Simba inaweza, tuishangilie mwanzo mwisho Taifa kesho

11Feb 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Simba inaweza, tuishangilie mwanzo mwisho Taifa kesho

KESHO mabingwa wa Tanzania Bara na wawakilishi pekee wa Afrika Mashariki na Kati kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba, watashuka Uwanja wa Taifa kuikaribisha Al Ahly ya Misri kwenye mechi yao ya tatu ya hatua ya makundi na ya pili kwa timu hiyo kucheza nyumbani.

Simba ambayo iko Kundi D, ambalo mbali na Al Ahly pia linazijumuisha AS Vita ya DR Congo na JS Saoura ya Algeria, hadi sasa ina pointi tatu tu baada ya kushuka dimbani mara tatu. Pointi hizo tatu Simba ilizipata katika mechi yake ya kwanza nyumbani dhidi ya JS Saoura.

Baada ya ushindi huo, kilichofuata kwa Simba ilikuwa ni aibu kubwa kufuatia kukubali vipigo viwili vikubwa ugenini.

Ikiwa ugenini DR Congo dhidi ya AS Vita na kisha Misri dhidi ya Al Ahly, Simba ilikubali kipigo cha mabao 5-0, hivyo kwa mechi hizo mbili tu mabingwa hao wa Tanzania Bara wakajikuta wakiruhusu mabao 10-0.

Hata hivyo, Simba iliyorejea nchini Jumanne iliyopita ikitokea Misri, Alhamisi iliyopita ilirejesha hamasa kwa mashabiki wake baada ya kupata ushindi wa mabao 3-0 kwenye mechi ya Ligi Kuu dhidi Mwadui FC.

Hivyo, tunaamini ushindi huo si tu umerejesha hamasa kwa mashabiki bali pia utakuwa umeamsha morali kwa wachezaji kuelekea kuivaa Al Ahly.

Ingawa pia baada ya Al Ahly kuichapa Simba kwa mabao 5-0, iliendeleza kasi yake ya kushinda kwenye Ligi Kuu Misri kwa kuichapa ENPPI mabao 2-1 ikiwa ugenini na kisha kuibuka na ushindi wa bao 1-0 nyumbani dhidi ya El Hodood, hilo halitutii hofu hasa tukizingatia Simba itakuwa nyumbani mbele ya mashabiki wake.

Ni ukweli usiopingika kuwa Al Ahly inauwezo mkubwa sana na inaizidi Simba kwa kila kitu ukianzia soka, miundombinu hadi kiuchumi, lakini tunaamini wawakilishi hao wa Tanzania hawatakubali kufanya makosa nyumbani.

Kama Simba ilionyesha kiwango cha juu nyumbani na kufanikiwa kushinda kwa mabao 3-0 dhidi ya JS Saoura ambayo nusura iwachape Al Ahly kama si kuchomoa katika dakika ya 86 nchini Algeria, kwa nini wawakilishi hao wa Tanzania washindwe kushinda?

Tunakubali hicho hakiwezi kuwa kigezo cha Simba kushinda, lakini kwa kuzingatia hilo na maandalizi ya kina kulingana na mpinzani wanayecheza naye tena nyumbani mbele ya mashabiki wao, ushindi unawezekana.

Kinachotakiwa ni wachezaji kujengwa kisaikolojia wakiaminishwa inawezekana, huku Kocha Patrick Aussems akirekebisha makosa yaliyojitokeza katika kikosi chake hususan safu ya ulinizi jambo ambalo tunaamini ameshalifanyia kazi.

Lakini pamoja na hayo yote, tunawakumbusha mashabiki kutambua kuwa wao ni mchezaji wa 12 hususan pale timu inapocheza uwanja wake wa nyumbani, hivyo waitumie fursa hiyo wakati huu uongozi wa Simba ukiwa umeshusha kiingilio na kuwa Sh. 2,000 ili kuwafanya Watanzania wengi kujitokeza kuishangilia.

Kwa kulitambua hilo hawana budi kusahau vipigo vilivyopita na kuhudhuria kwa wingi uwanjani kama si kuujaza kabisa Uwanja wa Taifa kuisapoti Simba mwanzo mwisho.

Sote tulishuhudia namna mashabiki 10,000 tu walioruhusiwa kuhudhuria mechi ya Al Ahly na Simba nchini Misri, walivyoishangilia timu yao mwanzo mwisho kama vile wapo 80,000. Ni wakati wa wadau wote wa soka na Watanzania kwa ujumla kuweka kando itikati zao za kiklabu na kwenda kuiunga mkono Simba kwa kuwa inaiwakilisha nchi.

Bendera inayopeperusha si ya Simba, bali ni ya Tanzania, hivyo ni wakati wakuweka kando Usimba na Uyanga ili kwenda kuishangilia Simba ambayo ipo katika nafasi ya tatu kwenye kundi hilo ambalo linaongozwa na Al Ahly ikiwa na pointi saba ikifuatiwa na AS Vita yenye alama nne na JS Saoura ikiburuza mkia kwa alama mbili. Kila la Kheri Simba.

Habari Kubwa