Serikali, taasisi zake wajenge utamaduni wa kulipia huduma

08Sep 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Serikali, taasisi zake wajenge utamaduni wa kulipia huduma

SERIKALI imetoa siku saba kwa wadaiwa sugu wote wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), zikiwamo wizara na taasisi za serikali kulipa madeni yao, zikishindwa zitupiwe vyombo nje.

Agizo hilo lilitolewa juzi na Rais John Magufuli, na kumweleza Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu, asimuogope mtu yeyote katika kutekeleza agizo hilo na kwamba kila anayedaiwa ni lazima alipe na asiyelipa atolewe nje.

Alisema watendaji wa taasisi za umma wanaomba safari za kwenda nje ya nchi na kila wanapokaa vikao wanalipana posho, lakini ni jambo la ajabu wanashindwa kulipa kodi kwa NHC. Alisema taasisi za umma ambazo hazilipi kodi zitolewe vyombo nje haraka ili ziwahi kuhamia makao makuu ya nchi mkoani Dodoma.

Kwa mujibu wa Mchechu, mpaka sasa NHC inadai Sh. bilioni 9.5 kutoka kwa wapangaji zikiwamo taasisi za umma. Deni hilo kubwa linaonyesha jinsi shirika linavyokosa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi.

Jambo linaloshangaza ni serikali na taasisi zake kutolipa kodi ya pango kwa kipindi kirefu licha ya fedha hizo kutengwa katika bajeti. Kama fedha hizo zinatengwa halafu hazipelekwi NHC basi kuna hujuma.

Wizara na taasisi za serikali kwa muda mrefu zimekuwa na tabia ya kutolipia kuduma zingine kama maji na umeme na tabia hiyo imechangia kwa kiwango kikubwa kudhoofisha au kuua mashirika ya umma yanayowapa huduma.

Kwa mfano, madeni ambayo serikali na taasisi zake zinadaiwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na mamlaka za maji ndiyo yaliyosababisha mashirika hayo kushindwa kutekeleza mipango ya utoaji wa huduma bora.

Shirika la Ndege Tanzania (ATC) liliyumba kutokana na tabia ya baadhi ya viongozi wa serikali ambao walikuwa wakisafiri bure, hivyo kulikosesha mapato.

Agizo alilotoa kwa NHC itakuwa vizuri kama atalitoa pia kwa Tanesco na mamlaka za maji kwamba wadaiwa wote sugu wakatiwe huduma za umeme na maji ili mashirika hayo yapate fedha zake kwa ajili ya kujiendesha na kutekeleza miradi.

Kiasi kikubwa ambacho wizara zinadaiwa na NHC kinatia shaka kiasi kwamba watu wanaweza kuhisi kwamba kuna mitandao serikalini ambayo inazitumia kwa manufaa yao.

NHC inasema kuwa baadhi ya wadaiwa ni iliyokuwa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi (Sh. bilioni mbili), Benki ya Azania (Sh. milioni 161) na Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa (Sh. milioni 631).

Wengine ni Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Sh. bilioni 1.3), Wizara ya Ujenzi (Sh. bilioni mbili), Tume ya Utumishi (Sh. milioni 109) na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Sh. bilioni moja.

Kimsingi, Serikali ya Awamu ya Tano imeyarithi madeni hayo, lakini tunazishauri wizara na taasisi zote za serikali zinazodaiwa kulipa deni hilo haraka ili NHC itekeleze majukumu yake hususan la kujenga nyumba kwa ajili ya watumishi wanaohamia Dodoma.

Tunawashauri makatibu wakuu wa wizara zote na wakuu wa taasisi za umma kuweka utaratibu wa kulipa madeni kwa wakati kwa kuwa fedha hizo zinakuwa zimetengwa kwenye bajeti, sambamba na kutengeneza mifumo ya ufuatiliaji wa ulipaji wa madeni hayo.

Hatua hizo ziende sambamba na kuwafichua na kuwachukulia hatua waliosababisha hali hiyo, ambayo inatoa picha mbaya kwa serikali na taasisi zake.

Habari Kubwa