Siku 100 za Rais Magufuli matumaini makubwa

14Feb 2016
Mhariri
Nipashe Jumapili
Siku 100 za Rais Magufuli matumaini makubwa

Kumekuwa na shauku kubwa ya wananchi kujua kilichofanywa na Serikali hii ya awamu ya tano katika siku zake 100 za mwanzo, ni shauku ya haki ambayo wananchi wengi waliotarajia mabadiliko ya uongozi nchini wapate tathmini ya kuelewa mwelekeo wa mabadiliko yenye matumaini kiuchumi.

Yapo mambo ya msingi ambayo yamefanyika katika kipindi cha tangu Serikali hii iingie madarakani, na kila Mtanzania amejionea kwa dhahiri na kukiri kuwa dhamira ya Serikali ya Rais Magufli ni ya kweli ya kutaka kuwaondolea wananchi wengi adha zitokanazo na hali ya umaskini inayowakabili.

Tunapoangalia mafanikio hayo, tunaiangalia Serikali yote ikiwa ni pamoja na utendaji wa safu ya uongozi alioiteua Rais mwenyewe ambayo ndiyo itakayowapa ushawishi Watanzania kuwa mwelekeo wa utawala uliopo utaweza kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kati.

Baadhi ya makundi ya kijamii pamoja na wasomi wa kada mbalimbali wameshayataja mafanikio mengi yaliyopatikana katika kipindi cha siku 100 za uongozi wa Serikali ya awamu ya tano, na lililotawala zaidi ni la Rais pamoja na viongozi wengine kuendelea kupambana na rushwa, ufisadi, ubadhirifu pamoja na uzembe katika maeneo yote ya kazi.

Watanzania wanahitaji maisha bora katika huduma za afya, elimu, miundombinu mbalimnali pamoja na uhuru wa kufanya shughuli za uzalishaji kwa uhuru na usalama ili kujikimu bila bughudha.

Tumeshuhudia mawaziri wakizunguka kila mahali ili kutatua matatizo yanayowakabili wananchi huko mikoani, na kwa sehemu kubwa wananchi wanaonyesha dalili za wazi kuukubali uongozi wa Serikali hii inayotekeleza ahadi iliyoziweka wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

Tunaamini kuwa kwa kauli za Rais Magufuli, matendo na dhamira yake, katika siku hizi 100 tangu aingie madarakani, wananchi wengi wamemwelewa, wamemkubali na wanamwamini, na katika kipindi hicho Rais Magufuli amewathibitishia Watanzania kuwa yeye ni kiongozi, mwenye sifa muhimu za uongozi.

Tunaamini kuwa kiongozi bora lazima awe na dira, maono na malengo kuhusu anakotaka Taifa liende, na pia lazima kuwe na mkakati wa kutekeleza dira na maono yake kabla ya kufikia lengo.

Katika siku 100 za kwanza Rais Magufuli amedhihirisha anayo sifa hiyo. Kiongozi bora anajua na haogopi kuweka vipaumbele na mpangilio wake wa utekelezaji na kuvisimamia, katika hizi siku 100 Rais Magufuli amethibitisha anayo sifa hiyo muhimu ya uongozi.

Kiongozi bora haogopi kufanya maamuzi magumu, hakuna mwenye shaka kuwa katika hizi siku 100, Rais wetu amedhihirisha kwa kauli na kwa vitendo kuwa, anapotetea maslahi ya Taifa na wananchi, haogopi kufanya na kusimamia maamuzi magumu.

Ingawa siku 100 hazitoshi kutekeleza kila ahadi iliyotolewa wakati wa kampeni za uchaguzi, tunaamini kila jambo litatekelezwa kwa awamu, masuala ya ajira kwa vijana pamoja na uanzishaji na uendelezaji wa viwanda pia ni mkakati unaohitaji muda wa kutosha.

Tunaamini kuwa Watanzania wanayo matarajio makubwa ya mabadiliko ya kiuchumi kutokana na ukweli kwamba Serikali imedhamiria kukusanya kodi pamoja na mapato mengine kutoka vyanzo mbalimbali ili fedha hizo zisaidie kuanzisha na kuendeleza viwanda na miradi mingine ya maendeleo.

Kasi hii ya ukusanyaji mapato ya Serikali iendelee kwa nguvu hii hii ili mabadiliko ya kweli yaweze kufikiwa kwa wakati uliopangwa, maendeleo ya nchi ni kuwabadili wananchi wake kuishi katika maisha bora zaidi.

Habari Kubwa