Rais Magufuli, upinzani kukutana mwanzo mpya

05Mar 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Rais Magufuli, upinzani kukutana mwanzo mpya

RAIS John Magufuli juzi alikutana na kufanya mazungumzo na wanasiasa watatu; Maalim Seif Sharif Hamad, Prof. Ibrahimu Lipumba na James Mbatia, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Baada ya mazungumzo hayo, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye aliwahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alisema yeye na Rais Magufuli walizungumzia masuala ya kudumisha amani, usalama na upendo kwa watu wote.

Alisema amefurahishwa na dhamira ya Rais Magufuli kukutana na viongozi mbalimbali na kujadiliana mambo yenye maslahi kwa nchi.

Prof. Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), alimpongeza Rais Magufuli kwa ahadi yake kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu utakuwa huru na wa haki.

Mtaalamu huyo wa uchumi pia alipongeza juhudi zinazofanywa na serikali kupambana na rushwa, kudhibiti matumizi mabaya ya serikali, kulinda na kutumia vizuri rasilimali za taifa, kuboresha elimu na kuimarisha uchumi.

Alitoa wito kwa Watanzania wote kuweka uzalendo mbele na kudumisha amani na utawala bora.

Naye Mbatia, mbali na kufurahishwa na dhamira ya Rais Magufuli juu ya Uchaguzi Mkuu kuwa huru na wa haki, aliwataka wanasiasa waache kukamiana na kuchochea mambo hasi dhidi ya taifa, badala yake waungane kuendeleza mambo mazuri yanayofanywa na serikali ikiwamo kuboresha elimu, upatikanaji wa nishati na mengine yenye maslahi mapana kwa wananchi.

Mbatia alitoa wito kwa wanasiasa na Watanzania wote kwa ujumla kuweka mbele maslahi ya taifa badala ya kukumbatia mambo yenye maslahi binafsi.

Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa upinzani tangu aingine madarakani mwaka 2015.

Tunaipongeza hatua ya Rais ya kuanza kukutana na vyama vya siasa kwa ajili ya kusikiliza maoni yao pamoja na kushauriana kuhusiana na mambo mbalimbali ya nchi yetu yenye maslahi mapana ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Jambo la kutia moyo ni kuwa mazungumza hayo yamefanyika katika kipindi ambacho taifa letu linajiandaa kufanya uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwaka huu, hivyo ni kiashiria kwamba uchaguzi huo utafanyika katika mazingira rafiki, ambayo pande zote zinasikilizana na kushauriana.

Kauli zilizotolewa na viongozi hao watatu wa upinzani zinadhihirisha kuwa wanatanguliza mbele umoja wa kitaifa na maslahi mapana ya taifa letu.

Jambo walilolisisitiza la kuwapo kwa uchaguzi huru na haki lilishazungumziwa na Rais Magufuli alipokutana na mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa mwaka huu, hivyo kudhihirisha kuwa serikali imedhamiria kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika katika mazingira rafiki.

Tunashauri kwamba milango aliyoifungua Rais Magufuli iendelee kuwa wazi kwa viongozi wa vyama vingine vya siasa nchini kwa lengo la kuendeleza majadiliano na mashauriano yenye lengo la kuhakikisha kuwa uchaguzi wa mwaka huu unakuwa wa amani na salama.

Huu ni wakati kwa vyama vya siasa ambavyo vitapata fursa ya kukutana na Rais kwenda na ajenda ambazo zina lengo la kusukuma mbele maendeleo ya nchi yetu na watu wake.

Vinginevyo, tunasema kuwa hatia ya Rais ni mwanzo mpya, hivyo fursa ya kukutana naye itumiwe vizuri.

Habari Kubwa