Ongezeko la utalii lilete hamasa kuutangaza

30Jul 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Ongezeko la utalii lilete hamasa kuutangaza

ONGEZEKO la idadi ya watalii wanaoingia nchini kama ilivyotangazwa na serikali ni habari njema kutokana na kuongezeka kwa pato la ndani la taifa na kukua kwa sekta ya utalii.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na serikali, watalii wanaoingia nchini wameongezeka toka milioni 1.3 hadi milioni 1.5 katika kipindi cha mwaka 2017/18.

Ongezeko hilo limesaidia taifa kupata pato la ndani la Dola za Kimarekani bilioni 2.4 (Sh. trilioni 4.5).

Kuingia kwa wingi kwa watalii nchini kunatokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali na wadau wake kutangaza vivutio vya utalii wa Tanzania kupitia fursa mbalimbali wanazozipata wanapokuwa nje ya nchi na hata ndani ya nchi.

Tanzania imejaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii vinavyoweza kuwafanya watalii kujionea maajabu ambayo nchi nyingine duniani hayawezi kupatikana.

Siku za hivi karibuni Tanzania imeshuhudia watu maarufu mbalimbali wakiwamo wasanii wa filamu, marais wastaafu kutoka nchi kubwa duniani, wakija kushuhudia maajabu hayo kwa kujionea wenyewe badala ya kuangalia kwenye picha au sinema.

Utajiri wa vivutio vya utalii vilivyomo nchini umefanya hata nchi jirani kutumia ujanja na kuvitangaza ni vya kwao ili tu kuwavutia watalii waingie nchini mwao.

Fursa hii ya kipekee ya kuwa na wanyama, mimea, wadudu mbalimbali na vivutio vya kipee vilivyoumbwa na Mwenyezi Mungu, havina budi kutangazwa kwa nguvu zote ili mapato yanayotokana na utalii yaendelee kukua siku hadi siku.

Kwa mujibu wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Khamis Kigwangala, sekta ya utalii nchini inachangia asilimia 17.6 ya pato la taifa.

Utalii wa wanyamapori umeelezwa kuendelea kuwa kitovu cha kivutio na hivyo kuifanya sekta hiyo kuongoza kuchangia pato la taifa.

Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Adolf Mkenda, wakati akitoa taarifa ya takwimu za utalii ameeleza kuwa ukuaji wa watalii wanaoingia nchini ni mara mbili ya watalii wanaofanya utalii duniani.

Mwaka 2018, wizara hiyo kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Kamisheni ya Utalii ya Zanzibar na Idara ya Uhamiaji, ilifanya utafiti wa watalii wanaondoka nchini kwa lengo la kupata taarifa zitakazosaidia kuandaa akaunti za taifa na takwimu za mizania ya malipo ya nje.

Mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kwa asilimia 7.2 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 2.4 kutoka bilioni 2.3 zilizopatikana mwaka 2017.

Watalii waliokuja kwa ajili ya likizo na burudani walikuwa asilimia 62.6 na wameendelea kuwa na wastani mkubwa wa matumizi wa Dola 394.0 kwa siku.

Watanzania pia wamekuwa wakihamasishwa kujenga utamaduni wa kufanya utalii wa ndani kwa kutembelea mbuga za wanyama na vivutio mbalimbali vilivyomo nchini ili kujionea na kushawishi wengine kwenda.

Wageni kutoka nje wanajiwekea akiba hata kwa miaka miwili kwa lengo la kuja Tanzania kujionea vivutio, lakini Watanzania wenyewe wanashindwa hata kwa siku moja kutembelea vivutio hivyo.

Kwenda kujionea mwenyewe ni njia nzuri ya kuhamasisha mtu mwingine kwenda na kwa uhamasishaji huo utasaidia kuongeza mapato kwenye sekta ya utalii.

Inaelezwa kuwa watalii waliotembelea Tanzania walikaa kwa wastani wa siku 10 katika mwaka 2018,  waliokuja kutembelea ndugu na jamaa walikaa kwa wastani wa siku 11.

Katika juhudi za kuitangaza sekta ya utalii, serikali inatarajia kuongeza matangazo ili kuvutia zaidi watalii na kufikia idadi ya watalii milioni tano kwa mwaka.

Habari Kubwa