Sheria ndogo zinahitajika udhibiti maambukizo corona

13May 2020
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Sheria ndogo zinahitajika udhibiti maambukizo corona

VITA dhidi ya maambukizo ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu (Covid-19) unaosababishwa na virusi vya corona, bado inaendelea nchini na duniani kwa ujumla.

Hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa kudhibiti maambukizo ya ugonjwa huo ambao hadi sasa umesababisha zaidi ya watu robo milioni kupoteza mausha na mamilioni kupata maambukizo.

Suala la kuchukua hatua za tahadhari dhidi ya maambukizo ya ugonjwa huu ni muhimu muhimu kwa kila mmoja ili kulinda maisha yake na ya wengine.

Hivyo maelekezo na ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya kuhusiana na tahadhari za kuchukua ni muhimu sana kufuatwa na kuzingatiwa bila kushurutishwa.

Kwa kukukumbushia mambo muhimu ambayo wataalamu wa afya wanayahimiza kama tahadhari dhidi ya maambukizo ya virusi vya corona ni kunawa mikoni na sehemu zingine za mwili ambazo ni rahisi kusababisha maambukizo kwa kutumia maji tiririka na sabuni.

Aidha, kutumia vitakasa mikoni, uvaaji wa barakoa, kuepuka kushikana mikono na pamoja na kuepukana na mikosanyiko.

Hata hivyo, pamoja na elimu inayotolewa na wataalamu pamoja na msisitizo wa kuchukua tahadhari hizo, bado sehemu kubwa ya jamii haionekani kuchukua tahadhari.

Kwa mfano, watu wengi kwenye maeneo kadhaa hawavai barakoa na wanaendelea kukaa kwenye mikusanyoko katika maeneo ya masoko, vijiweni, kwenye minada na mitaani.

Hali hiyo inatishia usalama wao wenyewe na wa wengine ambao wanajitahidi kuchukua tahadhari zinazoshauriwa na kuhimizwa na wataalamu wa afya.

Ni jambo la kushukuru kwamba serikali yetu mbali na kutotangaza hali ya dharura ya kufungia watu ndani, lakini pia imejiweka kando na matumizi ya nguvu dhidi ya watu ambao hawafuati maelekezo ya tahadhari dhidi ya kusambaa kwa virusi vya corona.

Itakumbukwa jinsi ambavyo baadhi ya nchi duniani zilivyolazimika kutumia nguvu ya dola dhidi ya wakaidi wa ‘lockdown’ na marufuku nyingine. Hilo lilipaswa kutupa funzo la kuheshimu na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na serikali yetu.

Kama ukaidi huo utaendelea, serikali inaweza kuamua kutumia nguvu zake dhidi ya wakaidi, hivyo, tunatoa angalizo kwamba kila mmoja popote alipo ahakikishe kuwa anachukua tahadhari kwa mujibu wa maelekezo ya wataalamu wa afya na serikali dhidi ya maambukizo ya virusi vya corona.

Tunazikumbusha halmashauri zetu za miji, wilaya, manispaa na majiji, mbali ya kutoa elimu ya kujikonga dhidi ya maambukizo hayo, zitumie sheria ndogo zilizopo na ikiwezekana kutunga mpya kwa ajili yan kudhibiti maambukizo ya janga hilo.

Sheria hizo pamoja na mambo mengine, zitasaidia kuwawezesha wananchi kwa elimu juu ya kujikinga na maambukizo na vile vile kuwaadabisha wanaokaidi maelekezo yanayotolewa na mamlaka za serikali na wataalamu wa afya.

Tumezisikia baadhi ya halmashauri nchini zilianza kuzitumisha sheria hizo wakati huu wa tishio la virusi vya corona. Kwa mfano, mwishoni mwa wiki hii, Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, mkoani Pwani ilitangaza kuwakamata na kuwapa adhabu ya kufanya usafi wa mazingira vijana watakaokutwa kwenye mikusanyiko.

Mkuu wa Wilaya hiyo alisema kuwa vijana wengi wamekuwa wakikaa kwenye mikusanyiko katika maeneo ya vijiweni. Licha ya kupewa elimu ya kuepukana na mikusanyiko.

Kutokana na ukaidi huo, alisema wataanza kuwakamata na kuwapeleka kwenye maeneo ya masoko na ofisi za umma kwa ajili ya kufanya usafi na mwisho wa siku wanawaachia kurejea makwao.

Tinashauri kuwa halmashauri zote zingine zitumie sheria hizo ndogo kwa kuwa tunaamini zitasaidia katika kipindi hiki cha vita dhidi ya corona.

Habari Kubwa