Ondoeni upungufu huu kuhusu corona

20May 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Ondoeni upungufu huu kuhusu corona

KIASI corona inavyopamba moto, inazidi kuwachanganya watu wengi na ndivyo wanavyohitaji kufahamu zaidi kuhusu maradhi haya kutokana na kuwapo na maelezo mengi yanayohusu ugonjwa huo.

Hii ni kutokana na ukweli kuwa maradhi haya ni mapya na hakuna utafiti wa kutosha kuhusu ugonjwa huo ambao licha ya kusababisha vifo kwa muda mfupi unaleta hofu.

Watu wengi wanakuwa na wakati mgumu kutokana na maelezo mengi yanayotolewa na vyanzo mbalimbali kuhusu dalili za corona, wakieleza kuwa zilizoonekana Italia, China au Marekani sizo zinazojitokeza Afrika.

Kuna maneno kuwa corona ya Afrika haina dalili kama kukohoa, mafua, homa, kukosa pumzi, vichomi na kubanwa mbavu.

Madai ya sasa ni kwamba ugonjwa huo hauna dalili kama hizo badala yake kinachotokea ni mtu anapopata corona huishiwa nguvu, kukosa pumzi, kulegea, kuanguka ghafla na kufa.

Ukweli ni kwamba watu wengi wana taarifa ambazo si sahihi ama ni za kuhofisha kuhusu maradhi hayo na tunachoweza kusema ni kwamba corona ina dalili nyingi na huenda hakuna tofauti na zile zilizoripotiwa Italia, China au Urusi.

Wataalamu wanaeleza kuwa dalili ni nyingi na mojawapo ni kupoteza uwezo wa kutambua harufu na ladha. Pua hushindwa kutambua harufu iwe kali, mbaya au nzuri.

Aidha, ulimi hauwezi kugundua ladha za vitu kama sukari, chumvi, soda, ndimu na mengineyo.

Kuna dalili nyingine kama kupooza mwili mzima kunakotokana na virusi vya COVID- 19 kutengeneza vibonge vya damu vinavyokwamisha damu kusafiri ndani ya mishipa midogo.

Aidha, wataalamu hasa Italia ambao wamefanya utafiti zaidi kwa wagonjwa na hata kuchunguza miili wanaeleza kuwa kuumwa tumbo ghafla, kutapika na kuharisha ni dalili ya corona pia.

Wanaeleza kuwa kuumwa huko kunatokana na mishipa midogo inayosafirisha damu, hewa na chakula kushambuliwa na virusi na kusababisha damu kuganda kutokana na kutengeneza vibonge vidogo vidogo vinavyozuia usafirishaji wa damu tumboni. Yote haya si mapya ni dalili zinazotokea pote duniani.

Suala la kuvaa barakoa nalo lipewa umuhimu kwani inavyoelekea watu hawafahamu sababu za kuzivaa.

Kwa kutumia uzoefu wa mataifa mengine yaliyoathirika hasa China wataalamu wanashauri kuzivaa ili kuzuia maji maji kutoka kwa mtu mwingine akiwamo muathirika zisiwafikie wengine iwapo anaongea, kupiga chafya, miayu na kukohoa.

Barakoa humkinga mtu mwingine na mate au makamasi pamoja na hewa kutoka puani au mdomoni mwa mtu mwingine aliye jirani naye hivyo ni muhimu kuvaa barakoa na si kuzivua wakati unazungumza.

Tunaona kuwa pengine kuna haja ya kutoa elimu zaidi kwa wananchi kuhusu maradhi kuanzia kunawa mikono, kuvaa barakoa, dalili za ugonjwa huu ikiwamo kujibu maswali yanayoulizwa ili kuwapa uelewa wa kutosha.

Kwa hiyo, tunashauri kuwa ni vyema wataalamu wa afya wakatumia vyombo vya habari kuuelimisha umma kuhusu dalili nyingi zinazozungumzwa na kuwashauri hatua za kuchukua ili watu wasiishi kwa hofu bali wawe na uelewa na taarifa sahihi.

Pamoja na vyombo vya habari wataalamu wanaweza kutoa elimu kwenye vituo vya mabasi, kwenye daladala, lakini hata ndani ya magari.

Wanaweza pia kurekodi taarifa hizo na kuziweka kwenye vipaza sauti sehemu mbalimbali wanapofika watu wengi kuanzia hospitalini, vituo vya polisi, mabasi, makanisani, msikitini, kwenye maduka, vituo vya afya, kwenye saluni na kutumia redio za daladala, za jamii na mabasi ya masafa kutangaza ujumbe huo.

Habari Kubwa