Serikali itenge fedha za kutosha za majanga

08Nov 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali itenge fedha za kutosha za majanga

KAYA 118 zenye watu zaidi ya 700 katika Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, hazina makazi, baada ya nyumba zao kubomolewa na nyingine kuezuliwa na mvua iliyonyesha kwa dakika 30 ikiwa imeambatana na upepo mkali Jumamosi iliyopita.

Mvua hiyo iliyoambatana na upepo mkali, ilinyesha usiku na kusababisha athari kadhaa, ikiwamo kuharibu mazao mashambani na watu watatu kujeruhiwa katika vijiji vya Chakamba, Igara, Bwasa na Lugara.

Kutokana na hali hiyo, wananchi hao wamejikuta katika wakati mgumu ikiwamo kulala nje na kuhitaji misaada kama chakula, magodoro, mahema na mahitaji mwengine ili waendelee na maisha yao ya kila siku.

Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Francis Chang’ah, alitangaza kwamba serikali imetoa msaada wa mabati 200 na magodoro 20, vikiwa na thamani ya shilingi milioni nane.

Mvua hiyo ilikuwa na nguvu kwa kuwa ilisababisha hata baadhi ya nyumba za ibada kubomoka.

Janga hilo limetokea siku chache, baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania TMA kutahadharisha kuwa mikoa ya Kanda ya Ziwa ya Kagera, Mwanza, Shinyanga, Mara, Simiyu na Geita itakuwa na mvua kubwa, hivyo kuwataka wakazi wake kuchukua tahadhari.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Frank Bahati, aliwaomba wadau mbalimbali wa wilaya hiyo na nje ya mkoa huo kujitokeza kuwasaidia waathirika hao misaada inayohitajika ikiwamo ya chakula na vifaa vya ujenzi.

Pamoja na misaada iliyotolewa na wilaya, bado waathirika wanahitaji misaada zaidi kwa kuwa iliyotolewa ni kidogo kukidhi mahitaji halisi ya waathirika.

Serikali inawajibu wa kuwasaidia wananchi pale wanapokumbwa na majanga ya asili kama matetemeko ya ardhi, kimbunga, mafuriko na mengine kwa sababu sio rahisi wananchi kuyamudu, ingawa ni jambo jena kwa wadau na raia wema kujitokeza kusaidia.

Tunasema hivyo kwa kuwa jukumu la serikali ni kulinda usalama wa raia na mali zao. Hata hivyo, kuna matukio mengi ya maafa ambayo yamekuwa yakitokea, lakini serikali inashindwa kuwasaidia waathika na wakati mwingine misaada inayotolewa ni kidogo sana.

Tunashauri kwamba serikali iweke utaratibu wa kutenga fedha za kutosha katika bajeti yake kwa ajili ya kukabiliana na maafa badala ya kusubiri yatokee.

Tunajua kwamba haina fedha za kutosha, lakini kama maafa kitakuwa kipaumbele cha serikali, kuna uwezekano mkubwa wa kukabiliana na majanga na kwa wakati.

Kwa mfano, tahadhari iliyotolewa na TMA kuhusu uwezekano wa kunyesha mvua kubwa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ilitakiwa serikali ijiandae kwa misaada na vifaa kwa ajili ya watu ambao wataathirika.

Janga la tetemeko la ardhi la Septemba 10, mwaka huu lililoacha vifo vya watu 17 na uharibifu mkubwa wa makazi na miundombinu kwenye Kanda ya Ziwa, lakini hasa mkoani Kagera, lilidhihirisha jinsi gani serikali haijajiandaa kikamilifu katika kukabiliana na majanga

Tetemeko hilo lilielezwa kuwa na ukubwa zaidi katika historia kutokea nchini katika miaka ya 2010, lilisababisha maelfu ya watu kukosa makazi, huku misaada ikitegemewa kutoka kwa wadau.

Kutenga bajeti ya maafa sambamba na kununua vifaa vya kisasa vya uokoaji utakuwa uamuzi mzuri.

Habari Kubwa