Salamu zetu kwa wazazi na walezi

07Aug 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Salamu zetu kwa wazazi na walezi

TANZANIA inaweza kujivuna kuwa ni nchi ambayo licha ya kuwapo kwa corona duniani, taifa hili limenusurika na kuendelea na ratiba ya masomo katika shule za msingi, sekondari na vyuo.

Wanafunzi wake wameendelea na shule na hadi sasa hali ni shwari na ni jambo la kumshukuru Mungu.

Kwa hiyo hiki ndicho kipindi cha kutoa msukumo kwa elimu hivyo wazazi, walezi na walimu waongeze ushirikiano chanya kufanikisha mafanikio ya elimu nchini.

Tanzania ni miongoni mwa nchi chache ambazo sasa zinajivunia kuwa kwenye kundi la uchumi wa kati, hivyo Watanzania tunapaswa kushirikiana kwa pamoja kuipa elimu kipaumbele kwani hata nchi zilizoendelea zilitilia mkazo wa kipekee elimu, hali iliyowawezesha kufikia mafanikio na maendeleo makubwa waliyonayo sasa.

Elimu ndiyo ufunguo wa kila kitu. Ndicho chanzo cha kuwa na uwezo wa kiuchumi, kiteknolojia na hata kifedha nchi zilizoendelea kusimamia maendeleo yake na kutoa mikopo na misaada kwa mataifa yenye uchumi unaokuwa kama Tanzania.

Kwa hiyo ni muhimu wazazi na walezi kushirikiana na serikali na kuona kuwa watoto wanasoma kwa hiari si kwa kushinikizwa.

Tunashauri wasome kwa hiari bila shinikizo la dola wala viongozi wengine wa serikali kwa kuwa iwapo tutawashinikiza kusoma wanaweza kukosa hamasa ya kujifunza kwa bidii.

Wazazi wengine wanawalazimisha watoto wao kujifelisha mitihani ya darasa la saba au kidato cha nne ili wasiendelee na elimu ya sekondari au ya juu na hili linawahusu zaidi mabinti.

Tunawasisizi wazazi na walezi wasiwe vikwazo na kuwazuia watoto wasijizatiti na kusoma kwa bidii hasa wakati huu wakijiandaa kwa mitihani ya darasa la saba na kidato cha nne.

Wapo baadhi ya walezi na wazazi wanaokuwa wagumu kuwapatia watoto wao mahitaji ya msingi ya shule kwa lengo la kuwakwamisha na kuwarudisha nyuma.

Iwapo mchezo huo utaachwa kuendelea unaweza kukwamisha wanafunzi na kuwasababishia kuchukia shule.

Ni kawaida kwa walezi kutumia kisingizio cha umaskini kuwanyima watoto wao mahitaji hayo ili kuwapunguzia kasi ya kusoma hasa wanapokaribia kwenye mitihani ambayo imebakiza miezi michache hilo si jambo jema.

Ni vyema wazazi kama hao wakafuatiliwa ili kukomesha mienendo hiyo kwa kuwa sehemu kubwa ya gharama za elimu inabebwa na serikali kupitia kodi za wananchi.

Tunasema hayo kwa sababu wapo baadhi ya wazazi hawatoi mahitaji muhimu kwa watoto wao mfano sare, madaftari, mikoba ya shule, viatu, chakula na hata kuwalipia gharama za kukaa bweni.

Yote haya husababisha kushindwa kupata mahitaji, haya yanakosababisha watoto wao kukwama kusoma na kuishia kuanguka kwenye Mtihani wa Taifa Kidato cha Nne.

Wazazi kutofuatilia maendeleo ya kitaaluma ya watoto wao ni jambo ambalo linakwamisha ufaulu.

Tunawakumbusha kuwa wana mchango mkubwa kufanikisha maendeleo ya kitaaluma ya watoto wao kutokana na nafasi kubwa waliyonayo kwa watoto.

Ndiyo maana wazazi na walezi ambao hawataki watoto wao wasome, hawatoi ushirikiano katika masuala ambayo yanaongoza thamani kitaaluma kwa watoto wao.

Kwa mfano, kushindwa kukagua kile ambacho mwanawe anajifunza shuleni, kutohudhuria vikao vya wazazi vya kujadili maendeleo ya taaluma ya mwanawe, kutompa hamasa mwanawe kusoma kwa bidii.

Tunawakumbusha mtoto anapokosa uangalizi na ufuatiliaji wa karibu kutoka kwao ni rahisi kufeli masomo.

Wazazi na walezi wakumbuke wana sehemu kubwa ya kupambana na kufanikisha kufikia mafanikio ya kitaaluma hasa wakati huu wa kuelekea kwenye mitihani ya la saba na kidato cha nne.

Habari Kubwa