Ripoti ya CAG imeonyesha uhalisi

30Mar 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Ripoti ya CAG imeonyesha uhalisi

JUZI Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), aliweka hadharani baadhi ya madudu yaliyopo kwenye Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na mashirika ya umma kwa kuonyesha mchwa wanaoendelea kulitafuna taifa pamoja na hasara kubwa iliyopo.

Mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, CAG alibainisha kuna ubadhirifu wa zaidi ya Sh. bilioni 3.6 katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kujiendesha kwa hasara na mwaka jana pekee kupata hasara ya Sh. bilioni 60, na kwa miaka mitano likitengeneza hasara.

Aidha, alibainisha mchwa waliopo kwenye halmashauri nchini ikiwamo kushindwa kutumia mifumo sahihi ya Teknolojia ya Mawasiliano (TEHAMA), jambo lililosababisha mapato mengi kuzidi kupotea.

Pia ilionekana dosari kwenye mashirika ya umma ambayo hayafanyi vizuri kiasi cha kupata hati chafu, jambo lililomlazimu Rais Samia kumwagiza CAG kuweka wazi taasisi na mashirika husika ili hatua zaidi zichukuliwe.

Ripoti hizi ni za kitaalamu ambazo ofisi ya CAG inazifanyia kazi kwa uchunguzi wa kina, na zitawekwa bayana baada ya kuwasilishwa bungeni wiki hii na ndipo mbivu na mbichi zitajulikana, lakini juzi kwa uchache ilionekana picha halisi.

Zimekuwa zikiwasilishwa na kuonyesha madudu mengi ambayo yanahitaji wahusika kuwajibika moja kwa moja, ili kuokoa fedha za umma ambazo zingetumika kuboresha huduma za jamii kama afya, elimu na miundombinu.

Kati ya maneno yaliyoguswa na CAG lipo eneo la serikali za mitaa ambalo baadhi ya halmashauri zimepata hati chafu na ni tatizo linalojirudia mara kwa mara tangu utawala wa awamu ya tatu na awamu ya nne.

Halmashauri zinapokea fedha nyingi kutoka serikali kuu na kupitia shughuli zake mbalimbali, inagusa maisha ya wananchi moja kwa moja, huku kukiwa na uwakilishi wa moja kwa moja wa wananchi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Tayari Rais ameshatoa maelekezo ya kusimamishwa kazi kwa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, kupisha uchunguzi huku akimwagiza Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kuchukua hatua kwa ubadhirifu uliobainishwa na CAG.

Aidha, Waziri wa TAMISEMI ameagiza kuchukuliwa hatua kwa wakaguzi wa ndani na waweka hazina wa halmashauri nane zilizopata hati chafu, huku akipeleka majina ya wakurugenzi wa halmashauri hizo kwa rais ambaye ndiye mamlaka ya uteuzi.

Ni matumaini yetu kuwa ripoti hizo zitafanyiwa kazi na kutakuwa na uwajibikaji wa kina kwa kila aliyehusika kwa namna moja au nyingine kusababisha hasara kubwa.

Tunatarajia kuona uwajibikaji na kurudishwa kwa fedha za umma, lakini uhalisia kwenye mashirika ya umma ambayo kwa uendeshaji wake yamegeuka kuwa mchwa anayetafuna fedha za umma ambazo zingetumika kwenye miradi ya maendeleo inayogusa maisha ya watu moja kwa moja.

Watanzania wanataka kuona uwajibikaji, wanataka kuona fedha zao zinatumiwa ipasavyo kwa kuwa bado wana mahitaji ya msingi kama ya zahanati, vituo vya afya, vifaa tiba, dawa, miundombiu ya elimu na huduma za maji, ambazo huenda wamezikosa kutokana na kukosa fedha za kugharamia.

Habari Kubwa