Sakata usambazaji mbolea liwape somo viongozi wetu

12Jan 2018
Mhariri
Nipashe
Sakata usambazaji mbolea liwape somo viongozi wetu

AGIZO lililotolewa na Rais John Magufuli, la kutaka kusambazwa haraka kwa mbolea kwa wakulima katia mikoa yenye upungufu ifikapo leo, limeacha funzo kubwa kwa viongozi na watendaji wa serikali.

Kitu kikubwa cha kujifunza ni kwamba wakati huu wa kuwahudumia wananchi, kuwaondolea kero, kufanyakazi kwa bidii na kusukuma maendeleo kwa kasi kubwa lazima viongozi na watendaji waache tabia ya kufanyakazi kwa mazoea.

Huko nyuma viongozi wetu wakiwamo mawaziri, manaibu mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa mikoa, wakuu wa wilaya, makatibu tawala wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri walijisahau katika utendaji wao wa kazi, hivyo badala ya kwenda kwa wananchi kufuatilia kero na utekelezaji wa shughuli za maendeleo, wamekuwa wakikaa ofisini wakisubiri kupelekewa taarifa na walioko chini yao.

Hata hivyo, staili hiyo ya kufanyakazi ina mapungufu makubwa na kimsingi haifai kabisa katika kipindi hiki ambacho viongozi hao wanatakiwa kuonyesha utendaji wenye tija na ufanisi. 

Baada ya kuwapo malalamiko mengi ya wakulima wa maeneo mbalimbali nchini kuhusu uhaba wa mbolea kipindi hiki, ambacho wanaihitaji sana kwa ajili ya kuanza kupanda mazao, Rais Magufuli alimpa Waziri wa Kilimo, Charles Tizeba siku saba kuhakikisha kwamba mbolea hiyo inasambazwa haraka na kuwafikia wakulima.

Taarifa zilizopo ni kwamba agizo hilo la Rais limetekelezwa kwa kasi, baada ya usambazaji huo kufanyika usiku na mchana.

Ndani ya siku mbili baada ya kutolewa kwa agizo hilo, kiasi kikubwa cha mbolea kilisafirishwa na kuwafikia wakulima wengi katika baadhi ya mikoa yenye msimu mmoja wa mvua ambao umeanza.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), Salum Mkumba, alisema baada ya agizo la Rais, waliamua kuanza kupakia mbolea hiyo kwa kutumia malori ya kukodi na magari makubwa ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Juzi zikiwa zimebaki siku mbili kwa Waziri Tizeba kutekeleza  agizo la Rais Magufuli, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema ameridhishwa na usafirishaji wa mbolea kutoka kwa wasambazaji wa pembejeo nchini kwenda kwa wakulima.

Pia alimwagiza Waziri Tizeba kushirikiana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, kuhakikisha mbolea inafika haraka kwa wakulima.

Majaliwa pia aiitaka TFC kuwa na mikakati madhubuti itakayowezesha upatikanaji wa mbolea kwa wakati wote nchini.

Majaliwa alitoa kauli ma maelekezo  hayo  alipokagua usafirishaji wa mbolea kwenye maghala makubwa matatu jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu alisema serikali inahitaji kuona wakulima wote nchini wanapata pembejeo za kilimo ikiwamo mbolea kwa wakati, ili kilimo kiwaletee tija.

Sakata la mbolea linapaswa kuwaamsha viongozi wetu watambue kuwa jukumu lao sio kukaa ofisini, bali kutembelea wananchi na kusikiliza kilio chao, ili wote wawasimamie walioko chini yao kuwahudumia na kutatua changamoto zinazowakabili.

Viongozi wanapaswa kufahamu ni wakati gani wananchi wanakuwa na mahitaji gani kwa mfano, kuhakikisha pembejeo zinawafikia wakulima mapema kabla ya msimu wa kilimo kuanza.

Kwa kuwa Rais Magufuli ni kiongozi mfuatiliaji na mwenye sifa ya kushughulikia matatizo haraka, wateule wake wanapaswa kuiga mfano wake, vinginevyo watashindwa kwenda na kasi yake.

Wasipobadilika watajikuta kila wakati wakiagizwa na aliyewateua, kitu ambacho tafsiri yake ni kushindwa kazi.

Katika mazingira ya viongozi kujisahau na kufanyakazi kwa mazoea, dawa pekee ya kuwarejesha kwenye mstari ni mamlaka za uteuzi kuwapa maagizo na watakaoshindwa kubadilika wajipime na kuachia ngazi. 

 

Habari Kubwa