Serikali iweke mipango endelevu ununuzi mazao

16Sep 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali iweke mipango endelevu ununuzi mazao

KILIO cha wakulima wa mahindi katika mikoa iliyozalisha kwa wingi ni kikubwa kutokana na kutonunuliwa kwa utaratibu wenye uwazi.

Jambo la kusikitisha na kushangaza ni kwamba serikali inatekeleza kidogo ahadi yake ya ununuzi wa mazao hayo.

Kutokana na hali hiyo, Bunge katika mkutano wa mwezi huu lilitoa maazimio ya kuitaka serikali kuhakikisha mahindi yananunuliwa, huku wabunge wakitaka kuongezwa kwa fedha, ambazo ziliongezwa kuwezesha ununuzi mazao hayo na kuweka kwenye Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB).

Mapema wiki hii, serikali ilitangaza kuanza kununua tani 90,000 baada ya kutoka Sh. bilioni 50, ili kunusuru soko la zao hilo na kila kilo moja ilinunuliwa kwa Sh. 500. Mikoa saba ambayo NFRA itakayoanza kununua ni Ruvuma, Rukwa, Njombe, Songwe, Mbeya, Katavi na Iringa, huku CPB ikinunua mikoa ya Rukwa, Katavi, Njombe, Songwe, Dodoma na Manyara.

Licha ya jitihada hizi, lakini kuna mambo ambayo hayako sawa kwa maana ya kwamba ununuzi wa mazao unafanyika kwa nguvu ya soda, kwa kuwa kama walijipanga vizuri maana yake tungeona tangu awali na yasingetokea malalamiko ya wakulima.

Tunaamini nchi inaongozwa kwa mipango ambayo hupangwa kuanzia ngazi za vijiji na mitaa hadi taifa, na ndiyo maana kuna maofisa kilimo kuanzia ngazi ya chini hadi taifa ambao hukusanya takwimu za wakulima na mazao.

Kutokana na takwimu hizo ni rahisi kujua makadirio ya mavumo kwa zao fulani kwa mwaka huo ni kiasi gani, na namna ya kuhakikisha soko la uhakika kwa wakulima, na kama NFRA itanunua basi wanajua uwezo wao ni kiasi gani kutoka na fedha iliyotengwa na serikali.

Mikoa inayozalisha zaidi inajulikana na kila mwaka inazalisha mazao hayo na mengine, hivyo ni muhimu kukawa na mipango endelevu kuhakikisha yananunuliwa kwa wakati na bei sahihi bila kuwaumiza wakulima.

Tunaona hakukua na sababu ya kusubiri kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi aielekeze serikali au Bunge kutoa maazimio na kuitaka serikali kutekeleza, bali kutokana na mipango iliyopo suala hilo lingemalizwa.

Ni muhimu serikali ikahakikisha wakulima wanakuwa na uhakika, na kama kuna kiasi fulani cha bajeti kinatengwa kila mwaka kikafahamika, kutokana na makisio ya mavuno kwa mwaka husika.

Ni matarajio yetu kuwa NFRA itajiendesha kibiashara kama wakala zingine kwa kuhakikisha mahindi ya wakulima yananunuliwa badala ya watu binafsi kununua na kisha kuiuzia serikali.

Malalamiko ya wakulima yamejitokeza Ruvuma, na walieleza wazi kuwa wapo baadhi ya watu serikalini ndiyo wanauza mahindi kwa wakala huku wakulima wakiendelea kusota.

Ni muhimu mipango ikaenda na uhalisia wa mambo kwamba makadirio yanaonyesha mwaka huu kwa sababu mbalimbali, wakulima wanatarajiwa kuvuna kiasi hiki na NFRA inatakiwa kuwa na uwezo wa kununua kiasi fulani na wengine wataruhusiwa kutafuta masoko ya ndani na nje.

Tunashauri kuwa suala hili lisichukuliwe kwa zima moto bali kuwe na mipango endelevu ya ununuzi wa mahindi, kwa kuhakikisha mipango ya kila mwaka ya serikali inaendana na uhalisia.

Haitarajiwi kwa kilichotokea mwaka huu haitarajiwi kijirudie mwakani, ufike wakati kama huu wakulima waanze kuhangaika kupata masoko na wakala ashindwe kununua mazao kama inavyotakiwa.