Sheria, kanuni zifuatwe Mtihani darasa la saba

07Sep 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Sheria, kanuni zifuatwe Mtihani darasa la saba

JUMLA ya watahiniwa 795,761 leo wataanza kufanya mtihani wa taifa wa darasa la saba nchini.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dk. Charles Msonde, alitangaza jana jijini Dar es Salaam na kufafanua kuwa maandalizi yote muhimu yamekamilika.

Dk. Msonde alisema kuwa vifaa vya mitihani katika kila manispaa, halmashauri nchi nzima vimefika, hivyo kilichobaki ni watahiniwa kufanya mtihani.

Hata hivyo, alisisitiza sheria, taratibu na kanuni za mtihani kufuatwa na kutoa angalizo kwamba NECTA haitasita kuwachukulia hatua walimu, wanafunzi na watu wote ambao watajihusisha na vitendo vya udanganyifu wa mtihani huo, ikiwamo kuwafutia matokeo yote watahiniwa watakaobainika kuhusika katika vitendo hivyo.

Pamoja na kauli ya NECTA kuwa vifaa vya mtihani vimeshafikishwa katika halmashauri zote, ushauri wetu ni kwamba baraza na halmashauri zote zihakikishe kwamba vifaa hivyo vinasafirishwa na kufika kwenye shule zote mapema ili mtihani uanze na kumalizika kwa muda unaotakiwa.

Walimu, wanafunzi, wasimamizi, wazazi na walezi ni wajibu wao kufuata sheria, kanuni na taratibu za mtihani ili kuepukana na vitendo vya udanganyifu ambavyo vinaweza kuwasababishia adhabu ikiwamo ya kuwafutia matokeo kama Dk. Msonde alivyotoa angalizo.

Athari za kufutiwa matokeo ni kubwa sana kwa kuwa mtu anapofutiwa matokeo anakuwa amepoteza fursa ya kupata elimu katika maisha yake yote, hivyo ni kuhimu kwa kila mmoja kulielewa hilo na kutothubutu kufanya udanganyifu wa aina yoyote.

Kadhalika, askari polisi watakaokwenda kusimamia vituo vya mitihani watatakiwa kuhakikisha kwamba mtihani unafanyika katika mazingira ya amani, tulivu sambamba na kuhakikisha vitendo vya udanganyifu havipewi nafasi.

Watahiniwa wanatakiwa kuwa makini kwa kujibu maswali kadiri walivyofundishwa na walimu wao kwa kuwa mtihani huo una umuhimu mkubwa kwa maisha yao.

Wanatakiwa kufahamu kuwa mtihani ndio msingi wa maisha yao kwani kufeli kunaweza kusababisha wakose fursa ya kupata elimu zaidi. Kutokana na umuhimu huo, hatutarajii kusikia kuwa kuna watahiniwa waliochora picha au kuandika mambo ya ajabu badala ya kujibu kwa ufasaha walichoulizwa.

Katika miaka ya karibuni imezuka tabia miongoni mwa watahiniwa wa elimu ya msingi na sekondari kuchora picha au kuandika mambo ambayo hayahusiani na mtihani husika. Tabia hii imekuwa ikichukuliwa kuwa ni miongoni mwa viashiria vya kuporomoka kwa kiwango cha elimu nchini.

Tunazishauri mamlaka husika za serikali zinazosimamia elimu kuhakikisha kuwa wasimamizi wa mtihani wanalipwa stahiki zao mapema kuepuka uwezekano wa kutokea mazingira ambayo yanaweza kuathiri mtihani huo.

Maandalizi mengine muhimu ni usafiri wa uhakika wa kuipeleka mitihani katika vituo na kuisafirisha kwa ajili ya kusahihishwa.

Ni matarajio yetu kuwa mtihani huo utafanyika katia amzingira mazuri ikiwa tu kila mmoja atatimiza wajibu wake huku suala la msingi likiwa kuzingatia na kufuata sheria, kanuni na taratibu za mtihani. Vinginevyo tunawatakia mafanikio watahiniwa wote.

Habari Kubwa