Polisi wazingatie weledi mikutano ya ndani kisiasa

18Jul 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Polisi wazingatie weledi mikutano ya ndani kisiasa

KWA muda mrefu vyama vya siasa nchini vimekuwa vikilalamikia mikutano yao ya ndani kuzuiwa na Jeshi la Polisi.

Viongozi wa vyama hivyo wamekuwa wakisema kuwa Jeshi la Polisi linazuia mikutano hiyo licha ya marufuku ya serikali ya kuzuia mikutano ya kisiasa kuhusu mikutano ya ndani.

Kutokana na hali hiyo, wadau mbalimbali wamekuwa wakieleza kutokuridhishwa na matukio ya mikutano ya ndani ya vyama vya upinzani kuzuiwa na Jeshi hilo na wakati mwingine kuisambaratisha na kuwakamata baadhi ya wahusika.

Mambo mengine ambayo yamekuwa yakihojiwa na kulalamikiwa ni chama tawala kufanya mikutano ya hadhara na ya ndani pamoja na baadhi ya viongozi wake kwenda kufanya mikutano nje ya maeneo yao kama katazo la mikutano ya kisiasa linavyoeleza bila kuchukuliwa hatua zozote.

 

Pengine baada ya kusikia malalamiko hayo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro, amelitolea ufafanuzi suala la mikutano ya kisiasa kwa kusema kuwa mikutano ya ndani haijapigwa marufuku kama inavyozungumzwa.

IGP Sirro alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na askari kwenye ziara yake ya kikazi mkoani Tabora, na kueleza kuwa mikutano hiyo inaweza kusitishwa tu pale itakapoonekana kwamba kuna viashiria vya uvunjifu wa amani.

Alisema kwamba licha ya mikutano hiyo kutopigwa marufuku,  ila kama kuna taarifa za tishio la usalama kwenye mkutano huo pokisi wanaweza kuzuia kwa faida ya Watanzania.

IGP Sirro alisema mikutano hiyo inaruhusiwa kunapokuwa na mazingira ya amani na kwamba wahusika wanachotakiwa kuzingatia ni kufuata sheria na taratibu zilizowekwa kila wakati.

Aliongeza kuwa Jeshi hilo linapokuwa limezuia mikutano ya ndani, watu wazingatie sheria na watii kwa sababu askari wanakuwa na taarifa zinazoweza kusababisha vurugu, hivyo  sasa tunawataka wahusika watii amri za polisi.

Alisema imekuwa kawaida kwa baadhi ya wanachama wa vyama vya upinzani kupiga kelele na kupinga hatua ya askari kuzuia mikutano ya ndani hali inayosababisha amani kutoweka kwenye eneo husika.

Hatupingi katazo la serikali la mikutano ya vyama vya siasa, lakini tunaona ni vizuri usimamizi wa katazo hilo ufanywa na Jeshi la Polisi kwa kuzingatia haki na usawa kwa vyama vyote.

Kadhalika, hatuungi mkono mikutano ya aina yoyote hata kama ni ya ndani kuwa na malengo ya kuvunja amani, hivyo tunavishauri vyama vya siasa kuheshimu na kufuata sheria za nchi.

Sirro amefanya jambo zuri kwa kutoa ufafanuzi wa kina kuhusiana na suala hilo ambalo kimsingi, limekuwa likizua mijadala na malalamiko miongoni mwa makundi ya jamii hususan vyama vya siasa.

Ni matarajio yetu kuwa Jeshi la Polisi litakuwa makini katika kusimamia mikutano ya vyama vya siasa iwe ya hadhara ambayo katazo hilo haivihusu hususan ile inayofanywa na viongozi wa kuchaguliwa katika maeneo yao kama wabunge na madiwani pamoja na ya ndani.

Utakumbukwa kuwa taifa letu linaelekea katika uchaguzi; wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani, hivyo ni wakati ambao Jeshi la polisi litapaswa kudhihirisha kuwa linatenda haki kwa makundi yote ya jamii pamoja na kutekeleza majukumu yake ya kusimamia haki kwa usawa, ufanisi na weledi.

Kwa kufanya hivyo, malalamiko yasiyo na msingi yatapungua, litaaminika kwa Watanzania wengi pamoja na jumuiya ya kimataifa.