Sakata kuishusha Kagera Sugar Bara liwe fundisho

01Jun 2019
Mhariri
DAR
Nipashe
Sakata kuishusha Kagera Sugar Bara liwe fundisho

KUFANYA kosa si kosa, ila kurudia kosa ndio kosa. Hayo ni baadhi ya maneno yaliyosemwa na wahenga na endapo jamii itayatumia vema, mambo yanaweza kwenda vizuri bila jambo lolote kuharibika.

Katika hali ya kushangaza, mara baada ya kumalizika kwa mechi za mwisho wa kufunga pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa mwaka 2018/19, kulitokea mkanganyiko kuhusiana na timu mbili ambazo zinatakiwa kushuka daraja moja kwa moja.

Mbali na timu zilizotakiwa kushuka daraja rasmi, pia ilitakiwa zifahamike klabu nyingine mbili ambazo zinatakiwa kucheza mechi za hatua ya mtoano maarufu play off ili kujua hatima yao, kama zinabaki kwenye ligi hiyo, au zinateremka kuelekea Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao.

Presha na mvurugano huo ulikuwa katika timu zilizokuwa mkiani, kwa sababu tayari kikosi cha Simba ambacho sasa kiko chini ya Mbelgiji, Patrick Aussems tayari kilikuwa kimeshafanikiwa kutetea taji hilo walilokuwa wanalishikilia.

Mbali na Simba, pia matokeo ya mechi za mwisho, yalikuwa hayaathiri nafasi ya pili ambayo ilishikwa na Yanga na ya tatu ambayo Azam FC walimaliza msimu wakiwa hapo.

Mvurugano na mahesabu yalikuwa yanaanzia katika nafasi ya 17, 18 na 19. Nafasi ya 19 ndio iliyoonekana kuvuruga watunza takwimu kwa kuonyesha tofauti.

Takwimu ambazo zilitolewa na wasimamizi wa ligi hiyo ambao ni Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) mara baada ya mechi zote kumalizika, zilibainika kuwa na makosa na kusababisha kuwapo na mijadala sehemu mbalimbali ambayo inabishana kuhusu msimamo upi ni sahihi na unatakiwa kufuatwa.

Msimamo huo wa chombo ambacho ni rasmi, ulionyesha timu ya Kagera Sugar ya Bukoba mkoani Kagera imeshuka daraja moja kwa moja huku Mwadui FC na Stand United zikitakiwa kujiandaa kucheza mechi za play off dhidi ya timu za Pamba na Geita Gold FC.

Hata hivyo, jambo la kushangaza, takwimu ambazo zilikuwa zinatolewa na gazeti la Nipashe pamoja na kituo kilichopewa haki ya kuonyesha mubashara mechi za ligi hiyo ndio walikuwa sahihi, sawa na mtunza takwimu wa klabu ya Kagera Sugar.

Wakati Ofisa Mtendaji wa Bodi ya Ligi akitangaza kuwa watachukua hatua kwa ofisa ambaye amehusika na upotoshaji huo, Nipashe linawakumbusha kujipanga upya kwa ajili ya msimu ujao, ili kosa hilo ambalo lilizua mtafaruku lisijirudie.

Kosa hilo ni moja ambalo limeonekana hadharani, lakini kuna mambo mengi yanafanyika ndivyo sivyo, ambayo hayapaswi kuonekana katika ligi hiyo ya juu kwa upande wa Tanzania Bara ambayo pia hutoa wachezaji wengi wanaoitumikia timu ya Taifa (Taifa Stars).

Hakuna jambo lisilowezekana, Bodi ya Ligi inatakiwa kuwa wepesi kujifunza mambo mazuri yanayofanywa na nchi za jirani kwa ili kuifanya ligi kuwa na thamani zaidi.

Kwa kufanya hivyo, tutashuhudia ushindani wa kweli, haki na wachezaji wa timu zote wanapata nafasi ya kuonyesha vipaji vyao na hatimaye kutimiza ndoto zao za kusajiliwa na klabu za nje ya Tanzania kama alivyoweza kuonekana nahodha wa Stars, Mbwana Samatta ambaye sasa anacheza soka la kulipwa huko Ubelgijini.Kujifunza mambo mazuri si makosa, ikiwekana kama ambavyo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linaleta wakufunzi wa makocha kuwanoa walimu wa timu za hapa nyumbani, inatakiwa ifanye hivyo hivyo kwa idara za takwimu na miundombinu ya uwanja ili kufikia maendeleo tunayoyahitaji.

Habari Kubwa