Simba kazeni buti bado mna nafasi robo fainali

21Jan 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba kazeni buti bado mna nafasi robo fainali

WAWAKILISHI pekee wa Afrika Mashariki na Kati kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba, juzi walikubali kichapo cha kwanza katika hatua ya makundi wakiwa ugenini DR Congo.

Simba ambayo ipo Kundi D pamoja na Al Ahly ya Misri, JS Saoura ya Algeria na AS Vita, juzi ilikubali kipigo cha aibu cha mabao 5-0 ugenini kutoka kwa timu hiyo ya DR Congo.

Kipigo hicho kimekuja ikitoka kushinda 3-0 dhidi ya JS Saoura katika mechi yake ya kwanza kwenye hatua hiyo ya makundi.

Hata hivyo, kwa soka ililoonyesha Simba kwenye mechi yake ya awali nyumbani, linatupa imani kubwa ya timu hiyo ya mtaa wa Msimbazi jijini Dar as Salaam, kuendelea kufanya vizuri kwenye mechi zijazo.

Sote tunatambua ugumu uliopo katika michuano hii inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), kwa timu kuweza kupata ushindi ugenini, ingawa kipigo cha mabao 5-0 kilikuwa kikubwa mno ukilinganisha na ubora wa Simba wa sasa.

Tumeshuhudia JS Saoura ikichezea kichapo hapa jijini Dar es Salaam kutoka kwa Simba, huku pia AS Vita ikipigwa 2-0 ugenini Misri dhidi ya Al Ahly.

Hivyo matokeo iliyoyapata Simba ugenini dhidi ya AS Vita, si kitu cha kushangaza na wala kukatisha tamaa kwa kuwa hata Brazil iliwahi kuchapwa mabao 7-1 mechi ya nusu fainali ya Kombe la Dunia 2014.

Hivyo katika michuano hii yenye utajiri mkubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika, kikubwa ni Simba kuhakikisha kwanza haifanyi makosa kwenye michezo yake miwili ya nyumbani.

Hata hivyo, kupata ushindi ama sare kwenye mechi zake mbili za ugenini zilizobaki dhidi ya Al Ahly Februari 2, mwaka huu na JS Saoura itakuwa ni hatua moja kubwa katika kujihakikishia nafasi ya kutinga robo fainali ya michuano hiyo.

Tunaamini hilo linawezekana endapo maandalizi ya kina nje na ndani ya uwanja yatafanyika kabla ya Simba kuifuata Al Ahly, lakini kubwa likiwa ni kuwajenga wachezaji kisaikolojia zaidi ili kuwarejesha mchezoni.

Kwa soka la Simba, inalolionyesha ikiwa uwanja wa nyumbani wapinzani wake wote wanatambua ni vigumu kuweza kuambulia angalau pointi moja Uwanja wa Taifa.

Kwa mantiki hiyo, Simba inatakiwa kuhakikisha mechi ijayo inapata pointi ugenini Misri ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kufuzu hatua ya robo fainali.

Hiyo ni kutokana na Al Ahly kulazimisha sare ya bao 1-1 ugenini Algeria dhidi ya JS Saoura, hivyo kushika usukani wa Kundi D ikiwa na pointi nne moja mbele ya AS Vita na Simba.

Nipashe kama wadau wakubwa wa soka, tunaahidi kuendelea kuiunga mkono Simba wakati huu ikibeba jukumu la kuipeperusha bendera ya nchi kimataifa.

Tunaitakia maandalizi mema Simba, wakati huu tukiamini huu ni mwaka wa Tanzania kufanya vizuri kimataifa kuanzia ngazi ya klabu hadi timu za taifa, hasa tukizingatia Serengeti Boys itaiwakilisha nchi kwenye michuano ya Afrika, Afcon U-20 itakayofanyika jijini Dar as Salaam Aprili mwaka huu na wakati huo huo Taifa Stars ikiwa katika nafasi nzuri ya kufuzu Afcon 2019 ya wakubwa.

Habari Kubwa