Sensa ya kilimo, uvuvi, ufugaji ina umuhimu

06Aug 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Sensa ya kilimo, uvuvi, ufugaji ina umuhimu

TAARIFA kwamba Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), inakusudia kufanya sensa ya kilimo, uvuvi na ufugaji nchini ili kupata matokeo ya mchango wa sekta hiyo kwenye pato la Taifa na kupanga mikakati mingine mipya, zina mantiki.

Ofisi hiyo imesema kuanzia  timu ya wataalamu wa NBS ipo mkoani Morogoro kwa ajili ya kufanya zoezi la majaribio katika mikoa sita ya Bara na miwili Zanzibar na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha ili kusaidia kupatikana kwa takwimu hizo.

Akizungumza katika Maonyesho ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea mkoani Simiyu. Mtakwimu Mwandamizi kutoka ofisi hiyo, Samwel Kawa, alisema  kupatikana kwa takwimu hizo zitawezesha kupanga, kupima na kufuatilia Tathmini ya Programu ya Pili ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (ASDP II) .

Alisema pia kupatikana kwa takwimu hizo kutasaidia kufikia uchumi wa kati wa Tanzania ya viwanda pamoja na malengo ya maendeleo endelevu na mpango wa pili wa Taifa wa maendeleo na usalama wa chakula pamoja na vita dhidi ya umaskini.

Kawa alisema sensa ya kilimo ya mwisho ilifanyika mwaka 2007/2008, hivyo kufanyika kwa sensa mpya kutatoa takwimu mpya kuhusu uzalishaji wa mazao, idadi sahihi ya mifugo pamoja na mazao yatokanayo na mifugo.

Jambo la msingi na la kuzingatia ni kwamba Tanzania kwa sasa inaelekea katika safari ya uchumi wa kati kupitia ujenzi wa viwanda. Ikumbukwe kwamba viwanda vinahitaji malighafi zitokanazo na kilimo, uvuvi na mifugo.

Kwa maana hiyo haiwezekani tena kuendesha na kusimamia sekta hizo nyeti bila kuwa na takwimu sahihi, halisi na zinazokwenda na wakati.

Tunaona kwamba uamuzi wa kufanya sensa ya kilimo, mifugo, uvuvi  kwa sasa ni wa mantiki kwa sasabu upo uwezekano kwamba takwimu nyingi za sasa hazina uhalisia kwa sababu umepita muda mrefu bila sensa hiyo kufanyika.

Taarifa kuwa  sensa ya mwisho ilifanyika mwaka 2007/2008, zinatoa picha kuwa tamwimu zinazotumika kuhusiana na masuala ya sekta hizo zina mapungufu makubwa yasioendana na hali halisi, hivyo upo uwezekano makubwa wa kutoa takwimu zisizo za uhakika.

Kwa hali hiyo unaweza kupotosha takwimu kuhusu uzalishaji wa mazao, idadi sahihi ya mifugo na mazao yatokanayo na mifugo pamoja na idadi ya samaki walioko nchini.

 

Kwa hiyo takwimu halisi za sekta hizo zitaiwezesha  serikali, wananchi, wadau pamoja na wawekezaji kuwa na uelewa mpana ili pale wanapotaka kufanya shughuli zao wafanye kwa kuzingatia takwimu.

Kwa mfano, serikali itapanga mipango yake ya kuzisaidia na kuziwezesha sekta hizo kwa kuzingatia mahitaji halisi.

NBS pia inasema sensa hiyo itakusanya taarifa kuhusu takwimu na hali ya takwimu nchini.

Kwamba kupitia takwimu hizo, itasaidia serikali kujua mchango wa sekta katika pato la taifa, kupima mikakati yake ya kufikia Tanzania ya viwanda na inatoa fursa kwa wadau wengine kujua fursa na changamoto ya sekta hiyo.

Tunaunga mkono hatua hiyo, huku tukiishauri serikali kuhakikisha kwamba inaweka utaratibu endelevu wa kufanya sensa ya sekta hizo  kwa wakati mwafaka ili kuwa na takwimu za kisasa, hivyo kubaini changamoto  zinazojitokeza na kuzitafutia ufumbuzi haraka.

Habari Kubwa