Sekta ya pamba sasa inahitaji mapinduzi

10Jun 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Sekta ya pamba sasa inahitaji mapinduzi

SEKTA ya pamba inahitaji mapinduzi kwa sasa ili kulirejeshea thamani zao hilo.

Pamba ni mojawapo ya mazao muhimu ambayo serikali ya sasa imeliweka katika orodha ya mazao ya kimkakati, kwa lengo la kuliongezea thamani, hivyo kuliingizia taifa pato zaidi la kigeni sambamba na kuwanufaisha wakulina wa zao hilo.

Mazao mengine ni kahawa, chai, mkonge, tumbaku na korosho, huku jitihada pia zikifanyika kwa lengo la kulifufua na kuliboresha zao la michikichi.

Tunaona umuhimu huu kutokana na yaliyozungumzwa na wadau wakati wa mkutano uliowakutanisha mwishoni mwa wiki jijini Mwanza, kwa lengo la kujadili kilimo cha zao hilo.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasungwa, aliweka wazi kuwa wakulima wa mazao yote nchini wakiwamo wa pamba, wanapaswa kulima kilimo cha kisasa ili kuongeza uzalishaji wenye tija, kujikita katika kilimo cha biashara na kuondokana na kilimo cha kujikimu.

Aliwaambia wajumbe wa Bodi ya Pamba Tanzania na wadau wa tasnia ya pamba

Kwamba wakulima wanapaswa kuhamasishwa kwenye kilimo cha kisasa ili kuongeza uzalishaji kwa kutumia pembejeo bora na teknolojia ya kisasa, ambayo mkulima ataweza kupata kilo 1,350 kwa hekari moja kama nchi nyingine zinazolima pamba.

Alisema wengi kwa sasa wanapata kilo 150,200, hivyo ifike mahali wafuate maelekezo na kuzingatia kanuni za kilimo cha kisasa, na kwamba dhamira ya serikali ni kuhakikisha kuwa kilimo nchini kinakuwa cha kibiashara na kuondokana na kilimo cha kujikimu.

Alisema, ifike mahali pamba yote nchini inachakatwa ndani ya nchi kwa kuhakikisha viwanda vinafufuliwa na watu wanawekeza ili kuwe na uhakika wa soko.

Lwa mujibu wa Waziri huyo, asilimia 65 ya viwanda inategemea malighafi kutoka kwenye kilimo, hivyo lazima mfumo wa kilimo wa kisasa uwezeshwe, kwani kilimo ndio kinatupatia asilimia 100 ya chakula," alisema.

Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk. Bernard Kibese, alisema hali ya uchumi ipo vizuri licha ya uwapo wa corona, huku akiwahakikishia wakulima wa pamba kuwa soko lipo kwani vyombo vya fedha vipo tayari kununua pamba yote itayazozalishwa nchini, na kuwa hakuna mnunuzi atakaye kosa mkopo.

Aliziagiza benki zote kutowapa wakulima wa pamba fedha mkononi isipokuwa kupitia akaunti za benki.

Kamati ndogo ya wadau wa pamba ilisisitiza uzalishaji wenye tija, na kuwa lengo ni ifikapo mwaka 2020/23 Tanzania iwe imezalisha tani milioni moja za pamba.

Ni jambo lililo wazi kuwa pamba inalimwa na wakulima wengi nchini, kwa kuzingatia kuwa ni eneo kubwa la nchi ambalo linaruhusu zao hilo kustawi, hivyo hiyo inapaswa kuwa changamoto kwetu ya kuhamasisha uzalishaji wake sambamba na kuweka mazingira bora na rafiki kwa ajili ya uzalishaji.

Serikali kwa upande wake kuanzia msimu huu utakoanza Juni 15, ihakikishe kwamba kampuni za ununuzi ni zenye sifa pamoja na wakulima kupitishiwa malipo yao benki ili kuepusha wizi na utapeli sambamba na malipo hayo kulipwa kwa wakati. Hatua hii itawapa moyo, hamasa na morali wakulima kuzalisha kwa wingi zao la pamba.

Tunaelewa kuwa suala la bei litapangwa na soko lenyewe, lakini serikali ikiona mambo yanakwenda ndivyo sivyo, ikiwamo bei ya kuwanyonya, iingilie kati kwa kuweka bei elekezi.

Baada ya hapo mkakati kamambe ubuniwe na kutekelezwa kuhakikisha wakulima wanalima kisasa, hivyo kuondokana na dhana kuwa pamba ya Tanzania ni chafu.

Kuna takwimu zinazoonyesha msimu uliopita, bei ya zao hilo katika soko la dunia kusuasua kutokana na changamoto kadhaa, lakini hili lisiwakatishe tamaa wakulima bali kuwapo nguvu ya pamoja ya wadau kuhakikisha sekta hiyo inafanyiwa mapinduzi.

Habari Kubwa