Serikali itimize ahadi yake ya kulegeza kibano kwa wasanii

19Dec 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali itimize ahadi yake ya kulegeza kibano kwa wasanii

MUZIKI, filamu ni moja ya tasnia ambazo zinawapa nafasi kubwa vijana kujiajiri.

Jumapili ya wiki iliyopita wadau wa tasnia hiyo walishuhudia Tuzo za Sanaa kwa wasanii wa Afrika Mashariki, hafla ambayo ilihudhuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.

Mengi yalizungumwa na Waziri Nape aliongea mengi, lakini yote aliyoyazungumza yalitokana na maoni au kauli za wasanii.

Wasanii wengi wa filamu na muziki walionekana kutoa lawama Kwa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) kwa namna ambavyo Baraza hilo limekuwa likiendesha shughuli zake hasa kwa kuwabana wasanii wa muziki na filamu.

Pamoja na kuwa tuzo hizo ni muhimu kwa wasanii hao, lakini pia wasanii walitumia nafasi hizo kueleza yale yanayowakera kwa kupitia mshereheshaji wa shughuli hiyo Salama Jabir.

Nipashe inajua nini ambacho Waziri Nape aliahidi kwa wasanii kuwa mambo yatalegea kwa kulegeza masharti ya Basata.
Nipashe inatumia nafasi hii kuikumbusha Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuwa wasanii bado wanakumbuka ahadi yao.

Zipo sheria na taratibu ambazo wasanii lazima wazifuate ili mambo yaende sawa.

Waziri Nnauye aliahidi kuwa ataangalia upya namna ya utaratibu wa Basata kuhusu namna ya kuwaongoza na kuwadhibiti wasanii wa Bongo Fleva katika nyimbo ambazo wanazitunga na kuzitoa.

Nape alisema ukweli kuwa zipo taratibu zinazowabana wasanii na Serikali imetambua hilo, hivyo itawaambia Basata kuangalia namna ya kulegeza kamba.

Tunamkumbusha Waziri Nape kuwa Nipashe inatambua ahadi yake aliyoitoa kwenye hafla ya tuzo za EATV kuwa Basata ambayo ipo chini ya Wizara yake italegeza kamba ya kuwabana wasanii.

Asante kwa EATV kwa tuzo ambazo zimetoa mwanga na ambazo zineishtua serikali kwa kutambua kazi za wasanii.

Tunachokumbusha kwa Waziri Nape ni kuhakikisha kwamba wanatimiza ahadi aliyoitoa ya kuhakikisha wasanii wanapunguziwa bughudha katika harakati zao za kazi za kisanii

“Kama ule upande wa pili tunabanwa, naagiza basi wenzetu wa Basata walegeze kidogo, na kwa kazi hii ya EATV Magufuli ataendelea kuniweka hapana,” hiyo ni kauli ya Nape akizungumzia tuzo za EATV.

Tunaiomba Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo kuhakikisha wanasimamia kile ambacho wamekitamka juu ya wasanii.

Lakini pia Nipashe tunaomba kanuni na maadili ya Mtanzania yazingatiwe kwenye tasnia nzima ya muziki na filamu.
Mfano, yapo mavazi ambayo kwa utamaduni wa Mtanzania huwezi kukubali yaonyeshwe kwenye umati wa watu.

Maadili yazingatiwe, lakini pia nafasi ya kuonyesha vipaji, juhudi na usanii wa wanamuziki uzingatiwe.

Nipashe tunaipongeza EATV kwa tuzo zao na tunashauri ubunifu zaidi utumike kwenye tuzo zijazo. Pia tunaiomba serikali kutimiza ahadi yake kwa vitendo ya ‘kulegeza’ kidogo mbano kwa wasanii.

Tunaamini kuwa kwa kufanya hivyo, wasanii watahamasika kufanya vuzuri zaidi katika kazi zao na zitawatoa kwa kutengeneza ajira za uhakika na pia kupata kipato zaidi.

Habari Kubwa