Serikali imeonyesha dhamira kuinua kilimo

28Nov 2017
Mhariri
Nipashe
Serikali imeonyesha dhamira kuinua kilimo

Mamlaka ya Kudhibiti Mbolea (TFRA) imekamata wafanyabiashara 25 kutokana na kukiuka sheria na taratibu za uhifadhi na kuuza mbolea kwa bei tofauti na iliyoelekezwa na serikali.

Ukamataji huo unafuatia taarifa ya Wizara ya Kilimo kuwa baadhi ya wafanyabiashara wadogo wa mbolea wamekuwa wakikiuka bei elekezi kutokana na kuuziwa kwa bei ya juu na wafanyabiashara wakubwa.

Kwa mujibu wa taarifa za wizara, baadhi ya watu wanaouza mbolea kwa jumla wamekuwa wakiwauzia wafanyabiashara wadogo kwa bei elekezi ya rejereja badala ya bei ya jumla, hivyo kuwalazimisha nao kuuza juu ya bei elekezi ya serikali na hivyo kufanya wakulima ama kuumia zaidi au kutotumia kabisa mbolea; hivyo kushusha ubora na wingi wa mazao yanayozalishwa.

Aidha, taarifa zilizopo wizarani zinabainisha kuwa mikoa ya Ruvuma, Lindi, Mtwara, Mwanza na Geita ina wafanyabiashara ambao hufungua mifuko na kuuza mbolea ya kupandia (DAP) kwa Sh. 2,000 kwa kilo ili wapate Sh. 100,000 kwa mfuko wa kilo 50 badala ya bei elekezi ya kuanzia Sh. 51,000-Sh. 56,000 kulingana na umbali kutoka Bandari ya Dar es Salaam.

Aidha, taarifa hizo zinaonyesha mbolea ya kukuzia (Urea) huuzwa na wafanyabiashara hao wasio waaminifu kwa Sh. 1,500 kwa kilo ili wapate Sh. 75,000 kwa mfuko wa kilo 50 badala ya bei elekezi ya kuanzia Sh. 41,000-Sh. 45,000.

Ujanjaujanja huu, kwa vyovyote, unakwamisha mkakati wa serikali wa kuongeza matumizi ya mbolea ambao umekuwa na umuhimu wa pekee hasa ikizingatiwa kwamba Rais John Magufuli ameweka lengo la kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati unaoendeshwa kwa viwanda kufikia mwaka 2025.

Ikumbukwe kuwa sehemu kubwa ya viwanda hivyo itategemea malighafi itokanayo na mazao ya kilimo, hivyo hujuma yoyote inayofanywa dhidi ya wakulima inatishia kufikiwa kwa azma hiyo miaka sita tu ijayo.

Ndiyo maana tunachukua fursa hii, Nipashe, kwanza kumpongeza Kaimu Mkurugenzi wa TFRA, Lazaro Kitandu, kwa mamlaka yake kufanikisha kukamatwa kwa wafanyabiashara hao 25 wa jumla lakini pia kusisitiza kuwa hatua hiyo imeonyesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuinua tija ya kilimo.

Hatua hiyo imeonyesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuinua tija ya kilimo, tunasema, kwa sababu tayari mhimili huo wa dola ulishaahidi kushughulikia watu wote, wakiwamo watendaji wa serikali, waliohusika na upigaji wa mabilioni ya shilingi kupitia pembejeo hewa.

Tunafahamu, Nipashe, kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inaendelea na uchunguzi wake kuwasaka wahusika wote wa ufisadi huo ambao Rais Magufuli amekuwa akiutolea mfano mara kwa mara anapopata fursa ya kuzungumzia aliyoyakuta baada ya kukabidhiwa nchi Novemba 5, 2015.

Lakini tunafahamu pia, Nipashe, kuwa serikali hiyo hiyo imeanzisha mifumo mipya miwili yenye lengo la kumwezesha mkulima kupata mbolea bora na kwa bei nafuu ili kuchochea ongezeko la uzalishaji nchini kukidhi mahitaji ya familia na kuuza ziada ndani na nje ya nchi.

Kwa hatua hizo, tunasema Nipashe, Serikali imeonyesha dhamira kuinua tija ya kilimo. SASA. 

Habari Kubwa