Riba za benki kilio cha muda mrefu, tuone marekebisho sasa

09Jul 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Riba za benki kilio cha muda mrefu, tuone marekebisho sasa

KILIO cha riba kubwa za mikopo inayotolewa na benki nchini ni cha muda mrefu kiasi cha wengi kushindwa kukopa, na kila kiongozi wa nchi aliyeingia madarakani aliliongelea na kuzitaka taasisi hizo kupunguza ili kuwezesha wananchi kukopa kwa ajili ya kutekeleza shughuli za maendeleo.

Kwa mara ya kwanza Rais wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete kipindi cha utawala wake alizungumzia suala hilo na kuzitaka benki kuangalia uwezekano wa kupunguza riba hizo ili kuwezesha watu wengi zaidi kukopa kwa ajili ya uwekezaji na maendeleo kwa ujumla.

Mafanikio yalikuwapo lakini ni kidogo sana na riba zilitofautiana kati ya benki moja hadi nyingine kwa kuwa wapo waliotoza hadi asilimia 22 na wengine asilimia 18, ambazo bado ziliendelea kuwa mzigo mzito kwa mkopaji.

Alipoingia Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli, alizungumzia suala hilo na mwaka 2018 Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ilipunguza riba ya kukopesha benki kutoka asilimia 16 hadi tisa, na iliahidi kushusha zaidi ili kuzifanya taasisi hizo kushusha riba na kuwezesha wananchi wengi wenye sifa kukopa kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Juzi Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, aliiagiza BoT kutekeleza haraka maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan, ya taasisi za fedha nchini kupunguza riba za mikopo.

Pia Naibu Gavana wa BoT, Dk. Bernard Kibesse, alimhakikishia waziri huyo kwamba wanakamilisha mazungumzo na benki washushe riba kama alivyoelekeza Rais Samia jijini Mwanza mwezi uliopita alivyozungumza na vijana.

Alikwenda mbali zaidi na kusema kuwa BoT inaendelea kurekebisha kanuni mbalimbali za mikopo inayotolewa na BoT kwa benki ili kuziongezea ukwasi na zenyewe zitumie fursa hiyo kushusha riba za mikopo.

Ikiwa jambo hili litatekelezwa ni wazi kuwa kutakuwa na manufaa kwa wananchi, taasisi za fedha na taifa kwa ujumla, kwa kuwa watakaochukua mikopo watawekeza na kuajiri, kuchangia GDP na kodi mbalimbali, lakini maendeleo yatazidi kustawi kutokana na shughuli za kiuchumi.

Pia benki zitaendelea kupata wateja wengi na faida, lakini serikali itaongeza idadi ya walipa kodi wakubwa, wa kati na wadogo, pia itapata kodi kutokana na shughuli za kiuchumi.

Kutokana na riba za benki kuwa juu wengi wamekimbilia kwenye vikundi kupata mikopo midogo, na baadhi Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS), ni muhimu riba hizi zikashuka kwa kuwa tunajua benki ndiyo zinaweza kutoa mikopo mikubwa kuanzia Sh. milioni 20 kuendelea.

Ikiwa riba zitakuwa rafiki maana yake wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani watakopa kwenye benki zetu na kuwekeza kwenye miradi au shughuli ambazo zitaajiri watu wengi, na kupunguza tatizo la ajira nchini ambalo linakuwa kwa kasi.

Ni wazi kuwa serikali haiwezi kuajiri kila Mtanzania bali kazi hiyo inafanywa pia na sekta binafsi ambayo ni injini ya ukuaji uchumi wa nchi yoyote duniani, na ndiyo imeajiri mamilioni ya watu na ili izidi kuchanua ni lazima kuiongezea nguvu kwa kupunguza riba za mikopo.

Wakati wa utawala wa Rais Kikwete alitambua umuhimu wa sekta binafsi na ndiyo maana alihakikisha anakuwa imara, kiasi cha kuajiri watu wengi na siyo kila mtu kukimbilia ajira za serikalini ambazo ni chache.

Ni matarajio yetu ahadi ya BoT itatekelezwa kwa vitendo na siku za hivi karibuni tunashuhudia benki zikitoza riba ndogo ambayo haitawaumiza wao wala wakopaji, na hilo litawezekana iwapo mamlaka ya usimamizi itawajibika kwa kufanya marekebisho ya kanuni zake.

Habari Kubwa