Riba mikopo ziangaliwe, elimu iwe kipaumbele

10Sep 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Riba mikopo ziangaliwe, elimu iwe kipaumbele

JUZI Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, wakati akifungua Kongamano la la Wanawake na Biashara jijini humo lililoandaliwa na Benki ya Biashara Tanzania (TCB), alitaka kuwapo kwa ubunifu wa hali ya juu kama nyenzo mahususi ya kuwakomboa wanawake kifedha.

Alisema ubunifu utasaidia kuwafanya kuwa nguvu kubwa ya kiuchumi itakayokuwa chachu muhimu ya maendeleo nchini, na kwamba ni muhimu sana benki nchini zikafanya utafiti kujua ni kwanini wanawake wengi wanashindwa kuchukua na kurejesha mikopo ya benki.

Pamoja na jitihada za kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia mikopo mbalimbali, bado kuna changamoto nyingi ikiwamo za upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu kutoka kwenye taasisi za fedha.

Riba ni kilio cha muda mrefu kwa watu wengi na jitihada mbalimbali zimefanyika, ingawa bado hazijasaidia kupunguza ili kuwezesha watu kupata mikopo kwa ajili ya kuanzisha au kuimarisha biashara zao.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wanawake wamejikuta kwenye mikopo umiza ambayo inatolewa na taasisi binafsi au watu binafsi, kiasi cha kuwa maumivu makali kwa kuwa wanairejesha kwa riba kubwa na kwa muda mrefu kiasi cha kuwa ni mara mbili ya kile kinachostahili kulipwa.

Wanawake wengi wamejikuta wakikimbilia kwenye vikundi vidogo vidogo kama VIKOBA, baada ya kukopa benki, kwa kuwa riba zimakuwa maumivu.

Wito wa Mkuu wa Mkoa Mtaka umekuja kwa wakati sahihi kwamba ni muhimu benki zikaangalia suala hilo, na kuweka utaratibu wa kuwavutia wanawake wengi zaidi kupata mikopo kwa ajili ya kuwekeza, ambako kutakuwa na matokeo kwenye maisha yao binafsi na kuchangia uchumi wa nchi.

Hakuna ubishi kuwa mikopo husaidia kuwawezesha watu kupata fedha za kuanzisha biashara kubwa au uwekezaji mwingine, ambao husaidia kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Kuwapo kwa uwezekano mkubwa wa kupata mikopo ya uhakika kunafungua mwanga wa kukua kiuchumi kwa wanawake wengi, lakini ni muhimu kutanguliza elimu ya matumizi sahihi ya mikopo husika ili kuwawezesha kufikia malengo mahususi.

Baadhi ya benki zimeanzisha akaunti mbalimbali za kuyawezesha makundi ya wanawake, watoto na vijana ambazo kwa kiasi kikubwa zimesaidia kujiwekea akiba, lakini sasa ni muhimu kwa benki hizo kuangalia namna ya kuwa na wanawake wengi wanaokopa na kurejesha mikopo husika.

Tayari tunaona kuna ubunifu wa kuwa na VIKOBA kupitia benki, na baadhi ya vikundi kwa sasa vinaweka fedha benki kutokana na matakwa ya kisheria, lakini bado kuna changamoto nyingi katika kufanikisha hayo.

Pamoja na jitihada za benki, lakini kuna fedha asilimia 10 ya bajeti ya halmashauri inayopaswa kutengwa kwa ajili ya vikundi vya wanawake, vijana na walemavu kwa ajili ya kuanzisha biashara mbalimbali.

Halmashauri nyingi na hata kwenye Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), zimeeleza kuwa fedha nyingi zilitolewa, lakini hazikurejeshwa kama ilivyokusudiwa, hali hii inaonyesha kuwa bado kuna kazi kubwa ya kutoa elimu kabla ya kutoa mikopo.

Tunaamini kwamba elimu kwanza itasaidia kuwawezesha wakopaji kuwa na uelewa kuhusu matumizi ya fedha hizo pamoja na umuhimu wa kuzirejesha kwa wakati mwafaka kuepukana na kujikuta wakifilisiwa mali zao pamoja na athari nyingine.

Habari Kubwa