni wengi, na kwamba mahitaji yanaongezeka, huku ikiuzwa ghali na kushauri kuwapo kwa wazalishaji wengi na uzalishaji kwa wingi ili ishuke bei na kuwezesha upatikanaji wake kwa urahisi.

Kwa sasa serikali imethibitisha kuwapo kwa wimbi la tatu la corona, na kwa mujibu wa Rais Samia Suluhu Hassan, kuna wagonjwa kama 100 na kati yake 70 walikuwa wanapumulia mashine, na kwa sasa tahadhari inachukuliwa ikiwamo kuhakikisha uvaaji wa barakoa kila wanapokuwa kwenye mikusanyiko.

Jana Rais Samia akiwa Kibaigwa mkoani Dodoma kwenye ziara ya kikazi, aliwataka wananchi kuchukua tahadhari zote muhimu kwa kuwa wimbi la tatu la corona lipo nchini na hata Dodoma lipo, ambalo ni hatari zaidi, jambo ambalo linadhihirisha zinahitajika tijihada za mtu mmoja mmoja, jamii na mamlaka kutoa elimu kwa umma ili kutoa tahadhari.

Hii ni hospitali moja katika ya nyingi zilizopo nchini, ambayo imeeleza wazi uhaba wa mitungi hiyo, hivyo nidhahiri kuwa kutokana na kuthibitika kuwapo kwa corona, idadi ya wanaohitaji kutumia oksijeni inaweza kuongezeka, jambo ambalo linahitaji hatua kuhakikisha inapatikana.

Tunaamini serikali ikijipanga vyema na wadau wengine itakuwa rahisi kukabili wimbi hili na madhara hayatakuwa makubwa kama ilivyotokea kwenye nchi nyingi. Wale waliojiandaa mapema walifanikiwa kukabili wimbi hilo kiasi cha kutoleta madhara, na wapo ambao wameshaacha kuvaa barakoa.

Tunaamini serikali na wadau wa afya wamesikia kilio cha hospitali hiyo, za rufani, teule, za mikoa, wilaya, vituo vya afya na zahanati, ili kusaidia kuboresha huduma za afya, hasa kwa wakati huu, na pale inapowezekana kuwa na mitungi ya oksijeni iwepo ya kutosha.

Hili ni muhimu kutokana na ukweli kuwa tunaona kwenye nchi za Uganda, Zambia na Afrika Kusini ambako zimezidiwa na corona kiasi cha hospitali kuzidiwa na oksijeni kutotosha mahitaji, hivyo kusababisha wengi kupoteza maisha wakati ingewezekana kwa kupata huduma sahihi za afya.

Ni muhimu mamlaka husika hasa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kushirikiana na wadau wa sekta binafsi kuchangia mitungi hiyo na kuhakikisha inasambazwa kwenye hospitali zote za serikali au zinazoendeshwa kwa ubia kati ya serikali na taasisi za dini.

Hii ni namna mojawapo ya kujipanga kukabiliana na kusambaa ikiwamo kuokoa maisha ya wananchi ambao watahitaji huduma hiyo kwa ukaribu zaidi, isisubiriwe hospitali zikishaelemewa wagonjwa ndipo mitungi hiyo iongezwe.

Tunaona ni muhimu serikali ikawa inatoa takwimu za hali ya ugonjwa huo ikiwa njia ya kuwafanya wananchi kuona ni hatari, kwa kuwa kwa sasa watu wanakwenda kwenye mikusanyiko bila kuchukua tahadhari, na hilo linaonekana kwenye masoko, sherehe, maeneo ya biashara na nyumba za ibada.

Bila kuwa na mitungi ya kutosha kuna hatari ya ugonjwa huo kusambaa kwa kasi, na kupoteza watu muhimu, ambao maisha yao yangeokolewa, kwa kuwa kabla ya wimbi hilo kulikuwa na mahitaji ya mitungi hiyo, uwepo wa wimbi umeongeza mahitaji ambayo ni lazima kuangalia mwelekeo na kuboresha. Maandalizi ni muhimu ili kukabiliana na hali yoyote inayoweza kujitokeza.

Habari Kubwa