Pongezi serikali kuruhusu mabadiliko mapya Simba

04Dec 2017
Mhariri
Nipashe
Pongezi serikali kuruhusu mabadiliko mapya Simba

KLABU ya Simba jana iliandika historia katika soka la Tanzania na Afrika Mashariki na Kati kwa ujumla, baada ya kuridhia rasmi kuanza mfumo mpya wa uendeshwaji wa klabu hiyo kwa njia ya hisa.

Mabadiliko hayo ya uendeshwaji wa klabu hiyo yametoa nafasi kwa ununuaji wa hisa za klabu hiyo na kuifanya timu kuendeshwa kikampuni zaidi.

Baada ya mchakato wa muda mrefu huku pia mvutano ukiwa mkubwa, hatimaye jana Kamati ya Zabuni ya klabu hiyo iliyokuwa imeundwa na kamati ya Utendaji ya Simba, ilimtangaza rasmi mshindi wa zabuni ya kununua hisa asilimia 50 za klabu hiyo.

Mfanyabiashara maarufu na mwanachama wa klabu hiyo, Mohamed Dewji "MO", ndiye aliyetangazwa mshindi  na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jaji mstaafu Thomas Mihayo.

Wakati mchakato huo ukiendelea, kulikuwapo na taarifa kuwa serikali imeingilia kati mchakato huo na kutoa maelekezo ambayo yalikuwa lazima Simba iyafuate ili kukamilisha mchakato huo.

Hata hivyo, katika mkutano wa juzi ambao mgeni rasmi Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe, aliwakilishwa na Msajili wa Vyama vya Soka na Klabu, Ibrahimu Mkwawa, alikanusha taarifa hizo.

Akisoma, hotuba ya Mwakyembe, Mkwawa, aliweka wazi kuwa serikali haina shida na mabadiliko ya klabu hiyo, huku ikifafanua kuwa jambo hilo lilipaswa kuigwa na klabu zingine.

Pamoja na kutoa maelekezo mengine, bado serikali ilionekana kuwa pamoja na klabu hiyo katika mabadiliko yake ambayo yalikuwa yakichagizwa na wanachama wa klabu hiyo.

Nipashe kama mdau mkubwa wa michezo nchini, tunaona serikali imefanya jambo la maana kuelezea mtazamo na msimamo wake juu ya mabadiliko ya Simba pamoja na klabu zingine zenye nia ya kufanya mabadiliko kama hayo.

Tunasema hivyo kutokana na kutambua kuwa mabadiliko yaliyofanywa na Simba na hata kama klabu zingine zitaiga utaratibu huo, ni wazi ni kwa sababu ya kutaka maendeleo kisoka na si vinginevyo.

Aidha, tunatambua kuwa Simba ilichelewa sana kufanya mabadiliko hayo, ambayo tunaamini kama yatatumiwa kwa dhamira ya dhati ya kuiletea maendeleo, muda si mrefu tutaishuhudia ikifika mbali na kuiletea Tanzania heshima kubwa kisoka kwa ngazi ya klabu.

Na ndio maana Nipashe tunaipongeza serikali kwa kuwa sehemu ya mabadiliko ya klabu ya Simba na klabu zingine zenye nia ya kubadili mfumo wao wa uendeshaji kama klabu hiyo ya mtaa wa Msimbazi jijini Dar es Salaam.

Kadhalika, tunaamini haitakuwa dhambi kwa klabu zingine kuiga mabadiliko haya ya Simba waliyoyafanya kwa ajili ya mustakabali wa maendeleo ya soka letu.

Kama ilivyoelezwa na serikali katika mkutano wa Simba wa jana, lazima kanuni ambazo zimeundwa katika kusimamia mabadiliko hayo ya uendeshwaji wa klabu za soka nchini ufuatwe kwa mustakabali wa soka letu.

Nipashe tunaipongeza Simba kwa nguvu yao ya pamoja kufanya mabadiliko hayo, lakini tunawasisitiza kusimama kwenye misingi na kufuata kanuni zote zilizowekwa na serikali katika kufanikisha mabadiliko hayo.

Habari Kubwa