Sheria, kanuni za usalama barabarani zirekebishwe

27Sep 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Sheria, kanuni za usalama barabarani zirekebishwe

WAKATI wiki ya usalama barabarani ilizinduliwa jana, takwimu zilizoko zinatisha kutokana na idadi ya vifo na majeruhi kuwa kubwa kwa miezi saba ya mwaka huu.

Kwa mujibu wa takwimu za Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabarani, Mohammed Mpinga, kuanzia Januari hadi Julai, 2016, watu 1,580 wamekufa, wengine 4,659 walijeruhiwa katika ajali 5,152 zilizotokea nchi nzima. Waliokufa kutokana na ajali za pikipiki ni 430, waliojeruhiwa ni 1,147 katika ajali 1,356.

Ajali nyingi zinasababishwa na uzembe wa madereva pamoja na kutofuatwa kwa sheria, taratibu na kanuni za barabarani. Wiki iliyopita zilitokea ajali tatu za mabasi katika mikoa mitatu ambazo zilisababisha vifo vya watu 27 na kujeruhi 43.

Kinachochangaza ni kwamba ajali zote tatu chanzo kinatajwa kuwa ni mwendokasi. Ajali ya basi la kampuni ya New Force iliyotokea mkoani Njombe wakati likitokea Dar es Salaam kuelekea mkoani Ruvuma, ilisababisha vifo vya watu 12 na majeruhi zaidi ya 10.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Prudensiana Protas, alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa dereva.

Ya pili litokea katika Kwimba mkoani Mwanza na ililihusisha basi la Kampuni ya Super Shem lililokuwa linatokea Mbeya kwenda Mwanza. Basi hilo liligongana na Hiace na kusababisha vifo vya watu 10 na majeruhi saba. Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, na Mkuu wa mkoa huo, John Mongella, walitaja mwendokasi kuwa chanzo chake.

Katika ajali ya tatu, Hiace mbili ziligongana wilayani Mkuranga, mkoa wa Pwani na kusababisha vifo vya watu wawili na 23 kujeruhiwa. Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Bonaventura Mushongi, alisema chanzo ni mwendokasi.

Maadhimisho ya Wiki ya Usalama Barabarani hayatakuwa na maana yoyote ikiwa hayatatumika kuchukua hatua mbalimbali zitakazoweza kupunguza janga la ajali.

Bila kufanya hivyo, kuna uwezekano mkubwa wa kuongezeka matukio ya ajali kwa miezi iliyobaki kabla ya kuumaliza mwaka huu.

Tunaiunga mkono kauli ya Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) kuwataka wadau wa usalama barabarani kuadhimisha wiki hii kwa kupaza sauti na kutoa wito wa kufanyiwa marekebisho ya sheria na kanuni za usalama barabarani hasa Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1972.

Kwamba maeneo ambayo yanapaswa kuzingatiwa katika marekebisho ni mwendo kasi, ulevi wakati wa uendeshaji, uvaaji kofia ngumu, kufunga mikanda na vizuizi kwa watoto.

Kuna umuhimu wa kuchukulia jambo hili kama dharura kwa kuzipa nguvu sheria hiyo kuwadhibiti wanaokiuka matumizi sahihi ya barabara.

Ingawa takwimu zinaonyesha kuwa waathirika wakuu wa usalama barabarani ni wanaume, lakini wanawake na watoto ndio wanaoathirika zaidi kwani watoto hukosa huduma na mahitaji ya msingi baada ya kupoteza watu wanaowategemea.

Hatua za ukaguzi wa mabasi, kudhibiti mwendokasi kwa kutumia kamera, doria, faini na kuwapima kilevi madereva mara kwa mara zinapaswa kuwa endelevu kwa lengo la kupunguza ajali.

Kunatarajia kwamna Wiki ya Usalama Barabarani, madereva na wamiliki wa mabasi watakumbushwa kufuata sheria na kanuni za usalama barabarani kwa lengo la kupunguza kasi ya ajali, ambazo zinalisababishia taifa hasara kutokana na kupunguza nguvu kazi yake.

Habari Kubwa