Polisi iongeze nguvu kudhibiti uhalifu huu

07Jul 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Polisi iongeze nguvu kudhibiti uhalifu huu

JESHI la Polisi limetangaza kufanikiwa kunyamazisha ujambazi uliokuwa umeanza kuibuka kimya kimya kwenye maeneo mengi nchini, hii ni habari njema.

Na kwamba miji ya Dar es Salaam, Arusha na Mwanza iliyotishiwa na wimbi la ujambazi hivi karibuni iko salama baada ya operesheni ya kwanza kupambana na majambazi kufanikiwa kwa ufanisi.

Aidha, pamoja na taarifa hizo, polisi inawaonya wanaodhani kuwa kufanya ujambazi ni njia sahihi ya kujipatia kipato waache tabia hiyo.

Lakini, si majambazi pekee inatoa karipio kali kwa hata wale wanaotumia pikipiki kupora ikitaja matendo hayo kuwa ni makosa makubwa na anayekamatwa askari watamalizana naye kimya kimya na kutaka Watanzania kufanyakazi halali kupata kipato halali.

Hata hivyo, kauli ya serikali inakuja wakati kwenye maeneo mengi ujambazi na wizi mdogo mdogo ni kero kubwa. Uhalifu huo ukihusisha uporaji wa kutumia pikipiki ambao umerejea kwa kasi na inavyoelekea unahitaji nguvu na operesheni zaidi kupambana.

Wizi huo unawaibia watu pochi, mikoba na simu kwenye vituo vya daladala, barabarani, mitaani hasa kwenye uficho lakini hata ndani ya vyombo vya usafiri.

Malalamiko ni mengi yakiwamo ya wizi wa vioo vya magari na vifaa vingine hasa barabarani wakati wa foleni. Jambo hili linaashiria kuwa siyo wakati wa kujisifu kumaliza tatizo la ujambazi wakati wizi na udokozi unazidi kukithiri.

Mathalani, maeneo mengi ya Dar es Salaam watu wanalalamikia kuibiwa runinga ‘flat screen’ nondo za madirisha huvunjwa na TV pamoja na vitu vingine huibwa.

Hivi karibuni limetokea tukio eneo la Temeke waliingia nyumbani kwa mtu na kujaribu kuiba gari, lakini wahusika waliwashtukia mapema, huku matukio ya watu kuibiwa vifaa vya magari yakiongezeka kwa kasi.

Si hivyo tu kuna madai kuwa wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro, maeneo ya Kaseni, Kifula, Kisanjuni na Msangeni umeingia wizi mpya wa kuvunja madirisha kupuliza dawa za usingizi na kuiba vitu vya ndani kama TV, simu na mali nyingine za thamani.

Katika eneo hilo kumekuwa na matukio sita yaliyoripotiwa kutokea kwenye nyumba mbalimbali za wakazi wa eneo hilo.

Hivi karibuni, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, lilieleza kuhusu kukamata zaidi ya watuhumiwa 100 wa wizi wa vifaa vya magari na vyombo vya usafiri na kuonyesha vifaa vingi walivyodai vimeibwa maeneo mbalimbali.

Pamoja na hayo bado wizi unaripotiwa Tegeta, Salasala, Boko, Mikocheni na Tabata na kwa sasa ni kawaida mnapokuwa watu 10 kwenye kundi, watatu au wanne utawasikia wakieleza kuwa na matukio ya wizi kwenye nyumba zao yanatisha.

Tunaona kuwa siyo jambo jema kwa jeshi hilo kujisifu, ndiyo maana tunashauri mbinu zilizotumika kudhibiti hali hiyo kwa miaka iliyopita zitumike tena kuhakikisha matukio haya yanakuwa historia.

Tunaona kuwa ni wakati wa kuimarisha kikamilifu polisi jamii na kudhibiti uhalifu kwenye mitaa mbalimbali, ikiwamo kuwapa walinzi motisha, vitendea kazi pamoja na kuwatumia askari wa pikipiki, kufanya doria na hata ikibidi kura za kuwatambua wahalifu.

Pamoja na hayo ni vyema Watanzania wakakumbuka kuwa wajibu wa ulinzi wa nchi ni jukumu lao kikatiba na kushirikiana na polisi ambayo ni taasisi ya dola yenye wajibu wa kulinda raia na mali zao na kuwapa ushirikiano wa kufichua uhalifu.

Habari Kubwa