Simba, itumie vizuri Mapinduzi kujiandaa

05Jan 2019
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Simba, itumie vizuri Mapinduzi kujiandaa

KIKOSI cha Simba na benchi lake la ufundi wapo Zanzibar wanaposhiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi lililoanza wiki hii visiwani humo.

Michuano hii ni ya kila mwaka ambapo inashirikisha timu kutoka Tanzania Bara, Zanzibar pamoja na timu mualikwa kutoka nje ya Tanzania ambaye huwa anakuja kunogesha michuano hiyo.

Kwa mwaka huu Simba imeenda kwenye michuano hiyo ikiwa inashiri Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo imetinga hatua ya makundi.

Simba itaanza hatua hiyo kwa kucheza nyumbani dhidi ya timu ya JS Saoura ya Algeria mchezo utakaochezwa Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Awali mashabiki wa timu hiyo na wadau wa soka walitegemea Simba wangepeleka kikosi cha pili kwenye michuano hiyo kama ilivyofanya Yanga.

Hata hivyo kocha wa Simba, Patrick Aussems, wakati mashabiki wakiwaza hivyo yeye alikuwa na mawazo mengine tofauti kwa kuamua kupeleka kikosi kizima kwenye michuano hiyo ya Mapinduzi.

Kimsingi alichokifanya Aussems ni kitendo kizuri kitakachoisaidia Simba kuelekea kwenye mchezo huo dhidi ya JS Saoura ambapo imebaki wiki moja kabla ya kukutana.

Nipashe, tunaamini Aussems anachotegemea kukivuna kwa kupeleka kikosi cha kwanza kwenye michuano ya Mapinduzi huku zikiwa zimebaki siku chache kufanyika pambano lao la ligi ya Mabingwa Afrika.

Nipashe, tunaamini kama Aussems atatumia vyema michuano hii na kuwa na siku chache za kujiandaa anaweza akapata matokeo mazuri kwenye mchezo dhidi ya JS Saoura.

Kikubwa ni kuangalia nini anakitaka kutoka kwa wachezaji wake, michuano ya Mapinduzi inaweza kuwa sehemu ya maandalizi ya Simba kuelekea kwenye mchezo huo wa ligi ya mabingwa Afrika.

Tayari kocha Aussems, ameweka wazi kikosi chake cha kwanza kitarejea Dare s Salaam kabla ya kumalizika kwa michuano hiyo hata kama Simba itasongo mbele kuingia hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

Sio maamuzi mabaya kwa Aussems kuipeleka kikosi kizima kwa kuwa inategemea na ratiba na program ya kocha Aussems kabla ya kuvaana na Waalgeria hao.

Nipashe tunakumbusha, Simba ni wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano hiyo ya Afrika, hivyo kila Mtanzania kwa Utanzania wake angependa kuona wawakilishi hao wanasonga mbele na kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Lakini bila maandalizi ya nguvu na mipango mizuri ni ngumu kufikia hatua hiyo, na hilo kocha Aussems analitambua na ndio maana ameonelea kushiriki sehemu ya michuano hiyo kwa kikosi chake cha kwanza ili kuwa kama mazoezi kwao.

Nipashe tunawakumbusha Simba, timu walizopangiwa kundi moja si timu za kuzibeza, ni timu kubwa na zenye uzoefu kwenye michuano ya CAF kwa ngazi za vilabu, umakini na utulivu huku kukiwa na mipango madhubuti ya ndani na nje ya uwanja inatakiwa kuweza kufanya vizuri kwenye kundi lao.

Nipashe hatuna shaka, Simba inafanya maandalizi mazuri kwa kuwa uongozi, wachezaji na benchi la ufundi unatambua ukubwa wa michauno ya Afrika.

Habari Kubwa