Simba jipangeni CAF, Kaizer Chiefs si wepesi

03May 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Simba jipangeni CAF, Kaizer Chiefs si wepesi

WAWAKILISHI pekee wa Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba, tayari wamefahamu wapinzani wao katika hatua ya robo fainali inayotarajiwa kupigwa kati ya Mei 14-15, kabla ya kurudiana Mei 21-22, mwaka huu, ambapo itaanzia ugenini dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Tangu kupangwa kwa droo hiyo mashabiki, wanachama na hata baadhi ya viongozi wa Simba wameipokea kwa mikono miwili huku wakiweka wazi kuwa safari ya kutinga nusu fainali ya michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), ni nyepesi kwao.

Simba ambayo kama ikivuka hatua hiyo itakutana na mshindi kati ya Wydad Casablanca ya Morocco ama MC Alger ya Algeria, wanaona droo hiyo imekuwa nyepesi na ingekuwa ngumu zaidi kwao endapo wangeangukia kwa timu kutoka Afrika Kaskazini (Uarabuni) MC Alger ama CR Belouizdad za Algeria.

Uongozi wa Simba, mbali ya kuwaona Kaizer Chiefs ni wepesi kwao kutokana na tamaduni za Afrika Kusini kutotofautiana sana na Afrika Mashariki hususan upande wa 'siasa' za soka, lakini kutawapunguzia usumbufu wa kusafiri umbali mrefu.

Hata hivyo, kwenye hatua ya makundi, Kaizer Chiefs imepenya kutokana na kanuni ya 'Head to Head' (matokeo zilipokutana) dhidi ya Horoya FC ya Guinea kutokana na timu hizo kila moja kumaliza na pointi tisa nyuma ya vinara wa Kundi lao la C, Wydad Casablanca waliohitimisha kileleni na pointi zake 13, huku Petro de Luanda ikiburuza mkia na alama yake moja.

Katika mechi zake sita za hatua za makundi, Kaizer Chiefs imeshinda mbili, sare tatu na kupoteza mchezo mmoja, huku ikifunga mabao matano tu na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita.

Lakini kama ni kitakwimu, Simba ipo juu zaidi kwani imeongoza Kundi lake la A ikiwa na alama 13, lililokuwa likiundwa na bingwa mtetezi wa michuano hiyo, Al Ahly ya Misri iliyomaliza nafasi ya pili na pointi 11, AS Vita ya DR Congo iliyoshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi saba Al-Merrikh ya Sudan iliyoburuza mkia na alama zake mbili.

Hata kwa upande wa takwimu za mabao, Simba ipo juu zaidi ya Kaizer Chiefs kwani yenyewe imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili pekee huku ikizifumania nyavu za wapinzani mara tisa.

Pamoja na takwimu hizo za kuvutia za Simba, hiyo haitoshi kubweteka na kujiaminisha kwamba imepata mpinzani mwepesi katika hatua hiyo, kwani mara nyingine mpira wa miguu una matokeo ya kushangaza hasa unapokwenda na matokeo yako uwanjani na kujiamini kupita kiasi.

Nipashe tunakiri kwa sasa Simba ipo kwenye kiwango cha juu na ni moja ya timu zinazoogopwa katika michuano hiyo, lakini hilo haliwezi kuwa sababu kwao ya kuamini kwamba Kaizer Chiefs watakuwa wepesi na kuacha kujiandaa ipasavyo.

Tunaamini njia pekee ya Simba kufanya vizuri, kwanza ni kufanya maandalizi ya kutosha na kumheshimu mpinzani wake kuelekea mechi hiyo ya robo fainali ambayo ni mtoano.

Ikumbukwe katika hatua ya makundi, pamoja na ubora wa kiwango cha juu wa Wydad Casablanca, ilikubali kipigo cha mabao 4-0 nyumbani dhidi ya Kaizer Chiefs na Jumapili ya Aprili 25, mwaka huu ikawatembezea kichapo cha mabao 2-1 nyumbani kwa majirani zao wa Afrika Kusini, Memelodi Sundowns kwenye mechi ya Ligi Kuu ya nchini humo.

Sote tunafahamu ubora wa Mamelodi katika michuano hiyo ya CAF ambayo nayo imemaliza kileleni mwa msimamo wa Kundi B ikiwa na pointi 13, hivyo kamwe Simba hawapaswi kuichukulia poa Kaizer Chiefs kwani inaweza kujikuta inatoka vichwa chini na wapinzani wao hao kusonga mbele.

Habari Kubwa