Poleni Polisi, ni wakati klabu kuungana

12Jul 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Poleni Polisi, ni wakati klabu kuungana

TASNIA ya michezo nchini ilipokea kwa mshtuko habari za ajali ya timu ya mpira wa miguu ya Polisi Tanzania siku ya Ijumaa.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Simon Maigwa ni kwamba ajali hiyo ya wachezaji wa Polisi Tanzania ilitokea saa tano asubuhi maeneo ya TPC Moshi wakitoka mazoezini.

Basi walilopanda likiwa na wachezaji 32, makocha na madaktari liligonga mti na kuacha njia, likisababisha wachezaji 16 kujeruhiwa, huku straika tegemeo wa klabu hiyo, Gerald Mdamu akivunjika miguu yote miwili.

Polisi Tanzania walikumbwa na janga hilo wakitokea mazoezi kujiandaa na mechi dhidi ya Kagera Sugar iliyotarajia kuchezwa Julai 14.

Nipashe linatoa pole kwa wachezaji, viongozi, benchi la ufundi, madaktari, ndugu na jamaa walioguswa na janga hilo, pamoja na Jeshi la Polisi kwa ujumla.

Tunaomba kwa Mungu awajalie wote waliopatwa na ajali afya njema, wapate nafuu, na hatimaye kupona, ili kurejea kwenye majukumu yao ya kawaida ya kazi zao.

Uzuri ni kwamba karibuni klabu zote za Ligi Kuu zimetuma salamu za pole na kuwatakia wapone haraka.

Klabu za Ligi Kuu na Daraja la Kwanza, Shirikisho la Soka na Bodi ya Ligi, zote zimeungana pamoja, zikionyesha kusikitishwa na wenzao kupatwa na janga hilo.

Hili limeonyesha upendo wa hali ya juu ambao haukudhaniwa kuwepo kwenye tasnia hiyo.

Wengi walidhani soka ni kama vita, kazi yao ni kupambana tu uwanjani na upinzani unabaki hivyo hivyo hata baada ya mechi kumalizika.

Nipashe tunaona kwamba, ajali hiyo imeonyesha umoja wa klabu zote za Tanzania. Zimeonyesha kuwa upinzani wao ni dakika 90 tu, lakini baada ya hapo wanabaki kuwa ni jamii ya soka na wote ni ndugu.

Tunaupongeza sana umoja huu ulioonyeshwa na klabu za Ligi Kuu na tunaamini hautaishia hapo.

Inawezekana umoja huu ukawa chachu ya kuundwa kitu ambacho kitazisaidia klabu na wachezaji kwa ujumla.

Ikumbukwe kuwa wachezaji wa klabu hizi wako kwenye mazingira ya hatari muda wote, wawapo ndani ya nje ya uwanja.

Wanachezaji wana mchezo wa hatari ambao unaweza kuwafanya wawe walemavu. Pia karibuni mwaka mzima wanasafiri, iwe kwenye ndege au gari.

Hivi vyote ni vyombo vya moto ambavyo havina dhamana kama tulivyoona kwenye ajali ya Polisi Tanzania.

Mfano ni mchezaji Gerald Mdami kwa sasa amevunjika miguu yote miwili. Bila kupindisha maneno ni kwamba anahitaji muda mrefu wa kukaa kabla ya kurejea tena uwanjani. Lakini anatakiwa yeye na familia yake waishi na kupata mahitaji.

Nipashe tunashauri kuwa ajali hii ya Polisi Tanzania na umoja huu ulioonyeshwa na klabu, utengeneze kitu ambacho kiwe kama mfuko wa maafa kwa ajili ya wachezaji, viongozi, benchi la ufundi, Maofisa Habari na hata madaktari waoambatana na timu ili kuweza kuwasaidia wanapopatwa na matatizo kama hayo.

Klabu zitengeneze utaratibu wa kukata asilimia fulani za pesa za viingilio ziingie kwenye mfuko huo kwa ajili ya kuwasaidia waathirika.

Habari Kubwa