Serengeti Boys msibweteke na ushindi mliopata nyumbani

02Jul 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Serengeti Boys msibweteke na ushindi mliopata nyumbani

KWA mara nyingine timu ya soka ya vijana ya Taifa ya umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) leo inatarajia kushuka dimbani kuwavaa wenyeji Shelisheli katika mechi ya marudiano ya kusaka nafasi ya kucheza fainali za zijazo za Kombe la Vijana Afrika.

Fainali za mashindano hayo ya vijana yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) zinatarajiwa kufanyika mwakani Madagascar.

Katika mechi ya kwanza iliyofanyika Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu Bakari Shime kilipata ushindi wa mabao 3-0.

Matokeo hayo ni mazuri na yanaonekana kuwa ni mwanzo mzuri wa safari ya timu hiyo ambayo kwa muda mrefu haijafanikiwa kucheza fainali hizo za Afrika.

Lakini kuona ushindi huo ndiyo kazi imemalizika, ni makosa kwa sababu mpira ni mchezo wa makosa na endapo wachezaji na benchi la ufundi 'watabweteka' mabo yanaweza kubadilika kwa sababu wapinzani wao wanaweza kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani.

Nipashe tumefurahishwa na kauli aliyoitoa Shime, siku moja kabla ya kuanza safari ya kuelekea Shelisheli kwamba, wataenda ugenini kupambana ili kusaka ushindi.

Mabao 3-0 waliyopata nyumbani wameyafuta kwenye akili zao na watachuka uwanjani leo wakiamini ndiyo wanaanza kazi.

Lengo la kufanya hivyo, Shime alieleza kwamba hatafurahi zaidi kuona Serengeti Boys inasonga mbele kwenye mashindano hayo kwa kushinda mechi zote mbili.

Hiyo itawajenga zaidi wachezaji wake na kuona kwamba kila mechi ambayo wanatakiwa kucheza, lengo lao kuu ni kusaka ushindi.

Ushindi au sare yoyote itakayopatikana katika mechi ya leo itawaongezea hamasa wachezaji kwa ajili ya hatua inayofuata ambayo nayo inatarajiwa kuwa na changamoto zaidi.

Mshindi wa jumla katika mechi hiyo ya leo kati ya wenyeji Shelisheli au Serengeti Boys atakutana na yosso wa Afrika Kusini ambao tunaamini ni moja ya timu za vijana zilizoandaliwa kwa muda mrefu, zikicheza pia mechi mbalimbali za kirafiki na wachezaji wake wakiwa ni waliopitia mafunzo ya soka wakiwa na umri mdogo zaidi.

Kwenye soka hakuna kinachoshindikana, kama Serengeti Boys iliweza kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye mashindano maalumu ya vijana yaliyofanyika India na kutambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), mnao uwezo wa kuifunga Shelisheli na kutinga katika raundi ya pili ya mashindano hayo.

Gazeti hili pia linapenda kuchukua nafasi kuzikumbuka kampuni za biashara na taasisi mbalimbali kujitokeza kuidhamini timu hiyo na si kukaa pembeni kusubiri ifanikiwe ndiyo iwaunge mkono.

Muda sahihi wa kuwaunga mkono vijana hawa ambao ndiyo tegemeo la Tanzania hapo baadaye ni sasa, mkipanda vizuri pamoja, mtavuna vizuri pamoja. Jitokezeni kusaidia timu hiyo ambayo inahitaji vifaa vya michezo na fedha za kugharamia kambi.

Baada ya timu ya Taifa (Taifa Stars) kuondolewa katika mbio za kusaka nafasi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) na Kombe la Dunia, Serengeti Boys ndiyo jicho pekee lililobakia huku tukikumbuka Rais wa TFF, Jamal Malinzi alimweleza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipokutana na wadau wa michezo nchini kuwa shirikisho hilo limejipanga kupambana kuona Tanzania inafuzu kucheza Fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2026.

Mwaka 2005, timu hiyo ilifuzu kushiriki fainali hizo za vijana Afrika lakini CAF iliiondoa na Tanzania kufungiwa kwa muda wa miaka mitatu baada ya kubainika kumtumia mchezaji Nurdin Bakari aliyekuwa na umri mkubwa.

Tangu hapo Tanzania haijafuzu tena kushiriki fainali hizo na imekuwa ikitolewa mapema.
Mungu ibariki Serengeti Boys, Mungu ibariki Tanzania.

www.guardian.co.tz/circulation

Habari Kubwa