Shughuli za serikali zifanyikie Dodoma

14Sep 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Shughuli za serikali zifanyikie Dodoma

SERIKALI ya awamu wa tano iliamua kuvunja mfupa ulioshindikana kwa muda mrefu wa  kuhamishia shughuli zake na ofisi kwenye makao makuu ya nchi ambayo yapo jijini Dodoma.

Hata hivyo, pamoja na serikali kuhamia Dodoma na kutungwa kwa sheria ya kuhalalisha uamuzi huo, inaelezwa kuwa bado wapo baadhi ya mawaziri na watendaji wa serikali wanaoendelea kusafiri hadi jijini Dar es Salaam kufanya mikutano, semina na makongamano.

Spika wa Bunge, Job Ndugai, ndiye aliyeibua sakata hilo, kwamba magari ya viongozi wa serikali yamekuwa ‘yakitiririka’ kila wakati kuelekea jijini Dar es Salaam kutokea Dodoma, baada ya siku mbili yanarudi Dodoma.

Kwa mujibu wa Spika Ndgai, hatua hiyo inaongeza gharama za matumizi kwa serikali kwa kuwa kiongozi akielekea jijini Dar es Salaam kutoka Dodoma kuna gharama za malipo mbalimbali zikiwamo posho kwa wasaidizi wake, dereva na wao wenyewe.

Tunakubaliana na kauli hiyo ya Spika kuwa ni kweli mawaziri na watendaji kwenda jijini Dar es Salaam kila mara ni kunaiongezea serikali gharama, kutokana na fedha wanazotumia ambazo ni kodi ya wananchi.

Kimsingi, yapo maeneo mengi ambayo yanahitaji kuboreshwa, kuanzia kwenye miundombinu ya afya, elimu, maji, barabara na kwingine ili Watanzania  waweze kupata huduma bora.

Hivyo, tunadhani kuna haja kwa viongozi hao kuipunguzia serikali mzigo kwa kufanya shughuli za kiserikali wakiwa makao makuu ya nchi badala ya kusafiri hadi jijini Dar es Salaam, hali ambayo inachangia kuongeza gharama zisizo za lazima.

Kama ambavyo serikali iliamua kuhamia Dodoma, basi tunaona ni vyema shughuli zote ziwe zinafanyikia kwenye makao makuu ya nchi, lakini kwa Dar es Salaam iwe kwa ulazima.

Tunaamini kwamba, njia hiyo itasaidia kuipunguzia serikali gharama ili fedha ambazo zingetumiwa na mawaziri na watendaji hao katika safari za Dar es Salaam, zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo na huduma kwa wananchi.

Si kwamba mawaziri na watendaji wasiende Dar es Salaam, bali kuwe na jambo maalum ambalo linawalazimu kufanyia nje ya Dodoma, lakini vinginevyo, tunadhani ni muhimu kila kitu kuishia makao makuu ya nchi.

Ushauri wetu unabaki kwenye umuhimu wa kubana matumizi ili fedha ambazo zingetumika kwenye safari hizo za viongozi, zielekezwe katika shughuli nyingine za maendeleo ya nchi kama ambavyo tumeainisha baadhi yake.

Ni wazi kwamba kwenye safari hizo za kutoka Dodoma hadi Dar es Salaam, kuna kulipwa posho za kulala, mafuta, lakini pia vipuri vya magari vinachakaa, hali ambayo inasababisha kuwapo kwa matumizi ya fedha.

Lakini tunaamini kwamba, matumizi hayo yanaweza kubanwa iwapo viongozi wataona umuhimu wa kufanyia mikutano, makongamano na vikao kwenye makao makuu ya nchi ambayo yako Dodoma.

Kadhalika, kuna uwezekano wa kufanya mikutano mingine kwa njia ya mtandao kama ambavyo imekuwa ikifanyika ikiwa tahadhari ya kujiepusha na maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19.

Tunatarajia kuona tabia hiyo inadhibitiwa, ikizingatiwa kuwa Spika Ndugai alilielekeza angalizo hilo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ambaye anaratibu shughuli za serikali za kila siku. Vinginevyo, uamuzi wa Dodoma kuwa makao makuu ya nchi na serikali hautakuwa na maana.