Siasa ziepukwe sasa kuijenga Taifa Stars

29Jun 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Siasa ziepukwe sasa kuijenga Taifa Stars

TIMU ya Taifa ya Soka ya Tanzania, 'Taifa Stars' imeendelea kufanya vibaya kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 nchini Misri, baada ya juzi kupoteza mechi yake ya pili mfululizo kwenye hatua ya makundi.

Stars ambayo ipo Kundi C pamoja na Algeria, Senegal na majira zao, Kenya, hii ni mara ya kwanza kushiriki michuano hiyo ya Afcon katika kipindi cha miaka 39, ikiwa ni tangu iliposhiriki fainali za Nigeria mwaka 1980.

Katika mechi yake ya kwanza kwenye michuano hiyo, Taifa Stars ilikubali kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Senegal kabla ya juzi kuchapwa 3-2 dhidi ya Kenya ('Harambee Stars).

Matokeo hayo yanaifanya Stars kuburuza mkia katika kundi lake, hivyo ni wazi sasa inasubiri tu kukamilisha ratiba kwa kucheza dhidi ya Algeria Julai Mosi, mwaka huu kabla ya kukwea pipa kurejea nyumbani kuendelea na taratibu nyingine.

Hata hivyo, mbali na maandalizi ya Stars ambayo hayakuwa ya kuvutia lakini kumekuwapo na mihemko mikubwa kutoka makundi mbalimbali hususan ya kisiasa zaidi, ambayo kila moja limekuwa na hoja zake kuhusu timu hiyo baada ya kupoteza mechi zake za awali.

Kwa ujumla maoni yanayotolewa huku kila moja likivutia upande wake, yamekuwa si ya kujenga kwa wakati huu ambao wachezaji wa Taifa Stars walikuwa wanapaswa kujengwa kisaikolojia zaidi kuliko tuhuma mbalimbali ambazo zimekuwa zikielekezwa kwao pamoja na benchi zima la ufundi.

Maoni mbalimbali yalianza kutolewa kutoka kwa wabunge, na wengi wakionyesha wazi kutomkubali Kocha Mkuu wa Stars, Mnigeria Emmanuel Amunike na wengine wakionyesha kutoridhishwa na kikosi anachokipanga, hayakuwa ya kuijenga timu hiyo kwani yalitolewa mara tu baada ya kupoteza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Senegal wakati wakihitaji faraja kipindi hicho.

Aidha, wapo baadhi ya viongozi walioonyesha kuvutia upande wao zaidi kwa kuwatia moyo wachezaji huku wakiamini hamasa yao inaweza kuleta ushindi kwa Stars kuelekea mchezo wake wa pili dhidi ya Kenya.

Ni kweli kabisa Stars ilihitaji hamasa ya aina hiyo kwa kuungwa mkono kwa kila hatua hata pale ilipoonekana kufanya vibaya, lakini kama Watanzania, haikustahili kuanza kugawanyika makundi mawili na kila moja kuvutia upande wake wakati huu 'askari wetu hao wakiwa vitani'.

Sisi Nipashe daima tunaamini umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, hivyo moja kwa moja waliozidi kuitia udhaifu Stars ni Watanzania wenyewe hususan baadhi ya wabunge na wadau wengine wa soka walioanza kumkosoa hadharani kocha pamoja na baadhi ya wachezaji wake.

Wenzetu Kenya, walitumia wachezaji wa zamani wa timu hiyo ya taifa akiwamo McDonald Mariga kwenda kuwahamasisha Harambee Stars, lakini Tanzania imekuwa ikitanguliza siasa mbele hata pale ambapo wanasiasa walipaswa kubaki kama washangiliaji na wawezeshaji kifedha tu kwa timu hiyo.

Tunaamini mchezaji mkongwe anapopewa fursa ya kwenda kuwahamasisha wachezaji, kuna kitu kikubwa wanaweza kujifunza kutoka kwake kuliko namna ambavyo wanasiasa na viongozi mbalimbali wa serikali wamekuwa mstari wa mbele zaidi kwenda moja kwa moja kuzungumza na wachezaji.

Hatulipingi hilo, lakini linapaswa kufanyika kwa umoja na ushirikiano mkubwa kuliko kama inavyoendelea katika timu ya taifa na kila mmoja akitaka kuitumia kama daraja la kujipatia umaarufu wakati Watanzania wanataka mafanikio kisoka.

Tunaona ipo haja sasa wanasiasa na viongozi wengine wa serikali kuacha kuitumia Stars kama daraja lao la kujipatia umaarufu kisiasa kwa kuwa tunafahamu fika wengi hutumia mlango wa soka kujipatia wafuasi wengi kutoka katika mchezo huo unaoongoza kwa kuwa na mashabiki wengi duniani.

Ikumbukwe Watanzania wanalipenda sana soka, lakini linaonekana kutowapenda kutokana na baadhi ya viongozi wachache wanaotumia kama mlango wa kujipatia mafanikio binafsi badala ya kuumiza kichwa ni namna gani tunaweza kuliinua kutoka hapa lilipo sasa.

Tayari Stars, imepoteza nafasi Afcon, hivyo makundi ya kisiasa yaliyojitokeza ni vema sasa kumulika na kutoa michango yao hususan ya kifedha ili kuijenga kuelekea michuano ijayo badala ya kuanza kuvutana na kutafuta mchawi aliyechangia kushindwa kupata mafanikio nchini Misri.

Habari Kubwa