Ratiba mpya Ligi Bara iwe kichocheo klabu kuchuana

09Sep 2017
Mhariri
Nipashe
Ratiba mpya Ligi Bara iwe kichocheo klabu kuchuana

PANGUA pangua ya ratiba ya mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara ni moja ya mambo ambayo yamekuwa yakipigiwa kelele na wadau wa soka hapa nchini.

Kelele hizo zinatokana na pangua hiyo mara kadhaa imeonekana kuzipendelea timu vigogo hapa nchini, Simba na Yanga ambazo viongozi wake wamekuwa wakitaka kuona zinapangiwa ratiba isiyowaumiza.

Pamoja na wapangaji ratiba kupanga mechi kwa kuzingatia jiografia ya nchi, lakini miaka ya nyuma ilionekana wazi kuzipa "unafuu" wa kuwa na siku za kusafiri na kupumzika kabla ya kucheza mechi inayofuata.

Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambaye pia ni mchezaji wa zamani na Mwenyekiti wa Chama cha Makocha Nchini (TAFCA), Wilfred Kidao aliunda kikosi kazi ambacho lengo lake lilikuwa ni kupanga ratiba mpya ambayo itazingatia kalenda ya mashindano ya kimataifa.

Ratiba ambayo itazingatia mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Shirikisho Afrika, Kalenda ya Fifa, Kombe la Mapinduzi na michuano ya Kombe la FA (maarufu Azam Confederation Cup).

Ukiiangalia ratiba hiyo utaona nafasi ya siku kati ya tano na nane kati ya mechi moja hadi nyingine, gazeti hili linaamini kuwa makocha watatumia vizuri nafasi hiyo kuandaa vyema timu zao na hatimaye kuonyesha viwango vinavyofanana na hadhi ya ligi.

Hii itasaidia kupata bingwa ambaye atatokana na kuwa na uwezo wa juu aliouonyesha kwenye mechi zote na kuvuna idadi kubwa ya pointi na si yule aliyefaidika kupata ushindi kwa kucheza na timu ambayo ilichelewa kufika kwenye kituo cha mchezo husika.

Kwa kutumia mwanya ambayo umetolewa kwenye ratiba hii mpya, ambayo pia inaweza kubainika kuwa na mapungufu machache, tunatarajia kuona kila timu ikionyesha kiwango cha juu kwa kupambana kwenye mechi za nyumbani na ugenini.

Imefika wakati mwenyeji akaonekana kweli ni mwenyeji kwa kuonyesha umuhimu wa kuwa kwenye uwanja wa nyumbani na mgeni akataabika kwa kushindwa kutawala kandanda.

Ifike wakati tuone timu inapokuwa nyumbani, inatawala kuanzia ndani hadi nje ya uwanja na hapo tunaamini timu itakayoibuka na ushindi ni ile ambayo itakayopambana kwa kuonyesha ubora uwanjani.

Mbali na kuzipa umuhimu mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, ambazo kila timu inayoshiriki ligi hiyo itacheza michezo 30, pia klabu hizo na zile za Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili na Mabingwa wa Mikoa wanatakiwa kujiandaa kupambana kwenye michuano ya Kombe la FA.

Michuano hiyo ni ya pili kwa ukubwa hapa nchini katika ngazi ya klabu kwa sababu inatoa mwakilishi wa Bara kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika huku Ligi Kuu ikitoa klabu inayopeperusha bendera ya nchi kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mbali na kutoa wawakilishi, ni sehemu nyingine ambayo wachezaji chipukizi na wenye vipaji huonekana huku wale ambao wako kwenye timu za Taifa wakipata nafasi ya kujiimarisha kwa kucheza mechi nyingi zaidi ukilinganisha na idadi ya michezo iliyokuwapo kabla ya kuanzishwa kombe hilo.

Nipashe inapenda kuwakumbusha wachezaji kuthamini kila aina ya mashindano kwa sababu kupitia michuano hiyo ndipo mawakala na viongozi wa timu hupata nafasi ya kusajili wachezaji na baadaye kuwa hazina ya nchi wanapoitwa kwenye vikosi vya timu za Taifa.

Habari Kubwa